Kutumia Picha ili Kuwasaidia Wasomaji wa Machapisho Yetu
Machapisho mengi ya Mashahidi wa Yehova yana picha za rangi zinazovutia ambazo zinaambatana na habari inayozungumziwa, hata hivyo haikuwa hivyo zamani. Toleo la kwanza la Zion’s Watch Tower, lililochapishwa mwaka 1879, lilikuwa na picha chache sana. Kwa makumi ya miaka, machapisho yetu yalikuwa na maandishi mengi, na mara mojamoja kukiwa na mchoro au picha ya rangi nyeupe na nyeusi.
Mengi ya machapisho yetu siku hizi yana picha nyingi sana. Wachoraji na wapiga picha wetu wamechora na kupiga picha nyingi sana, na miongoni mwa picha na michoro hiyo ni ile unayoona katika machapisho yetu na tovuti hii. Kufanya utafiti mwingi na wa kina kunasaidia sana ili kupata picha ambazo zinafundisha historia na kweli muhimu za Biblia.
Kwa mfano, fikiria picha inayoonyeshwa katika makala hii, ambayo imetumiwa kwa mara ya kwanza katika sura ya 19 ya kitabu “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu. Hiyo ni picha ya jiji la kale la Korintho. Inalingana na masimulizi yaliyo katika sura ya 18 ya kitabu cha Biblia cha Matendo, mtume Paulo yuko mbele ya be’ma, au kiti cha hukumu. Watafiti waliwapatia wachoraji mambo waliyopata katika ugunduzi wao wa kiakiolojia, mambo yanayohusiana na mahali ambapo kiti hicho kilikuwepo na rangi ya marumaru zilizotumiwa kujenga mahali hapo ambapo huenda ndipo Paulo alifikishwa mbele ya Gallio. Pia, watafiti waliwajulisha kuhusiana na mavazi ya Waroma wa karne ya kwanza ili kwamba liwali Gallio (ambaye amesimama katikati ya picha) achorwe akiwa amevaa mavazi ya kifahari. Akiwa amevaa kanzu ndefu ambayo ina pindo kubwa la zambarau na viatu vinavyoitwa calcei. Pia, watafiti walitaja kuwa Gallio aliposimama be’ma, inaonekana kwamba alielekeza uso wake upande wa kaskazini-magharibi, ili ikiwezekana mchoraji awe na wazo kuhusiana na uelekeo wa mwanga katika picha hiyo.
Kupanga Vizuri na kwa Utaratibu
Tunazipanga picha na kuzihifadhi kwenye faili ili kuzitumia tena kukiwa na uhitaji. Kwa miaka mingi, tulihifadhi michoro kwenye bahasha kubwa, michoro iliyo katika chapisho moja ilihifadhiwa katika bahasha moja. Picha zilihifadhiwa kulingana na habari inayozungumziwa. Kadiri mafaili hayo yalivyoongezeka, ndivyo kutafuta au kuitumia tena picha kulivyoendelea kuwa jambo gumu zaidi.
Mnamo 1991, tulikamilisha kuunda programu ya kompyuta ambayo ingerahisisha sana kazi ya kutafuta michoro na picha hizo, na hivyo kutosheleza mahitaji yetu. Programu hiyo inaitwa Huduma za Mfumo wa Picha, hadi kufikia sasa imehifadhi zaidi ya picha 440,000. Zaidi tu ya picha ambazo tayari zimetumiwa katika machapisho yetu, maelfu ya picha za ziada zimehifadhiwa kwa lengo la kuzitumia katika machapisho yatakayotolewa wakati ujao.
Programu hiyo imerekodi mambo kama vile, lini na mahali ambapo kila picha imetumiwa, jina la kila aina ya picha ambayo imetumiwa, na wakati au tarehe ya picha. Sasa kuna uwezekano wa kutafuta haraka picha zinazofaa kwa ajili ya machapisho mapya yanayoandaliwa.
Nyakati nyingine tunawaomba wamiliki wa picha fulani waturuhusu tutumie picha hususa tunayohitaji. Kwa mfano, labda tunataka picha ya pete au bangili za sayari ya Zohali ili tuitumie kwenye makala fulani katika gazeti la Amkeni! Wasaidizi wetu wanatafuta picha hususa inayofaa na kisha wanawasiliana na mmiliki wa picha hiyo ili kuomba ruhusa ya kuitumia. Baadhi ya wamiliki huturuhusu kutumia picha bila malipo yoyote, kwa sababu wanatambua kazi yetu ya elimu ya Biblia ya ulimwenguni pote. Wengine wanataka tuwalipe kiasi fulani cha pesa au tuonyeshe mahali ambapo tumeitoa picha hiyo. Baada ya kufikia makubaliano, picha hiyo inatumiwa katika chapisho lililokusudiwa na kisha kuingizwa katika programu yetu ya kuhifadhia picha.
Leo, baadhi ya machapisho yetu yamejaa picha. Kwa mfano, katika tovuti hii tuna hadithi za Biblia zilizochorwa; na broshua Msikilize Mungu ambayo ina rangi zinazovutia sana inapatikana kwenye tovuti hii na pia imechapishwa. Broshua hiyo inafundisha mambo muhimu ikitumia maneno machache sana. Machapisho hayo na mengine mengi tunayochapisha na yale yanayopatikana mtandaoni, yote yanazungumzia Biblia.