Awamu ya 9 ya Picha za Uingereza (Septemba 2019 Hadi Februari 2020)
Katika awamu hii ya picha, utaona jinsi ujenzi ulivyokamilishwa katika ofisi mpya ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Uingereza na jinsi wafanyakazi walivyoanza kuhamia katika ofisi hii kati ya Septemba 2019 na Februari 2020.
Septemba 10, 2019—Jengo la Ofisi
Wataalamu wa bustani wakipalilia udongo ili wapande mbegu za majani. Makazi A na B yanaonekana upande wa nyuma.
Septemba 19, 2019—Jengo la Ofisi
Bwawa lililochimbuliwa lililo mbele ya jengo la ofisi. Bwawa hili ni sehemu ya mfumo uliobuniwa wa kutoa maji taka katika eneo la Chelmsford unaofaana vizuri na mfumo wa asili uliopo. Mfumo huu unasaidia kusafisha maji, unapunguza uwezekano wa mafuriko na unaboresha mazingira ya wanadamu na wanyama.
Septemba 19, 2019—Jengo la Ofisi
Mume na mke mafundi seremala wakiunganisha mbao zitakazotumika kutenganisha ofisi moja na nyingine.
Oktoba 14, 2019—Makazi A
Mfanyakazi wa kikosi cha useremala akibandika alama ya chumba cha kutengeneza nywele kwa kutumia kifaa maalumu.
Oktoba 28, 2019—Eneo la Tawi
Seremala akiweka alama za njiani kwa kutumia kifaa maalumu. Alama hizo zinawaongoza wakazi na wageni wanatembelea eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 34.
Novemba 4, 2019—Jengo la Kaskazini la Utayarishaji
Mwakilishi wa idara ya zimamoto akipima nguvu ya maji kwenye bomba linalotumika kuzima moto.
Novemba 14, 2019—Jengo la Ofisi
Mshiriki wa Halmashauri ya Mradi wa Ujenzi akiongoza ibada ya asubuhi iliyorushwa kupitia mfumo mpya wa ofisi ya tawi. Programu hii ilionyeshwa pia kwa familia ya Betheli iliyopo London.
Novemba 19, 2019—Jengo la Kaskazini la Utayarishaji
Fundi umeme akiweka taa ya barabarani kwenye mwingilio wa eneo kwa ajili ya watu walioruhusiwa tu.
Novemba 19, 2019—Eneo la kutegemeza ujenzi
Wafanyakazi wakitoa nyaya za shaba ili zitumiwe tena.
Novemba 25, 2019—Eneo la kutegemeza ujenzi
Ndugu anayetembeza wageni katika Kituo cha Wageni akielezea muundo wa eneo la ujenzi. Wageni zaidi ya 95,000 walitembelea ofisi hii ilipokuwa ikijengwa.
Desemba 5, 2019—Jengo la Ofisi
Mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Uingereza akizungumza na kikosi cha ujenzi katika mkutano wa mwisho wa kila mwezi kabla idara za Betheli hazijakabidhiwa majengo hayo. Zaidi ya wafanyakazi 11,000 walijitolea nguvu na wakati wao ili kushiriki katika mradi huu.
Desemba 10, 2019—Jengo la Kaskazini la Utayarishaji
Timu ya Watayarishaji wa Video na Idara ya Utangazaji wamezoezwa kutumia vifaa vya studio mpya. Wafanyakazi wengi huvaa viatu vya bluu vinavyovaliwa juu ya viatu vingine ili kulinda sehemu zilizomalizwa kujengwa.
Desemba 30, 2019—Jengo la Ofisi
Wafanyakazi wakifagia mchanga uliobaki katikati ya matofali madogo katika barabara ya magari inayoelekea kwenye Jengo la Ofisi.
Januari 16, 2020—Jengo la Kusini la Utayarishaji
Fundi wa magari akitengeneza basi dogo katika gereji mpya. Kwa kuwa majengo yote ya tawi yako katika eneo moja, familia ya Betheli haitahitaji kuwa na mabasi mengi ya kusafiri ili kwenda kazini kila siku. Magari hayo ya ziada sasa yatauzwa. Kwa nyuma kuna gari dogo la kubebea mizigo linalotumiwa na kikosi cha Udumishaji wa Eneo.
Januari 29, 2020—Makazi D
Ndugu wakishusha mizigo ya Mwanabetheli. Kikundi cha watu 27 kiliwasaidia Wanabetheli kuhama kati ya mwezi wa Januari na Februari. Kufikia mwanzoni mwa mwezi Machi, familia nzima ya Betheli ilikuwa ikiishi na kufanya kazi katika ofisi ya tawi mpya.
Februari 6, 2020—Jengo la Ofisi
Wapishi wakiandaa kachumbari kwa ajili ya familia ya Betheli.
Februari 7, 2020—Eneo la Kutegemeza Makazi
Makao ya muda yakiondolewa baada ya kuuzwa. Ujenzi ulipokuwa ukiendelea, makao haya yaliwasaidia wafanyakazi waishi karibu na eneo jipya la ofisi ya tawi. Makao ya aina hiyo yalitumiwa kwa kusudi la kupunguza kiasi cha gesi ya kaboni katika mradi huo. Mradi huo ulivutia kituo kinachojulikana cha uchunguzi kinachosimamia kiwango cha ubora wa miradi ya ujenzi kinachoitwa BREEAM. Upande wa nyuma kuna majengo mapya ya makazi.
Februari 14, 2020—Jengo la Ofisi
Wafanyakazi wa idara ya utafsiri wakiweka chumba cha kurekodi sauti. Studio hii hutumiwa badala ya mfumo wa kurekodi sauti ambao kila timu ya utafsiri hupewa na hutumiwa ili kurekodi machapisho ya lugha za asili za vikundi vya utafsiri vilivyo chini ya ofisi ya tawi ya Uingereza kama vile Ireland na Scotland.
Februari 24, 2020—Jengo la Ofisi
Ndugu aliye katika Idara ya Usanifu-Majengo na Ujenzi akizungumza na mwakilishi wa shambani aliye kusini mashariki mwa Uingereza kupitia video. Wawakilishi wa shambani huzungumza kwa ukawaida na ofisi ya tawi ili kujadili kuhusu ujenzi na udumishaji wa Majumba ya Ufalme. Upande wa nyuma, ndugu na dada wengine wanajadili jinsi ya kuhakikisha Majumba ya Ufalme mapya na yanayokarabatiwa yanavyoweza kuwa na joto na hewa ya kutosha.
Februari 25, 2020—Jengo la Ofisi
Wajitoleaji wapya wakiwa mapokezi kabla ya kuhudhuria mkutano wa kuwakaribisha na kisha kuambiwa idara watakazofanya kazi. Ofisi ya tawi ya Uingereza ilipohamia katika eneo la Chelmsford, wajitoleaji zaidi ya 500 walikuwa wamefanya kazi pamoja na Wanabetheli. Upande wa nyuma, mafundi wanajaribu na kuweka vizuri televisheni zitakazotumiwa kama sehemu ya maonyesho kwa wageni watakaotembelea.