Awamu ya 1 ya Picha za Warwick (Mei Hadi Agosti 2014)
Mashahidi wa Yehova wanajenga majengo mapya yatakayotumiwa kama makao makuu ya ulimwenguni pote katika mji wa Warwick, New York. Kuanzia Mei hadi Agosti 2014, wajenzi walipiga hatua kubwa katika kujenga Jengo la Gereji, Jengo la Ofisi za Usimamizi na Huduma, na majengo C na D ya makazi. Picha zifuatazo zinaonyesha baadhi ya kazi ambazo zilifanywa katika kipindi hicho chenye shughuli nyingi.
Mei 1, 2014—Eneo la Ujenzi la Warwick
Picha imepigwa upande wa kusini magharibi, kutazama kaskazini kutoka juu ya Ziwa la Sterling Forest (Ziwa la Blue Lake). Mbele, kazi inaendelea kwenye vyumba vya chini vya jengo la makazi D. Karibu na ziwa, kuta za saruji zinatayarishwa kwa ajili ya jengo la makazi C.
Mei 14, 2014—Kituo cha kuunganisha vifaa nje ya eneo la ujenzi
Wafanyakazi wakiunganisha bafu litakalotumiwa kwenye majengo ya makazi ambalo linafanana na dimbwi. Linatia ndani fremu, ukuta wa mbao, mfumo wa kupitisha maji, umeme, na hewa, na beseni kubwa la kuogea. Bafu hilo litakamilika baada ya dimbwi hilo kuunganishwa ndani ya jengo.
Mei 22, 2014—Jengo la Gereji
Mafundi bomba wakiwa kazini kwenye vyumba vya chini ya ardhi. Mradi unapokuwa ukiendelea eneo hili litatumika kama chumba cha kulia cha watu 500 hivi, na maeneo mengine katika jengo yatatumiwa na watu wengine 300. Mradi utakapokaribia kwisha, vyumba hivi vya kulia vya muda vitaondolewa, na jengo litakamilishwa ili kutumiwa kama jengo la kudumisha magari.
Juni 2, 2014—Jengo la Gereji
Kikundi cha watu kikitawanya udongo juu ya paa uliotengenezwa kwa njia ya pekee ili kupanda mimea. Paa lililopandwa mimea husaidia mazingira kwa kupunguza matumizi ya nishati, kupunguza kasi ya maji ya mvua yanayoanguka kutoka katika paa, na kuchuja uchafu kutoka katika maji hayo.
Juni 5, 2014—Jengo la Ofisi za Usimamizi/Huduma
Jengo hili litatia ndani majengo matatu yaliyounganishwa yenye upana wa mita 42,000 za mraba. Wajenzi ambao si Mashahidi wa Yehova watajenga nguzo za chuma za kushikilia majengo hayo.
Juni 18, 2014—Jengo la Udumishaji wa Magari
Wafanyakazi wakitumia gesi kuweka paa la lami. Kamba za usalama zinawashikilia ili wasianguke.
Juni 24, 2014—Jengo la Makazi C
Mifereji (mabomba) ya mfumo wa kusambaza hewa iliyounganishwa mapema inawekwa kwenye jengo. Asilimia 35 hivi ya Mashahidi wanaofanya kazi kwenye mradi wa Warwick ni wanawake.
Julai 11, 2014—Mji wa Montgomery, New York
Majengo haya, ambayo yanatumiwa kama bohari na kituo cha kuunganisha vifaa vya ujenzi, yalinunuliwa Februari 2014 ili kutegemeza mradi huo. Yana nafasi ya mita 20,000 za mraba. Vitu vyeupe vinavyoonekana upande wa juu kulia katika picha ni vigae vya bafu vilivyo tayari kusafirishwa.
Julai 24, 2014—Jengo la Makazi C
Katika picha hii, tunaona upande wa kaskazini mashariki wa jengo hilo. Jengo hili litatumiwa na wafanyakazi 200 hivi wa makao makuu. Vyumba vingi kati ya hivyo vitakuwa na ukubwa wa kati ya mita 30 na 55 za mraba na vitakuwa na jiko dogo, bafu, na baraza dogo.
Julai 25, 2014—Jengo la Udumishaji/Maegesho ya Magari ya Wenyeji
Kutayarisha eneo kwa ajili ya ujenzi. Upande wa juu kushoto, mashine ya kuvunja mawe inavunja mawe ambayo yatatumiwa baadaye kwenye mradi huu. Kufikia mwisho wa mradi huu, mita 260,000 za mchemraba za udongo zitakuwa zimeondolewa kwenye eneo la ujenzi la Warwick. Kwa wastani lori 23 zinatumiwa kila siku.
Julai 30, 2014—Jengo la Udumishaji wa Magari
Mimea ikipandwa juu ya paa.
Agosti 8, 2014—Eneo la Ujenzi la Warwick
Picha iliyopigwa kutoka juu ya kreni, inayoonyesha upande wa kusini magharibi kutoka juu ya jengo la ofisi. Upande wa chini kushoto ni Jengo lililokamilika la Maegesho ya Magari ya Wageni, ambalo linajaa kila siku gari za wafanyakazi. Baadhi ya Mashahidi wamesafiri umbali wa saa 12 ili kufanya kazi ya kujitolea kwa siku tatu au nne tu.
Agosti 13, 2014—Jengo la Udumishaji wa Magari
Kazi inakaribia kwisha kwenye chumba cha kulia cha muda. Mfumo wa video (haujaunganishwa bado) na vikuza sauti vitakavyowekwa kwenye dari vitawezesha wafanyakazi kuunganishwa na ofisi ya tawi ya Marekani kwa ajili ya ibada ya asubuhi na programu nyingine za kiroho.
Agosti 14, 2014—Jengo la Ofisi za Usimamizi/Huduma Mbalimbali
Zege ikimwagwa katika jengo. Kulia, mfanyakazi akitumia mashine ya kushindilia zege ili kuhakikisha hakuna nafasi inayobaki katikati na kuhakikisha kwamba imeshindiliwa vizuri.
Agosti 14, 2014—Jengo la Ofisi za Usimamizi/Huduma Mbalimbali
Mifereji (mabomba) ya kupitisha nyaya za umeme katikati ya jengo, ikiwa tayari kufunikwa na zege itakayofunika chumba cha chini ya ardhi cha jengo hilo.
Agosti 14, 2014—Jengo la Ofisi za Usimamizi/Huduma Mbalimbali
Kumwagwa kwa zege kunakaribia kwisha. Ilikuwa ndiyo zege nyingi zaidi kuwahi kumwagwa tangu kuanza kwa mradi wa Warwick hadi sasa, yenye mita 540 za mchemraba. Zege hiyo ilitayarishwa kwenye kituo kilichotengwa ndani ya eneo la ujenzi, na ilibebwa na malori nane na pampu mbili za kupampu zege, na yaliimwaga kwa saa 5 1/2. Katikati ya picha ni ngazi mojawapo za jengo hilo.
Agosti 14, 2014—Jengo la Makazi C
Kujenga ukingo kwenye paa. Nyuma, ujenzi unaendelea kwenye chumba cha chini cha jengo la makazi A.
Agosti 15, 2014—Jengo la Makazi C
Bafu lililokamilika likiinuliwa kwa kreni hadi kwenye orofa ya tatu. Mradi wa Warwick umetumia kwa wingi sehemu zilizounganishwa mapema, na hivyo kupunguza msongamano katika eneo la ujenzi na kuongeza kasi ya kazi pia.
Agosti 20, 2014—Jengo la Makazi C
Mwanakandarasi akisimamisha ukuta uliounganishwa mapema na unaohifadhi nishati. Saruji ya ukuta ilichanganywa na rangi, hivyo hauhitaji kupakwa rangi au kufanyiwa udumishaji mara nyingi. Kuta hizo zinawekwa haraka, na hilo litasaidia kumalizia mradi huo kwa wakati.
Agosti 31, 2014—Eneo la Ujenzi la Warwick
Picha kutoka upande wa kusini magharibi. Mbele, maandalizi ya kumwaga zege kwenye orofa nyingine ya jengo la makazi D; nyuma yake, jengo la makazi C linakaribia kwisha.