Awamu ya 4 ya Picha za Ujenzi, Uingereza (Machi Hadi Agosti 2017)
Katika mfululizo huu wa picha, ona maendeleo yaliyofanywa kwenye ujenzi wa ofisi mpya ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Uingereza kuanzia mwezi wa Machi na Agosti 2017.
Machi 28, 2017—Eneo la ofisi ya tawi
Akitumia kreni, mwanakandarasi anapandisha chumba chenye kioo mbele. Chumba hicho kitainuliwa juu na kutumiwa kutazama eneo la ujenzi kutoka mahali salama. Kituo cha wageni na sehemu hiyo ya kutazama eneo la ujenzi ilifunguliwa kwa mara ya kwanza mwezi wa Mei 2017, na kufikia Agosti wageni zaidi ya 17,000 walikuwa wametuma taarifa za kuomba kutembelea eneo la ujenzi.
Machi 29, 2017—Jengo la Makazi F
Wanakandarasi wanatumia kreni kuhamisha meza ya saruji iliyounganishwa awali kuipeleka kwenye Jengo la Makazi F, jengo la kwanza la makazi kujengwa. Kwa sababu kuna nafasi ya kutosha kuzunguka majengo, meza hizo zinaweza kuhamishwa haraka bila sehemu zake kutenganishwa.
Aprili 7, 2017—Makazi
Majengo matano ya makazi yanajengwa kwa wakati mmoja. Katika eneo la mbele, wanakandarasi wanafunga vyuma kabla ya kumwaga msingi wa saruji kwa ajili ya Makazi B. Eneo la nyuma upande wa kulia, wanakandarasi wanamwaga msingi wa zege kwenye jengo la Makazi D. Eneo la nyuma upande wa kushoto, mwendesha kreni anajiandaa kusimamisha ukuta kwa ajili ya lifti na ngazi za Makazi E.
Aprili 19, 2017—Eneo la ofisi ya tawi
Fundi katika kikosi kimoja anatumia kifaa fulani kuhakikisha sehemu ambayo mabomba mawili ya plastiki ya kuzima moto yameunganishwa. Mabomba hayo mawili yanaunganishwa kwa kutumia moto ambao unayeyusha plastiki na kuzifanya ziungane. Sehemu hiyo inakaguliwa ili kuhakikisha uimara na ubora. Kwa ujumla, mabomba hayo yana urefu wa kilomita nne hivi.
Aprili 25, 2017—Makazi
Mfanyakazi anasafisha mfereji mpya usiovujisha maji. Mifereji hiyo inaruhusu barabara zijengwe juu ya maji na kuhakikisha maji ya mvua yanaingia kwenye mabwawa, na hivyo kuzuia mafuriko.
Aprili 28, 2017—Makazi F
Mke na mume wanaojua kusoma ramani za ujenzi wanatia alama sehemu ambapo kuta za jengo zitakuwa.
Mei 5, 2017—Makazi
Upande wa mashariki, picha ya angani ya makazi matano yanayojengwa. Kufikia Septemba, kuta za nje zilikuwa kamili, kazi ya kujenga kuta za ndani za Makazi F (kulia nyuma) ilikuwa inaendelea, na kazi ya kupaka rangi jengo hilo ilikuwa imeanza. Wakati huohuo, wafanyakazi walianza kusimamisha kuta za nje na madirisha ya Makazi E (nyuma kushoto). Makazi B, C, na D (upande wa mbele) yalikuwa yakitayarishwa ili timu za wasoma-ramani, mafundi-bomba, mafundi-umeme, na wengine zianze kazi.
Mei 18, 2017—Eneo la Kutegemeza Kazi
Robert Luccioni, msaidizi wa Halmashauri ya Utangazaji ya Baraza Linaloongoza na msimamizi wa Idara ya Usanifu na Ujenzi ya Ulimwenguni Pote (WDC), anatia moyo vikosi vya ujenzi kwa kutoa hotuba ya Biblia. Idara ya WDC inasimamia kazi ya kuchora na kujenga ofisi mpya za tawi na kuhakikisha kwamba kazi yote inafanya kwa njia bora zaidi na kwa gharama zinazofaa.
Mei 25, 2017—Eneo la ofisi ya tawi
Wafanyakazi wanatayarisha zege itakayotumiwa kujenga eneo litakalokuwa na gesi, intaneti, na vifaa vya umeme. Upande wa kulia, wafanyakazi wanatumia kifaa cha kumwaga zege kuweka msingi wa ua utakaopunguza kelele itakayotolewa na vifaa vitakavyokuwa humo ndani.
Juni 7, 2017—Makazi E
Timu ya usanifu majengo inapitia michoro kabla ya kutia alama sakafu kwa ajili ya nguzo za chuma.
Juni 13, 2017—Makazi F
Mfanyakazi akisimamisha nguzo za chuma kwa ajili ya kuta za nje.
Juni 22, 2017—Makazi E
Majukwaa ya kujengea yanasimamishwa kuzunguka Makazi E, yanawasaidia wafanyakazi wafikie kuta kwa urahisi.
Julai 11, 2017—Makazi F
Mpaka-rangi anapaka kitu fulani cha kuhifadhi madirisha mapya yaliyowekwa. Kitu hicho kinapokauka kinazuia madirisha yasiharibiwe ujenzi unapoendelea na kitatolewa baadaye.
Julai 13, 2017—Makazi F
Timu ya mafundi-bomba inakagua mfumo wa kupasha joto ulio chini ya ardhi katika chumba cha makazi. Marekebisho yote yanayohitajiwa yatakapofanywa, mabomba hayo yatafunikwa na zege.
Julai 19, 2017—Eneo la ofisi ya tawi
Mfanyakazi akikata maua ya porini kwenye eneo nje ya mwingilio mkuu wa ofisi ya tawi. Maua hayo yanazuia magugu, na hivyo kupunguza muda na jitihada zinazohitajiwa kutunza eneo hilo lililo karibu na barabara kuu yenye shughuli nyingi.
Agosti 1, 2017—Jengo la ofisi
Akitumia mfumo wa GPS, mfanyakazi anatia alama sehemu itakayokuwa mwingilio wa majengo ya ofisi, anatumia kigingi kuonyesha mahali penyewe, na kukipaka rangi ili kionekane vizuri. Sehemu hii itakuwa na jikoni na vilevile chumba cha kulia chakula na jumba. Majengo ya makazi yanaonekana upande wa nyuma.
Agosti 8, 2017—Makazi
Mke na mume wanatayarisha kifaa cha kuzuia zege isitoke inapomwagwa kwa ajili ya kutengeneza shimo la kuzuia mafuriko ambalo ni sehemu ya mfumo wa kuondoa maji katika majengo. Upande wa nyuma, Makazi E na F yanafunikwa na paa la plastiki ili iwe rahisi kusawazisha kiwango cha joto katika msimu wa baridi kali.
Agosti 9, 2017—Eneo la ofisi ya tawi
Mjitoleaji akijifunza jinsi ya kutumia kifaa. Kifaa hicho kinatumiwa kuinua mawe yenye uzito wa kilo 70 hivi kila moja. Mawe hayo yanapowekwa sehemu inayofaa, zege inamwagwa pande mbili ili kuyashikilia.
Agosti 16, 2017—Eneo la ofisi ya tawi
Bomba la maji linapowekwa, mfanyakazi anahakikisha kwamba litaingia vizuri kwenye sehemu yake. Mabomba ya maji yenye urefu wa kilomita tano hivi yanahitajiwa kwenye ofisi mpya ya tawi.
Agosti 22, 2017—Makazi E
Mfanyakazi anayeshughulikia sehemu za nje za majengo anatumia msumeno wa mawe kukata matofali. Matofali nusu yanatumiwa kurembesha sehemu zilizo mwishoni mwa majengo ya makazi. Kwa ujumla matofali 300,000 hivi yatatumiwa kwenye majengo ya makazi.