Wajitoleaji Waanza Ujenzi Tuxedo
Ni saa 12 na dakika 45 asubuhi huko Tuxedo, New York. Anga halina mawingu na tabaka jembamba la barafu limefunika ziwa dogo la maji lililo karibu na jengo lenye orofa nne ambalo wanaume na wanawake vijana wanaingia. Wamevaa nguo na viatu vya kazi na wamesafiri asubuhi hiyo kutoka katika hoteli na nyumba zilizo karibu, katika maeneo ya Patterson, Wallkill, na hata kutoka Brooklyn, eneo lililo umbali wa kilomita 80 hivi.
Kabla ya siku hii, idadi kubwa ya watu hawa walikuwa wamesafiri kutoka mbali zaidi, yaani, kutoka sehemu mbalimbali za Marekani na kwingineko. Wamejitolea kufanya kazi hapa Tuxedo, wengine kwa juma moja, wengine kwa majuma sita, na wengine kwa muda mrefu zaidi. Walijilipia wenyewe nauli na hawatarajii mshahara wowote kutokana na kazi watakayofanya. Licha ya hilo watu hawa wanafurahia sana kuwa hapa.
Kwa sasa, kuna wajitoleaji wapatao 120, ingawa idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka katika miezi inayokuja. Wajitoleaji hao wanaingia kwenye chumba cha kulia chakula na kuketi kwenye viti vilivyozunguka meza, kila meza ina viti kumi. Wengi wao wanakunywa kahawa huku harufu tamu ya nyama ikienea kutoka jikoni. Saa moja kamili wote wanasikiliza kupitia viwambo vya kompyuta, mazungumzo ya andiko fulani la Biblia. Dakika kumi na tano baadaye, wahudumu wanaleta kiamsha kinywa mezani. Kiamsha kinywa hicho kinatia ndani nyama, mkate, mayai na uji uliotayarishwa kwa unga wa shayiri. Kuna chakula cha kutosha.
Baada ya sala ya mwisho kutolewa, ni wakati wa kwenda kufanya kazi. Wajenzi wanazungumza kwa furaha huku wakivalia kofia zao ngumu, miwani ya usalama, mavazi ya kuwatambulisha kutoka mbali, na mikanda ya kubebea vitu vizito.
Wanatarajiwa kuyageuza majengo ambayo awali yalitumiwa na Kampuni ya Kutengeneza Karatasi huko Tuxedo, na kuyafanya kuwa makazi na mahali ambapo vifaa vya ujenzi kwa ajili ya makao makuu ya ulimwenguni pote ya Mashahidi wa Yehova vitawekwa, ambapo ni karibu sana na mji wa Warwick. Jumanne, Machi 12, 2013, kamati ya upangaji wa mji wa Warwick ilitoa kibali cha kuidhinisha ramani ya ujenzi huo wa Tuxedo.
Wajitoleaji hao wa muda wanapokewa jinsi gani wanapofika kwa mara ya kwanza katika makao yao ya muda? “Tulipofika,” anasema William, kutoka New Jersey, “ndugu waliokuwa katika eneo la mapokezi walitujulisha mambo ya msingi kama vile—vyumba vyetu viko wapi, hali ya eneo au mazingira yetu, na jinsi ya kutumia funguo zetu. Kila mmoja alitusaidia. Tulipofika Tuxedo, tulikutana na msimamizi wetu baada ya kupata kiamsha-kinywa naye akatueleza kazi tutakayofanya.”
Wale wanaoshiriki katika ujenzi huu wanahisije? Yajaira na mume wake walitoka Puerto Rico na wanasaidia kufanya kazi ya kusimamisha kuta zilizotengenezwa kwa aina fulani ya chokaa ngumu. Anasema hivi: “Sisi huamka saa kumi na nusu asubuhi. Tunasafisha chumba chetu, tunakunywa kahawa na kuelekea kwenye basi ambalo limekuja kutuchukua. Mwishoni mwa siku tunajihisi tukiwa wachovu, lakini tuna furaha sana. Kila mtu anafuraha sana.”
Uwanja wa Warwick umezungukwa na msitu. Zach na mke wake, Beth, kutoka Minnesota, wanasaidia kutayarisha eneo hilo la ujenzi. Alipoulizwa kwa nini yeye na mume wake waliamua kuja kusaidia katika mradi huo, Beth alisema: “Tunaamini kwamba kumtumikia Yehova ndilo jambo bora zaidi maishani. Tulitaka kutumia ujuzi wetu kumtumikia.”