Sera ya Mashahidi wa Yehova ya Kulinda Taarifa Ulimwenguni Pote
Tengenezo la kidini la Mashahidi wa Yehova (“shirika la kidini”) linaheshimu haki ya watu ya faragha na ya kulinda taarifa za kibinafsi. Likiwa shirika la kidini linatambua umuhimu wa mawasiliano ya wazi na ya kweli linapokusanya taarifa za kibinafsi na za siri ili kusimamia mahitaji ya Mashahidi wa Yehova linapotimiza utendaji na michango ya kidini, pamoja na kuhakikisha kwamba linadumisha siri na kuzilinda kabisa. (Methali 15:22; 25:9) Hatufunui habari za siri.—Methali 20:19.
Nchi mbalimbali zimepitisha sheria za kulinda taarifa ili kuhakikisha haki ya faragha ya kila mtu inalindwa. Tengenezo letu pamoja na ofisi zake za tawi, sikuzote limekuwa likiheshimu haki ya faragha na kudumisha siri, hata kabla ya kuundwa kwa sheria za kulinda taarifa. Tengenezo hili la dini litaendelea kulinda taarifa linazopokea kama ilivyo kawaida yake ya muda mrefu.
Kanuni za Kulinda Taarifa. Tengenezo linatunza taarifa zote za kibinafsi kulingana na kanuni zifuatazo:
Taarifa za kibinafsi zitashughulikiwa kwa njia ya haki na ya kisheria.
Taarifa za kibinafsi zitakusanywa, kushughulikiwa, na kutumiwa kwa madhumuni ya kutimiza utendaji wa dini na kushughulikia michango.
Taarifa za kibinafsi zitakuwa sahihi na ambazo hazijapitwa na wakati. Kosa lolote litasahihishwa mara tu linapogunduliwa na tengenezo.
Taarifa za kibinafsi zitatunzwa na tengenezo kwa kadiri zinavyohitajika ili zitumiwe kwa makusudi yanayofaa.
Haki za wenye taarifa zitaangaliwa kwa uzito.
Hatua za kiufundi na mipango itafanywa ili kuzuia usambazaji wa taarifa binafsi bila idhini au kinyume cha sheria. Taarifa zote binafsi zinahifadhiwa kwenye kompyuta zenye nywila na zinazotumiwa tu na watu wenye idhini ya kufanya hivyo. Ofisi zenye kompyuta hizo hufungwa baada ya saa za kazi na walioidhinishwa tu ndio wenye ruhusa ya kuingia kwenye ofisi hizo.
Taarifa binafsi hazitatolewa kutoka ofisi moja ya tawi kwenda nyingine ila tu ikiwa ni lazima kufanya hivyo kwa ajili ya kutimiza utendaji wa dini au inapohusu michango ya hiari ya tengenezo la Mashahidi wa Yehova. Mashahidi wa Yehova wote wamekubali mambo hayo kwa hiari kwa kujitambulisha na kukubali kuwa Mashahidi wa Yehova.
Kanuni hizi za kulinda taarifa zinasimamia matumizi ya taarifa za kibinafsi yaliyoonyeshwa kwenye kitabu Tengenezo Linalofanya Mapenzi ya Yehova, ambacho kinatolewa kwa Mashahidi wa Yehova wote wanaofikia hatua ya kuwa wahubiri. Kwa habari zaidi, ona kitabu Tengenezo Linalofanya Mapenzi ya Yehova.
Haki za kila mtu za kulinda habari za kibinafsi au za siri na kurekebisha au kufuta taarifa za kibinafsi au za siri zinaidhinishwa kulingana na utaratibu wa Mashahidi wa Yehova uliobainishwa kwenye Sera ya Ulimwenguni Pote ya Kutumia Taarifa za Kibinafsi chini ya kichwa Haki Zako.
Sera ya Mashahidi wa Yehova ya Kulinda Taarifa Ulimwenguni Pote iliyobainishwa hapo juu inaonyesha jinsi Mashahidi wa Yehova wanavyoshughulikia taarifa za kibinafsi.