“Msimamo wa Ujasiri Unaofanya Tuwaheshimu”
“Msimamo wa Ujasiri Unaofanya Tuwaheshimu”
WAKATI wa utawala wake wa ukatili akiwa kiongozi wa Ujerumani, Adolf Hitler alipokea makumi ya maelfu ya barua. Mnamo mwaka wa 1945, baada ya majeshi ya Urusi kuteka eneo linalozunguka jiji la Berlin, barua nyingi kati ya hizo zilipelekwa Moscow na kuhifadhiwa huko. Mwanahistoria Henrik Eberle amechunguza maelfu ya barua hizo zilizohifadhiwa ili ajue watu waliomwandikia Hitler na kwa nini walifanya hivyo. Eberle alichapisha uamuzi aliofikia katika kitabu chake Briefe an Hitler (Barua Alizoandikiwa Hitler).
“Walimu na wanafunzi, watawa na makasisi, watu wasio na kazi na wafanyabiashara wakubwa, maofisa wakuu wa jeshi la wanamaji na askari-jeshi wa kawaida—wote walimwandikia Hitler,” akasema Dakt. Eberle. “Wengine walimheshimu kama Masihi aliyezaliwa kwa mara ya pili; na wengine wakamwona kama chanzo kikuu cha uovu.” Je, Hitler alipokea barua za malalamiko kutoka kwa viongozi wa kidini kuhusu mateso yaliyokuwa yakitekelezwa na Wanazi? Ndiyo, alipokea, lakini hazikuwa nyingi.
Hata hivyo, kati ya barua hizo zilizohifadhiwa Moscow, Eberle alipata faili iliyokuwa na barua ambazo Hitler aliandikiwa na Mashahidi wa Yehova kutoka sehemu mbalimbali nchini Ujerumani, wakilalamikia mateso yaliyotekelezwa na Wanazi. Mashahidi kutoka nchi 50 hivi walimwandikia Hitler barua na telegramu zipatazo 20,000 wakilalamikia jinsi Mashahidi wa Yehova walivyokuwa wakiteswa. Maelfu ya Mashahidi walikamatwa na mamia kadhaa wakauawa au kufa kwa sababu ya kuteswa na Wanazi. Dakt. Eberle anamalizia kwa kusema: “Unapofikiria mamilioni ya watu walioteswa na Wanazi, idadi hiyo [ya Mashahidi walioteswa] inaonekana kuwa ndogo. Lakini watu hao waliteswa kwa sababu walikuwa na umoja na msimamo wa ujasiri unaofanya tuwaheshimu.”