Kitabu cha Kwanza cha Samweli 19:1-24

  • Sauli aendelea kumchukia Daudi (1-13)

  • Daudi amkimbia Sauli (14-24)

19  Baadaye Sauli akazungumza na Yonathani mwana wake na watumishi wake wote kuhusu kumuua Daudi.+  Kwa kuwa Yonathani mwana wa Sauli alimpenda sana Daudi,+ alimwambia hivi Daudi: “Sauli baba yangu anakusudia kukuua. Tafadhali jihadhari itakapofika asubuhi, nenda mahali pa siri na ujifiche huko.  Nitakuja na kusimama kando ya baba yangu shambani mahali utakapokuwa. Nitaongea na baba yangu kukuhusu, nikipata habari yoyote, bila shaka nitakuambia.”+  Basi Yonathani akamsifu Daudi+ mbele ya Sauli baba yake. Akamwambia: “Mfalme, usimtendee dhambi mtumishi wako Daudi kwa sababu yeye hajakutendea dhambi na mambo aliyokufanyia yamekunufaisha.  Alihatarisha uhai wake* alipomuua yule Mfilisti,+ na Yehova akawapa Waisraeli wote ushindi* mkubwa. Uliona jambo hilo, ukashangilia sana. Basi kwa nini uitendee dhambi damu isiyo na hatia kwa kuagiza Daudi auawe bila sababu?”+  Sauli akamsikiliza Yonathani na kuapa hivi: “Kwa hakika kama Yehova anavyoishi, hatauawa.”  Baadaye Yonathani akamwita Daudi na kumwambia mambo hayo yote. Kisha Yonathani akampeleka Daudi kwa Sauli, naye akaendelea kumtumikia kama awali.+  Baada ya muda vita vikatokea tena, na Daudi akaenda kupigana na Wafilisti na kuwaua Wafilisti wengi sana, nao wakakimbia kutoka mbele yake.  Na roho mbaya kutoka kwa Yehova ikamjia Sauli+ alipokuwa ameketi nyumbani mwake akiwa na mkuki mkononi, huku Daudi akipiga muziki kwa kinubi.+ 10  Sauli akajaribu kumpigilia Daudi ukutani kwa mkuki, lakini akamkwepa Sauli, na mkuki huo ukapenya ukutani. Daudi akakimbia na kutoroka usiku huo. 11  Baadaye Sauli akawatuma wajumbe nyumbani kwa Daudi ili wailinde na kumuua asubuhi,+ lakini Mikali mke wa Daudi akamwambia Daudi: “Usipotoroka usiku wa leo, kesho utakuwa mfu.” 12  Mara moja Mikali akamteremsha Daudi kupitia dirishani, ili akimbie na kutoroka. 13  Mikali akachukua sanamu ya terafimu* na kuiweka kitandani, akaifunika kwa vazi na kuweka wavu wa manyoya ya mbuzi mahali ambapo Daudi hulaza kichwa chake. 14  Basi Sauli akawatuma wajumbe wamlete Daudi, lakini mke wa Daudi akawaambia: “Ni mgonjwa.” 15  Kisha Sauli akawatuma wajumbe hao wamwone Daudi, akawaambia: “Mleteni kwangu akiwa kwenye kitanda chake ili auawe.”+ 16  Wajumbe hao walipoingia, walikuta sanamu ya terafimu* kitandani na wavu wa manyoya ya mbuzi mahali anapolaza kichwa chake. 17  Sauli akamuuliza Mikali: “Kwa nini ulinidanganya hivi na kumwacha adui yangu+ akimbie na kutoroka?” Mikali akamjibu Sauli: “Aliniambia, ‘Niache niende, nisije nikakuua!’” 18  Basi Daudi alikimbia na kutoroka, akafika kwa Samweli kule Rama.+ Akamwambia mambo yote ambayo Sauli alikuwa amemtendea. Kisha yeye na Samweli wakaenda zao, wakakaa kule Naiothi.+ 19  Baada ya muda Sauli aliambiwa hivi: “Tazama! Daudi yuko Naiothi kule Rama.” 20  Mara moja Sauli akawatuma wajumbe wamkamate Daudi. Walipowaona manabii waliozeeka wakitoa unabii na Samweli akiwa amesimama na kuwaongoza, roho ya Mungu ikawajia wajumbe wa Sauli, nao pia wakaanza kutenda kama manabii. 21  Walipomwambia Sauli habari hizo, mara moja akawatuma wajumbe wengine, nao pia wakaanza kutenda kama manabii. Basi Sauli akawatuma tena wajumbe wengine, kikundi cha tatu, nao pia wakaanza kutenda kama manabii. 22  Mwishowe yeye pia akaenda Rama. Alipofika kwenye tangi kubwa la maji lililoko Seku, akauliza: “Samweli na Daudi wako wapi?” Wakamjibu: “Wako Naiothi+ kule Rama.” 23  Sauli alipokuwa njiani kutoka huko kwenda Naiothi kule Rama, roho ya Mungu ikamjia pia, naye akatembea huku akitenda kama nabii mpaka alipoingia Naiothi kule Rama. 24  Akararua pia mavazi yake, naye pia akatenda kama nabii mbele ya Samweli, akalala huko mchana wote na usiku huo wote akiwa uchi.* Ndiyo sababu wanasema: “Je, Sauli pia ni mmoja wa manabii?”+

Maelezo ya Chini

Au “Aliitia nafsi yake mikononi mwake.”
Au “wokovu.”
Au “mungu wa familia; sanamu.”
Au “mungu wa familia; sanamu.”
Au “akiwa na mavazi machache.”