Kitabu cha Kwanza cha Samweli 27:1-12
-
Wafilisti wampa Daudi Siklagi (1-12)
27 Hata hivyo, Daudi akasema moyoni mwake: “Siku moja mkono wa Sauli utaniua. Jambo bora la kufanya ni kukimbilia+ nchi ya Wafilisti; halafu Sauli atakata tamaa ya kunitafuta katika eneo lote la Israeli,+ nami nitaponyoka kutoka mkononi mwake.”
2 Basi Daudi akaondoka pamoja na wanaume 600+ waliokuwa naye, akavuka kwenda kwa Akishi+ mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi.
3 Daudi na wanaume wake wakakaa na Akishi huko Gathi, kila mwanamume na familia yake. Daudi alikuwa na wake zake wawili, Ahinoamu+ wa Yezreeli na Abigaili+ Mkarmeli, mjane wa Nabali.
4 Sauli alipoambiwa kwamba Daudi alikuwa amekimbia kwenda Gathi, aliacha kumtafuta.+
5 Ndipo Daudi akamwambia Akishi: “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, naomba unipe mahali katika mojawapo ya majiji ya mashambani, ili niishi huko. Kwa nini mimi mtumishi wako niishi pamoja nawe katika jiji hili la kifalme?”
6 Basi Akishi akampa Siklagi+ siku hiyo. Ndiyo sababu tangu siku hiyo Siklagi limekuwa jiji la wafalme wa Yuda.
7 Daudi aliishi katika eneo la mashambani la Wafilisti kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne.+
8 Daudi alikuwa akipanda pamoja na wanaume wake kuwavamia Wageshuri,+ Wagirzi, na Waamaleki,+ kwa maana walikuwa wakikaa katika nchi iliyoanzia Telamu mpaka Shuri+ na kushuka mpaka nchi ya Misri.
9 Daudi alipokuwa akiishambulia nchi, hakumwacha hai mwanamume wala mwanamke yeyote,+ bali alichukua kondoo, ng’ombe, punda, ngamia, na mavazi, kisha alirudi kwa Akishi.
10 Na Akishi alipokuwa akimuuliza: “Ulivamia wapi leo?” Daudi alimjibu: “Upande wa kusini wa* Yuda”+ au “Upande wa kusini wa Wayerahmeeli”+ au “Upande wa kusini wa Wakeni.”+
11 Daudi hakumwacha hai mwanamume au mwanamke yeyote ili wasiletwe Gathi, kwa kuwa alisema: “Wasije wakawaambia habari zetu wakisema, ‘Hivi ndivyo Daudi alivyofanya.’” (Alizoea kufanya hivyo muda wote alioishi katika eneo la mashambani la Wafilisti.)
12 Kwa hiyo Akishi akamwamini Daudi akisema moyoni mwake: “Bila shaka ananuka miongoni mwa watu wake wa Israeli, kwa hiyo atakuwa mtumishi wangu sikuzote.”
Maelezo ya Chini
^ Au “Dhidi ya Negebu ya.”