Kitabu cha Kwanza cha Samweli 9:1-27

  • Samweli akutana na Sauli (1-27)

9  Kulikuwa na mtu wa Benjamini aliyeitwa Kishi,+ mwana wa Abieli, mwana wa Zerori mwana wa Bekorathi mwana wa Afia, Mbenjamini+ aliyekuwa tajiri sana.  Alikuwa na mwana aliyeitwa Sauli,+ kijana mwenye sura nzuri, hakuna mwanamume yeyote kati ya Waisraeli aliyekuwa na sura nzuri kuliko yeye, na aliposimama watu wote walimfikia mabegani.  Punda wa Kishi baba ya Sauli walipopotea, Kishi alimwambia hivi Sauli mwanawe: “Tafadhali mchukue mtumishi mmoja mwende mkawatafute punda.”  Wakapita katika eneo lenye milima la Efraimu na katika nchi ya Shalisha, lakini hawakuwapata. Wakasafiri kupitia nchi ya Shaalimu, lakini hawakuwapata punda huko. Wakapita katika nchi yote ya Wabenjamini, lakini hawakuwapata.  Wakafika katika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia mtumishi wake aliyekuwa pamoja naye: “Njoo, acha turudi, ili baba yangu asianze kutuhangaikia badala ya kuhangaikia punda.”+  Lakini mtumishi huyo akamwambia: “Tazama! Kuna mtu wa Mungu katika jiji hili, mtu anayeheshimiwa. Kila jambo analosema lazima litimie.+ Twende huko sasa. Labda anaweza kutuambia njia ya kufuata.”  Basi Sauli akamwambia hivi mtumishi wake: “Tukienda, tutampelekea nini mtu huyo? Mifuko yetu haina mikate; hatuna zawadi yoyote ya kumpelekea huyo mtu wa Mungu wa kweli. Tuna nini?”  Basi mtumishi huyo akamjibu hivi Sauli: “Tazama! Nimebeba mikononi mwangu robo ya shekeli* ya fedha. Nitampa huyo mtu wa Mungu wa kweli, naye atatuambia njia ya kufuata.”  (Zamani katika Israeli, mtu alikuwa akisema hivi alipoenda kutafuta mwongozo wa Mungu: “Njoo, twende kwa mwonaji.”+ Kwa maana mtu ambaye leo anaitwa nabii, zamani aliitwa mwonaji.) 10  Ndipo Sauli akamwambia hivi mtumishi wake: “Ulilosema ni jema. Haya twende.” Basi wakaenda katika jiji alimokuwa yule mtu wa Mungu wa kweli. 11  Walipokuwa wakipanda kwenda jijini, walikutana na wasichana waliokuwa wakienda kuteka maji. Basi wakawauliza: “Je, mwonaji+ yuko katika jiji hili?” 12  Wakajibu: “Ndiyo. Hajafika mbali sana. Fanyeni haraka, kwa sababu amekuja jijini leo, kwa maana leo watu wanatoa dhabihu+ mahali pa juu.+ 13  Mara tu mtakapoingia jijini, mtamkuta kabla hajapanda kwenda mahali pa juu kula chakula. Watu hawatakula mpaka atakapofika, kwa maana yeye ndiye anayebariki dhabihu. Baada ya kufanya hivyo, wale walioalikwa wanaweza kula. Basi pandeni sasa moja kwa moja, mtamkuta.” 14  Basi wakapanda kwenda jijini. Walipokuwa wakiingia katikati ya jiji, Samweli alikuwa akija kukutana nao akielekea mahali pa juu. 15  Siku iliyotangulia kabla ya Sauli kufika, Yehova alikuwa amemwambia* Samweli: 16  “Kesho wakati kama huu, nitatuma mtu kwako kutoka katika nchi ya Benjamini.+ Utamtia mafuta awe kiongozi juu ya watu wangu Waisraeli,+ naye atawaokoa watu wangu kutoka mikononi mwa Wafilisti. Kwa sababu nimeyaona mateso ya watu wangu, na kilio chao kimenifikia.”+ 17  Samweli alipomwona Sauli, Yehova akamwambia: “Huyu ndiye mtu niliyekwambia, ‘Yeye ndiye atakayewaongoza watu wangu.’”*+ 18  Kisha Sauli akamkaribia Samweli katikati ya lango na kumuuliza: “Tafadhali niambie, nyumba ya mwonaji iko wapi?” 19  Samweli akamjibu Sauli: “Mimi ndiye mwonaji. Panda utangulie mbele yangu mahali pa juu, nawe utakula pamoja nami leo.+ Asubuhi nitakuruhusu uende, nami nitakueleza mambo yote unayotaka kujua.* 20  Kuhusu wale punda waliopotea siku tatu zilizopita,+ usiwe na wasiwasi juu yao, kwa maana wamepatikana. Vitu vyote vyenye kutamanika vya Israeli ni vya nani? Je, si vyako na vya nyumba yote ya baba yako?”+ 21  Ndipo Sauli akasema: “Je, mimi si Mbenjamini kutoka katika kabila dogo zaidi kati ya makabila ya Israeli,+ na je, familia yangu si familia ya chini kabisa kati ya familia zote za kabila la Benjamini? Basi kwa nini unaniambia hivyo?” 22  Kisha Samweli akamchukua Sauli na mtumishi wake, akawaleta katika ukumbi wa kulia chakula, akawapa mahali pa kuketi mbele ya watu walioalikwa wapatao 30.⁠ 23  Samweli akamwambia mpishi: “Kilete chakula nilichokupa na kukuambia, ‘Kiweke kando.’” 24  Basi mpishi akainua ule mguu na nyama iliyokuwa juu yake, akauweka mbele ya Sauli. Samweli akasema: “Kilichokuwa kimehifadhiwa kimewekwa mbele yako. Kula, kwa maana kilihifadhiwa kwa ajili yako katika karamu hii. Kwa sababu niliwaambia, ‘Nimewaalika wageni.’” Basi Sauli akala pamoja na Samweli siku hiyo. 25  Kisha wakashuka kutoka mahali pa juu+ na kwenda jijini, naye akaendelea kuzungumza na Sauli kwenye paa la nyumba. 26  Wakaamka mapema, na kulipopambazuka, Samweli akamwita Sauli kutoka paani akisema: “Jitayarishe, ili nikusindikize.” Basi Sauli akajitayarisha na yeye pamoja na Samweli wakatoka nje. 27  Walipokuwa wakishuka kuelekea ukingoni mwa jiji, Samweli akamwambia Sauli: “Mwambie mtumishi+ atangulie mbele yetu,” basi akatangulia. “Lakini wewe, simama tuli sasa, ili nikujulishe neno la Mungu.”

Maelezo ya Chini

Shekeli moja ilikuwa na uzito wa gramu 11.4. Angalia Nyongeza B14.
Tnn., “amefunua sikio la.”
Au “atakayewazuia watu wangu wasipite mipaka.”
Tnn., “mambo yote yaliyo moyoni mwako.”