Kitabu cha Kwanza cha Wafalme 16:1-34

  • Hukumu ya Yehova dhidi ya Baasha (1-7)

  • Ela, mfalme wa Israeli (8-14)

  • Zimri, mfalme wa Israeli (15-20)

  • Omri, mfalme wa Israeli (21-28)

  • Ahabu, mfalme wa Israeli (29-33)

  • Hieli ajenga upya Yeriko (34)

16  Kisha neno hili la Yehova dhidi ya Baasha likamjia Yehu+ mwana wa Hanani:+  “Nilikuinua kutoka mavumbini na kukufanya kuwa kiongozi wa watu wangu Waisraeli,+ lakini uliendelea kutembea katika njia ya Yeroboamu na kusababisha watu wangu Waisraeli watende dhambi hivi kwamba walinikasirisha kwa dhambi zao.+  Kwa hiyo ninamfagilia mbali Baasha na nyumba yake, nami nitaifanya nyumba yake kuwa kama nyumba ya Yeroboamu+ mwana wa Nebati.  Mtu yeyote wa nyumba ya Baasha anayefia jijini ataliwa na mbwa; na mtu yeyote wa nyumba yake anayefia shambani ataliwa na ndege wa angani.”  Na mambo mengine katika historia ya Baasha, mambo aliyofanya na ukuu wake, je, hayajaandikwa katika kitabu cha historia ya nyakati za wafalme wa Israeli?  Kisha Baasha akafa na kuzikwa pamoja na mababu zake kule Tirsa;+ na Ela mwana wake akawa mfalme baada yake.  Tena, neno la Yehova dhidi ya Baasha na nyumba yake lilikuja kupitia nabii Yehu mwana wa Hanani, kwa sababu ya uovu wote aliotenda machoni pa Yehova na kumkasirisha kwa kazi za mikono yake, akawa kama nyumba ya Yeroboamu, na pia kwa sababu alimuua Nadabu.*+  Katika mwaka wa 26 wa Mfalme Asa wa Yuda, Ela mwana wa Baasha akawa mfalme wa Israeli kule Tirsa, naye alitawala kwa miaka miwili.  Zimri mtumishi wake, mkuu wa nusu ya kikosi chake cha magari ya vita, alipanga njama dhidi yake alipokuwa Tirsa akinywa na kulewa nyumbani kwa Arsa, msimamizi wa nyumba yake kule Tirsa. 10  Zimri akaingia, akampiga+ na kumuua katika mwaka wa 27 wa Mfalme Asa wa Yuda, naye akawa mfalme baada yake. 11  Alipokuwa mfalme, mara tu alipoketi kwenye kiti chake cha ufalme, aliiangamiza nyumba yote ya Baasha. Hakumwacha mwanamume yeyote,* iwe ni mtu wake wa ukoo* au ni rafiki yake. 12  Basi Zimri akaiangamiza nyumba yote ya Baasha, kama Yehova alivyokuwa amesema dhidi ya Baasha kupitia nabii Yehu.+ 13  Alifanya hivyo kwa sababu ya dhambi zote ambazo Baasha na mwanawe Ela walikuwa wametenda na dhambi ambazo walisababisha Waisraeli kutenda na kumkasirisha Yehova Mungu wa Israeli kwa sanamu zao za ubatili.+ 14  Na mambo mengine katika historia ya Ela, mambo yote aliyofanya, je, hayajaandikwa katika kitabu cha historia ya nyakati za wafalme wa Israeli? 15  Katika mwaka wa 27 wa Mfalme Asa wa Yuda, Zimri akawa mfalme kwa siku saba kule Tirsa wanajeshi walipokuwa wamepiga kambi dhidi ya Gibethoni,+ jiji la Wafilisti. 16  Baada ya muda wanajeshi waliokuwa wamepiga kambi wakasikia hivi: “Zimri amepanga njama na pia amemuua mfalme.” Basi siku hiyo huko kambini Waisraeli wote wakamweka Omri,+ mkuu wa jeshi, kuwa mfalme wa Israeli. 17  Omri na Waisraeli wote wakapanda kutoka Gibethoni na kulizingira Tirsa. 18  Zimri alipoona kwamba jiji limetekwa, akaingia katika mnara wenye ngome wa nyumba ya mfalme* na kuiteketeza kwa moto akiwa ndani yake, naye akafa.+ 19  Alifanya hivyo kwa sababu ya dhambi zake mwenyewe alizofanya alipotenda maovu machoni pa Yehova kwa kutembea katika njia ya Yeroboamu na kwa sababu ya dhambi aliyosababisha Waisraeli wafanye.+ 20  Na mambo mengine katika historia ya Zimri pamoja na njama yake, je, hayajaandikwa katika kitabu cha historia ya nyakati za wafalme wa Israeli? 21  Wakati huo ndipo watu wa Israeli walipogawanyika makundi mawili. Kundi moja lilimfuata Tibni mwana wa Ginathi likitaka kumfanya kuwa mfalme, na kundi lingine likamfuata Omri. 22  Lakini watu waliokuwa wakimfuata Omri waliwashinda watu waliokuwa wakimfuata Tibni mwana wa Ginathi. Basi Tibni akafa, na Omri akawa mfalme. 23  Katika mwaka wa 31 wa Mfalme Asa wa Yuda, Omri akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala kwa miaka 12. Alitawala Tirsa kwa miaka sita. 24  Alinunua mlima wa Samaria kutoka kwa Shemeri kwa talanta mbili za fedha,* akajenga jiji juu ya mlima huo. Jiji alilojenga aliliita Samaria,*+ jina la Shemeri mmiliki* wa mlima huo. 25  Omri akaendelea kutenda maovu machoni pa Yehova, akatenda maovu kuliko wote waliomtangulia.+ 26  Alitembea katika njia zote za Yeroboamu mwana wa Nebati na katika dhambi aliyokuwa amesababisha Waisraeli wafanye na kumkasirisha Yehova Mungu wa Israeli kwa sanamu zao za ubatili.+ 27  Na mambo mengine katika historia ya Omri, mambo aliyofanya na mambo makuu aliyotekeleza, je, hayajaandikwa katika kitabu cha historia ya nyakati za wafalme wa Israeli? 28  Kisha Omri akafa na kuzikwa pamoja na mababu zake huko Samaria; na Ahabu+ mwana wake akawa mfalme baada yake. 29  Ahabu mwana wa Omri akawa mfalme wa Israeli katika mwaka wa 38 wa Mfalme Asa wa Yuda, na Ahabu mwana wa Omri akatawala Israeli kwa miaka 22 huko Samaria.+ 30  Ahabu mwana wa Omri alikuwa mwovu sana machoni pa Yehova kuliko wote waliomtangulia.+ 31  Na kana kwamba lilikuwa jambo dogo kwake kutembea katika dhambi za Yeroboamu+ mwana wa Nebati, hata alimwoa Yezebeli+ binti ya Ethbaali, mfalme wa Wasidoni,+ akaanza kumwabudu Baali+ na kumwinamia. 32  Isitoshe, alisimamisha madhabahu kwa ajili ya Baali katika nyumba ya Baali+ aliyoijenga* kule Samaria. 33  Ahabu pia alitengeneza mti mtakatifu.*+ Ahabu alifanya mambo mengi zaidi yaliyomkasirisha Yehova Mungu wa Israeli kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. 34  Katika siku zake, Hieli kutoka Betheli alijenga upya Yeriko. Alipojenga msingi wake, Abiramu mzaliwa wake wa kwanza alikufa, na alipoweka malango yake, Segubu mwana wake wa mwisho akafa, kama Yehova alivyokuwa amesema kupitia Yoshua mwana wa Nuni.+

Maelezo ya Chini

Yaani, mwana wa Yeroboamu.
Tnn., “mtu yeyote anayekojoa ukutani.” Huu ni msemo wa Kiebrania wa kuwadharau wanaume.
Au “watu wanaolipiza kisasi chake cha damu.”
Au “jumba la mfalme.”
Talanta moja ilikuwa na uzito wa kilogramu 34.2. Angalia Nyongeza B14.
Maana yake “Mali ya Ukoo wa Shemeri.”
Tnn., “bwana.”
Au “hekalu la Baali alilojenga.”
Angalia Kamusi.