Kitabu cha Pili cha Samweli 11:1-27

  • Daudi afanya uzinzi na Bath-sheba (1-13)

  • Daudi apanga Uria auawe (14-25)

  • Daudi amchukua Bath-sheba kuwa mke wake (26, 27)

11  Mwanzoni mwa mwaka,* wakati ambapo wafalme huenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu na watumishi wake pamoja na jeshi lote la Israeli kuwaangamiza Waamoni, nao wakalizingira Raba,+ lakini Daudi alibaki Yerusalemu.+  Jioni moja Daudi aliamka kitandani akaenda kutembeatembea juu ya paa la nyumba ya mfalme.* Akiwa kwenye paa alimwona mwanamke akioga, na mwanamke huyo alikuwa mrembo sana.  Daudi akamtuma mtu fulani aulize kuhusu mwanamke huyo, mtu huyo akamwambia: “Ni Bath-sheba,+ binti ya Eliamu;+ mke wa Uria+ Mhiti.”+  Kisha Daudi akawatuma wajumbe wamlete.+ Basi akaja kwa Daudi, naye Daudi akalala naye.+ (Wakati huo mwanamke huyo alikuwa akijitakasa uchafu wake.*)+ Kisha, mwanamke huyo akarudi nyumbani kwake.  Mwanamke huyo akapata mimba, akatuma ujumbe huu kwa Daudi: “Nina mimba.”  Ndipo Daudi akatuma ujumbe huu kwa Yoabu: “Mtume kwangu Uria Mhiti.” Basi Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi.  Uria alipofika, Daudi akamuuliza habari za Yoabu, habari kuhusu wanajeshi, na kuhusu vita.  Kisha Daudi akamwambia Uria: “Shuka uende nyumbani kwako ukapumzike.”* Uria alipotoka nyumbani mwa mfalme, alipelekewa zawadi ya hisani kutoka kwa mfalme.*  Lakini Uria alilala kwenye mlango wa nyumba ya mfalme pamoja na watumishi wengine wote wa bwana wake, naye hakushuka kwenda nyumbani kwake. 10  Kwa hiyo Daudi akaambiwa: “Uria hakushuka kwenda nyumbani kwake.” Ndipo Daudi akamuuliza Uria: “Umetoka safarini, sivyo? Kwa nini hukushuka kwenda nyumbani kwako?” 11  Uria akamjibu Daudi: “Sanduku la agano+ na wanaume wa Israeli na Yuda wanakaa katika vibanda, na bwana wangu Yoabu na watumishi wake wanapiga kambi uwanjani. Ninawezaje kwenda nyumbani kwangu kula na kunywa na kulala na mke wangu?+ Kwa hakika kama unavyoishi na kama ulivyo hai,* sitafanya hivyo!” 12  Basi Daudi akamwambia Uria: “Kaa hapa leo pia, na kesho nitakuruhusu uende.” Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku hiyo na siku iliyofuata. 13  Halafu Daudi akaagiza aitwe ili ale na kunywa pamoja naye, akamfanya alewe. Lakini jioni, Uria alienda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, naye hakushuka kwenda nyumbani kwake. 14  Asubuhi Daudi akamwandikia Yoabu barua, akampa Uria aipeleke kwa Yoabu. 15  Katika barua hiyo, Daudi aliandika hivi: “Mwekeni Uria kwenye mstari wa mbele mahali ambapo vita ni vikali zaidi. Kisha mmwache na kurudi nyuma yake ili apigwe na kuuawa.”+ 16  Yoabu alikuwa amelichunguza jiji kwa makini, basi alimweka Uria mahali ambapo alijua kuna wanajeshi mashujaa. 17  Wanaume wa jiji walipotoka nje na kupigana na Yoabu, baadhi ya watumishi wa Daudi waliuawa, na Uria Mhiti alikuwa miongoni mwa watu waliouawa.+ 18  Sasa Yoabu akampelekea Daudi habari zote za vita. 19  Alimpa mjumbe maagizo haya: “Utakapomaliza kumwambia mfalme habari zote za vita, 20  huenda mfalme atakasirika na kukuuliza, ‘Kwa nini mlienda karibu sana na jiji kupigana? Je, hamkujua kwamba watawapiga mishale kutoka juu ya ukuta? 21  Ni nani aliyemuua Abimeleki+ mwana wa Yerubeshethi?+ Je, si mwanamke aliyemwangushia jiwe la juu la kusagia kutoka juu ya ukuta na kumuua kule Thebesi? Kwa nini mlienda karibu sana na ukuta?’ Kisha utamwambia, ‘Pia mtumishi wako Uria Mhiti amekufa.’” 22  Basi mjumbe huyo akaenda na kumwambia Daudi kila jambo ambalo Yoabu alimtuma amwambie. 23  Mjumbe huyo akamwambia Daudi: “Wanaume wao walituzidi nguvu, nao walitoka ili kutushambulia uwanjani; lakini tuliwarudisha nyuma mpaka kwenye lango la jiji. 24  Na wapiga mishale walikuwa wakiwapiga kwa mishale watumishi wako kutoka juu ya ukuta, na baadhi ya watumishi wako mfalme wakafa; mtumishi wako Uria Mhiti akafa pia.”+ 25  Ndipo Daudi akamwambia mjumbe huyo: “Mwambie hivi Yoabu: ‘Jambo hili lisikuhangaishe, kwa maana upanga humnyafua huyu na pia yule. Zidisheni mashambulizi dhidi ya jiji na mlishinde.’+ Nawe umtie moyo.” 26  Mke wa Uria aliposikia kwamba Uria mume wake amekufa, akaanza kumwombolezea mume wake. 27  Mara tu kipindi cha kuomboleza kilipokwisha, Daudi akaagiza aletwe nyumbani kwake, akawa mke wake+ na kumzalia mwana. Lakini jambo ambalo Daudi alikuwa amefanya lilimchukiza sana* Yehova.+

Maelezo ya Chini

Yaani, majira ya kuchipua.
Au “jumba la mfalme.”
Huenda ni uchafu wa hedhi.
Tnn., “ukanawe miguu yako.”
Au “fungu la mfalme,” yaani, fungu ambalo mwenyeji humtumia mgeni mheshimiwa.
Au “kama nafsi yako inavyoishi.”
Tnn., “lilikuwa jambo ovu machoni pa.”