Kitabu cha Pili cha Samweli 13:1-39

  • Amnoni ambaka Tamari (1-22)

  • Absalomu amuua Amnoni (23-33)

  • Absalomu akimbilia Geshuri (34-39)

13  Sasa Absalomu mwana wa Daudi alikuwa na dada mrembo aliyeitwa Tamari,+ basi Amnoni+ mwana wa Daudi akampenda.  Amnoni akateseka sana hivi kwamba akawa mgonjwa kwa sababu ya Tamari dada yake, kwa maana alikuwa bikira na ilionekana kwamba haiwezekani kwa Amnoni kumfanyia jambo lolote.  Sasa Amnoni alikuwa na rafiki aliyeitwa Yehonadabu,+ mwana wa Shimea,+ ndugu ya Daudi; na Yehonadabu alikuwa mtu mjanja sana.  Kwa hiyo akamuuliza: “Kwa nini wewe, mwana wa mfalme, unasononeka kila asubuhi? Kwa nini usiniambie?” Amnoni akamjibu hivi: “Ninampenda Tamari, dada+ ya ndugu yangu Absalomu.”  Yehonadabu akamwambia: “Lala kitandani mwako, ujifanye mgonjwa. Baba yako akija kukuona, mwambie, ‘Tafadhali, mruhusu dada yangu Tamari aje kuniandalia chakula kidogo. Akitayarisha chakula cha mgonjwa* mbele ya macho yangu nitakichukua kutoka mkononi mwake na kula.’”  Basi Amnoni akalala kitandani na kujifanya mgonjwa, hivyo mfalme akaja kumwona. Ndipo Amnoni akamwambia mfalme: “Tafadhali, mruhusu dada yangu Tamari aje kuniokea keki mbili zenye umbo la moyo mbele ya macho yangu, ili nichukue chakula kutoka mkononi mwake.”  Kwa hiyo Daudi akamtumia Tamari ujumbe nyumbani, akisema: “Tafadhali, nenda katika nyumba ya ndugu yako Amnoni, umtayarishie chakula.”*  Basi Tamari akaenda katika nyumba ya ndugu yake Amnoni, alimokuwa amelala. Akachukua unga, akaukanda na kuoka keki mbele ya Amnoni.  Kisha akachukua kikaango na kumpa keki hizo. Lakini Amnoni akakataa kula, akasema: “Waambie watu wote waondoke!” Basi watu wote wakaondoka. 10  Kisha Amnoni akamwambia Tamari: “Niletee chakula* katika chumba cha kulala, ili nikichukue kutoka mkononi mwako na kukila.” Basi Tamari akachukua keki zenye umbo la moyo ambazo alikuwa ameoka na kumletea Amnoni ndugu yake katika chumba cha kulala. 11  Alipomletea ili ale, Amnoni akamkamata kwa nguvu na kumwambia: “Njoo, ulale nami, dada yangu.” 12  Lakini Tamari akamwambia: “Usifanye hivyo ndugu yangu! Usiniabishe, kwa maana jambo kama hili halipaswi kufanywa katika Israeli.+ Usitende jambo hili la aibu.+ 13  Nitaondoaje aibu yangu? Nawe utaonwa kuwa kama mmojawapo wa wanaume wapumbavu katika Israeli. Sasa, tafadhali, ongea na mfalme, kwa maana hatakukataza unichukue.” 14  Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza, akamzidi nguvu Tamari na kumwaibisha kwa kumbaka. 15  Kisha Amnoni akaanza kumchukia kwa chuki kali sana, hivi kwamba chuki hiyo ikawa kubwa sana kuliko upendo aliokuwa nao mwanzoni kumwelekea. Amnoni akamwambia: “Inuka; nenda zako!” 16  Ndipo Tamari akamwambia: “Usinifukuze, ndugu yangu, kwa maana kitendo cha kunifukuza sasa ni kibaya zaidi kuliko jambo ulilonitendea!” Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza. 17  Basi akamwita kijana aliyemtumikia na kumwambia: “Tafadhali, mwondoe mtu huyu mbele yangu, na ufunge mlango.” 18  (Sasa Tamari alikuwa amevaa joho la pekee,* kwa maana hayo ndiyo mavazi yaliyovaliwa na mabinti wa mfalme waliokuwa mabikira.) Kwa hiyo mtumishi huyo akamtoa nje na kufunga mlango. 19  Tamari akatia majivu kichwani mwake,+ akalirarua joho bora alilokuwa amevaa; akaweka mikono yake kichwani na kwenda zake, huku akilia kwa sauti alipokuwa akitembea. 20  Ndipo Absalomu ndugu yake+ akamuuliza: “Je, ni Amnoni ndugu yako aliyelala nawe? Sasa nyamaza, dada yangu. Yeye ni ndugu yako.+ Usiruhusu jambo hili likae moyoni mwako.” Hivyo, Tamari akaishi peke yake katika nyumba ya Absalomu ndugu yake. 21  Mfalme Daudi aliposikia mambo hayo yote, alikasirika sana.+ Lakini hakutaka kumuumiza hisia Amnoni mwanawe, kwa sababu alimpenda, na alikuwa mzaliwa wake wa kwanza. 22  Absalomu hakumwambia Amnoni jambo lolote jema au baya; kwa maana Absalomu alimchukia+ Amnoni kwa sababu alikuwa amemwaibisha Tamari dada yake.+ 23  Baada ya miaka miwili kamili, wakataji manyoya ya kondoo wa Absalomu walipokuwa kule Baal-hasori, karibu na Efraimu,+ Absalomu aliwaalika wana wote wa mfalme.+ 24  Basi Absalomu akaja kwa mfalme na kumwambia: “Kondoo wangu, mimi mtumishi wako, wanakatwa manyoya. Nakuomba wewe mfalme na watumishi wako twende pamoja.” 25  Lakini mfalme akamwambia Absalomu: “La, mwanangu. Tukienda sisi sote, tutakuwa mzigo kwako.” Ingawa aliendelea kumsihi, mfalme hakukubali kwenda, lakini alimbariki. 26  Ndipo Absalomu akamwambia: “Ikiwa hutaenda, tafadhali mruhusu Amnoni ndugu yangu aende pamoja nasi.”+ Mfalme akamuuliza: “Kwa nini aende pamoja nawe?” 27  Lakini Absalomu akamsihi, kwa hiyo mfalme akamruhusu Amnoni na wana wote wa mfalme waende pamoja na Absalomu. 28  Kisha Absalomu akawaagiza hivi watumishi wake: “Mwangalieni Amnoni, moyo wake utakapokuwa umechangamka kwa sababu ya divai, nitawaambia, ‘Muueni Amnoni!’ Ndipo mtakapomuua. Msiogope. Je, si mimi ndiye huwaamuru? Iweni imara na jasiri.” 29  Basi watumishi wa Absalomu wakamtendea Amnoni kama Absalomu alivyowaagiza; kisha wana wale wengine wa mfalme wakainuka, na kila mmoja wao akapanda nyumbu wake na kukimbia. 30  Walipokuwa njiani, habari hii ikamfikia Daudi: “Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, na hakuna hata mmoja aliyebaki hai.” 31  Ndipo mfalme akasimama, akararua mavazi yake, na kulala chini, nao watumishi wake wote walikuwa wamesimama kando yake na mavazi yao yalikuwa yameraruliwa. 32  Hata hivyo, Yehonadabu+ mwana wa Shimea,+ ndugu ya Daudi, akasema: “Bwana wangu usifikiri kwamba wamewaua wana wote wa mfalme, kwa maana Amnoni peke yake ndiye aliyekufa.+ Absalomu ndiye aliyeagiza auawe kwa sababu alikuwa amekusudia kufanya hivyo+ tangu Amnoni alipomwaibisha Tamari+ dada yake.+ 33  Sasa bwana wangu mfalme usisikilize habari hii inayosema, ‘Wana wote wa mfalme wamekufa’; ni Amnoni peke yake aliyekufa.” 34  Wakati huo, Absalomu akakimbia.+ Baadaye mlinzi akainua macho yake, akaona watu wengi wakija barabarani nyuma yake kando ya mlima. 35  Ndipo Yehonadabu+ akamwambia mfalme: “Tazama! Wana wa mfalme wamerudi, kama tu nilivyokwambia mimi mtumishi wako.” 36  Mara tu alipomaliza kuzungumza, wana wa mfalme wakaingia, wakilia kwa sauti; mfalme pia na watumishi wake wote wakalia kwa uchungu sana. 37  Lakini Absalomu akakimbia na kwenda kwa Talmai+ mwana wa Amihudi mfalme wa Geshuri. Daudi akamwombolezea mwana wake kwa siku nyingi. 38  Absalomu alipokimbia na kwenda Geshuri,+ alikaa huko kwa miaka mitatu. 39  Mwishowe Mfalme Daudi akatamani kwenda kumwona Absalomu, kwa maana alikuwa ametulia* baada ya kifo cha Amnoni.

Maelezo ya Chini

Au “mkate wa faraja.”
Au “mkate wa faraja.”
Au “Niletee mkate wa faraja.”
Au “lenye mapambo.”
Au “amepata faraja.”