Kitabu cha Pili cha Samweli 18:1-33

  • Absalomu ashindwa; kifo chake (1-18)

  • Daudi ajulishwa kuhusu kifo cha Absalomu (19-33)

  • Daudi amwombolezea Absalomu (1-4)

18  Kisha Daudi akawahesabu watu waliokuwa pamoja naye na kuweka juu yao wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia.+  Na Daudi akatuma theluthi ya wanaume chini ya amri ya* Yoabu,+ na theluthi nyingine chini ya amri ya Abishai+ mwana wa Seruya,+ ndugu ya Yoabu, na theluthi nyingine chini ya amri ya Itai+ Mgathi. Kisha mfalme akawaambia wanaume hao: “Mimi pia nitaenda pamoja nanyi.”  Lakini wakasema: “Usiende,+ kwa maana tukikimbia, hawatashughulika nasi;* na nusu yetu tukifa, hawatajali juu yetu, kwa maana thamani yako ni sawa na watu 10,000 miongoni mwetu.+ Kwa hiyo, litakuwa jambo bora zaidi ikiwa utatutumia msaada kutoka jijini.”  Mfalme akawaambia: “Nitafanya jambo lolote mnaloona ni jema zaidi.” Kwa hiyo mfalme akasimama karibu na lango la jiji na wanaume wote wakatoka wakiwa katika makundi ya mamia na maelfu.  Kisha mfalme akampa agizo hili Yoabu, Abishai, na Itai: “Mtendeeni kwa upole kijana Absalomu kwa ajili yangu.”+ Wanaume wote walimsikia mfalme akiwapa wakuu wote agizo hilo kuhusu Absalomu.  Wanaume hao wakaenda kupigana na Waisraeli, walipigana vita hivyo katika msitu wa Efraimu.+  Huko, watu wa Israeli+ wakashindwa na watumishi wa Daudi,+ na wanaume wengi wakauawa siku hiyo—wanaume 20,000.  Vita vikaenea katika eneo lote. Isitoshe, msitu uliwaua* watu wengi zaidi kuliko waliouawa kwa upanga siku hiyo.  Mwishowe Absalomu akakutana kwa ghafla na watumishi wa Daudi. Absalomu alikuwa amepanda juu ya nyumbu, na nyumbu huyo akaingia chini ya matawi yaliyosongamana ya mti mkubwa, na kichwa chake kikakwama kwenye mti huo hivi kwamba akabaki amening’inia hewani huku nyumbu wake akiendelea kukimbia. 10  Mtu fulani aliona jambo hilo na kumwambia Yoabu:+ “Jamani! Nimemwona Absalomu akining’inia kwenye mti mkubwa.” 11  Yoabu akamwambia hivi mtu huyo: “Ikiwa ulimwona, kwa nini hukumuua papo hapo na kumwangusha chini? Ikiwa ungefanya hivyo, ningefurahia kukupa vipande kumi vya fedha na mshipi.” 12  Lakini mtu huyo akamwambia Yoabu: “Hata kama ningepewa vipande 1,000 vya fedha, nisingeunyoosha mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme, kwa maana tulimsikia mfalme akikupa agizo hili, wewe na Abishai na Itai: ‘Haidhuru wewe ni nani, mlindeni kijana Absalomu.’+ 13  Nisingetii na hivyo kumuua,* jambo hilo lingejulikana kwa mfalme siku moja, nawe hungenilinda.” 14  Ndipo Yoabu akasema: “Sitaendelea kupoteza muda pamoja nawe!” Basi akachukua mikuki mitatu midogo* na kumchoma nayo Absalomu kwenye moyo alipokuwa angali hai akining’inia kwenye mti mkubwa. 15  Kisha watumishi kumi waliombebea Yoabu silaha wakaja na kumpiga Absalomu mpaka wakamuua.+ 16  Sasa Yoabu akapiga pembe, na watu wakarudi na kuacha kuwafuatia Waisraeli; Yoabu akawaambia wasiwafuatie. 17  Wakamchukua Absalomu na kumtupa ndani ya shimo kubwa msituni, nao wakarundika rundo kubwa sana la mawe juu yake.+ Kisha Waisraeli wote wakakimbia na kurudi katika nyumba zao. 18  Absalomu alipokuwa hai, alikuwa amechukua na kujisimamishia nguzo katika Bonde la* Mfalme,+ kwa maana alisema: “Sina mwana atakayeendeleza kumbukumbu ya jina langu.”+ Basi akaiita nguzo hiyo kwa jina lake, na tangu siku hiyo inaitwa Mnara wa Ukumbusho wa Absalomu. 19  Ahimaazi+ mwana wa Sadoki akasema: “Tafadhali, niruhusu nikimbie na kumpelekea mfalme habari hizi, kwa maana Yehova amemtendea kwa haki kwa kumweka huru kutoka mikononi mwa maadui wake.”+ 20  Lakini Yoabu akamwambia: “Hutapeleka habari hizi leo. Unaweza kuzipeleka siku nyingine, lakini hutampelekea mfalme habari hizi leo kwa sababu aliyekufa ni mwana wake mwenyewe.”+ 21  Kisha Yoabu akamwambia mtu fulani Mkushi:+ “Nenda, umwambie mfalme mambo uliyoona.” Kwa hiyo Mkushi huyo akamwinamia Yoabu na kukimbia. 22  Ahimaazi mwana wa Sadoki akamwambia tena Yoabu: “Liwalo na liwe, tafadhali niruhusu nikimbie na kumfuata yule Mkushi.” Hata hivyo, Yoabu akamwambia: “Mwanangu, kwa nini ukimbie wakati huna habari yoyote ya kupeleka?” 23  Lakini bado akasema: “Liwalo na liwe, acha nikimbie.” Yoabu akamwambia: “Kimbia!” Basi Ahimaazi akakimbia kupitia njia ya wilaya ya Yordani,* na hatimaye akampita huyo Mkushi. 24  Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili ya jiji,+ na mlinzi+ akapanda ukutani hadi juu ya paa la lango. Akatazama na kumwona mtu fulani akikimbia peke yake. 25  Kwa hiyo mlinzi huyo akaita kwa sauti na kumjulisha mfalme. Mfalme akasema: “Ikiwa yuko peke yake, analeta habari.” Mtu huyo alipozidi kukaribia, 26  mlinzi akamwona mtu mwingine akikimbia. Kwa hiyo mlinzi huyo akamwambia mlinda lango: “Tazama! Mtu mwingine anakimbia peke yake!” Mfalme akasema: “Huyo pia analeta habari.” 27  Mlinzi akasema: “Naona mtu wa kwanza akikimbia kama Ahimaazi+ mwana wa Sadoki,” basi mfalme akasema: “Huyo ni mtu mwema, naye analeta habari njema.” 28  Kisha Ahimaazi akamwambia hivi mfalme kwa sauti: “Mambo yote ni sawa!” Ndipo akamwinamia mfalme kifudifudi. Halafu akasema: “Abarikiwe Yehova Mungu wako, ambaye amewatia mikononi mwako wanaume waliokuasi* bwana wangu mfalme!”+ 29  Hata hivyo, mfalme akauliza: “Je, kijana Absalomu hajambo?” Ahimaazi akajibu: “Niliona vurugu kubwa Yoabu alipomtuma mtumishi wa mfalme na mimi mtumishi wako, lakini sikuelewa maana yake.”+ 30  Kwa hiyo mfalme akasema: “Sogea kando, simama hapa.” Basi akasogea kando na kusimama hapo. 31  Ndipo yule Mkushi akafika+ na kusema: “Bwana wangu mfalme na apokee habari hizi: Leo Yehova ametekeleza haki kwa kukuweka huru kutoka mikononi mwa wote waliokuasi.”+ 32  Lakini mfalme akamuuliza huyo Mkushi: “Je, kijana Absalomu hajambo?” Ndipo Mkushi akajibu: “Maadui wote wa bwana wangu mfalme na wote waliokuasi ili kukudhuru na wawe kama huyo kijana!”+ 33  Jambo hilo likamtaabisha mfalme, akapanda kwenye chumba kilicho paani juu ya lango na kulia, alikuwa akisema hivi huku akitembea: “Mwanangu Absalomu, mwanangu, mwanangu Absalomu! Laiti ningekufa badala yako, Absalomu mwanangu, mwanangu!”+

Maelezo ya Chini

Tnn., “mkono wa.”
Tnn., “hawataweka moyo wao juu yetu.”
Tnn., “uliwala.”
Au “Ikiwa ningeitendea nafsi yake kwa hila.”
Au labda, “vishale.” Tnn., “fito za chuma.”
Au “Nchi Tambarare ya Chini ya.”
Tnn., “ile wilaya.”
Tnn., “walioinua mkono wao dhidi yako.”