Kitabu cha Pili cha Samweli 20:1-26
20 Sasa palikuwa na mfanya fujo fulani aliyeitwa Sheba,+ mwana wa Bikri, Mbenjamini. Alipiga pembe+ na kusema: “Hatuna ushirika wowote na Daudi, na hatuna urithi wowote katika mwana wa Yese.+ Enyi Waisraeli, kila mtu aende kwa miungu* yake!”+
2 Basi wanaume wote wa Israeli wakaacha kumfuata Daudi na kuanza kumfuata Sheba mwana wa Bikri;+ lakini wanaume wa Yuda wakashikamana na mfalme wao, kuanzia Yordani mpaka Yerusalemu.+
3 Mfalme Daudi alipofika nyumbani kwake* huko Yerusalemu,+ aliwachukua wale masuria kumi aliokuwa amewaacha waitunze nyumba yake,+ akawaweka ndani ya nyumba chini ya ulinzi. Aliwapa chakula, lakini hakulala nao.+ Walibaki kifungoni mpaka siku walipokufa, nao waliishi kama wajane, ingawa mume wao alikuwa hai.
4 Sasa mfalme akamwambia Amasa:+ “Waite wanaume wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe pia unapaswa kuwepo.”
5 Kwa hiyo Amasa akaenda kuwaita wanaume wa Yuda, lakini alichelewa kurudi wakati alioambiwa arudi.
6 Ndipo Daudi akamwambia Abishai:+ “Huenda Sheba+ mwana wa Bikri atatuletea madhara makubwa zaidi kuliko Absalomu.+ Wachukue watumishi wangu mimi bwana wako umfuatie, ili asipate majiji yenye ngome na kutuponyoka.”
7 Basi wanaume wa Yoabu,+ Wakerethi, Wapelethi,+ na wanaume wote mashujaa wakaenda kumfuatia; wakaondoka Yerusalemu ili kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
8 Walipokaribia jiwe kubwa lililoko Gibeoni,+ Amasa+ akaja kuwapokea. Sasa Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya vita, naye alikuwa ametia upanga katika ala yake na kuufungia kiunoni. Aliposogea mbele, upanga huo ukaanguka.
9 Yoabu akamuuliza Amasa: “Je, hali yako ni njema ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wa kulia kana kwamba anataka kumbusu.
10 Amasa hakuchukua tahadhari kuhusiana na upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, basi Yoabu akamchoma tumboni kwa upanga huo,+ na matumbo yake yakamwagika ardhini. Hakuhitaji kumchoma tena; alikufa alipochomwa mara moja. Kisha Yoabu na ndugu yake Abishai wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.
11 Mmoja wa vijana wa Yoabu akasimama karibu na Amasa na kusema: “Yeyote anayemuunga mkono Yoabu na yeyote ambaye ni wa Daudi, na amfuate Yoabu!”
12 Wakati huo wote Amasa alikuwa akigaagaa kwenye damu yake katikati ya barabara. Kijana huyo alipoona kwamba watu wote walikuwa wakisimama hapo, akamwondoa Amasa barabarani na kumpeleka shambani. Kisha akatupa vazi juu yake, kwa sababu aliona kwamba kila mtu aliyefika mahali alipokuwa alisimama.
13 Baada ya kumwondoa barabarani, wanaume wote walimfuata Yoabu ili kumfuatia Sheba+ mwana wa Bikri.
14 Sheba akapita miongoni mwa makabila yote ya Israeli mpaka jiji la Abeli la Beth-maaka.+ Wabikri wakakusanyika pamoja na kumfuata.
15 Yoabu na wanaume wake wakaja na kumzingira katika jiji la Abeli la Beth-maaka na kutengeneza boma kuzunguka jiji hilo, kwani lilikuwa ndani ya boma. Na wanaume wote waliokuwa pamoja na Yoabu walikuwa wakiuharibu ukuta ili kuuangusha chini.
16 Na mwanamke fulani mwenye hekima akasema hivi kwa sauti kutoka jijini: “Sikilizeni wanaume, sikilizeni! Tafadhali, mwambieni Yoabu aje hapa, ili niongee naye.”
17 Basi Yoabu akamkaribia, kisha mwanamke huyo akamuuliza: “Je, wewe ni Yoabu?” Akamjibu: “Ndiyo.” Ndipo mwanamke huyo akamwambia: “Yasikilize maneno yangu mimi kijakazi wako.” Yoabu akasema: “Ninasikiliza.”
18 Mwanamke huyo akaendelea kusema: “Zamani walikuwa wakisema, ‘Acheni watafute ushauri kule Abeli, na hivyo ndivyo walivyotatua matatizo.’
19 Mimi ni mmojawapo wa watu wanaopenda amani na waaminifu katika Israeli. Unataka kuliharibu jiji ambalo ni kama mama katika Israeli. Kwa nini uangamize* urithi wa Yehova?”+
20 Yoabu akamjibu hivi: “Ni jambo nisiloweza kamwe kuwazia kwamba niliangamize na kuliharibu.
21 Sivyo ilivyo. Lakini mtu fulani anayeitwa Sheba+ mwana wa Bikri kutoka eneo lenye milima la Efraimu+ amemwasi* Mfalme Daudi. Mkimtoa nje mtu huyo, nitaondoka jijini.” Ndipo mwanamke huyo akamwambia Yoabu: “Haya! Utatupiwa kichwa chake ukutani!”
22 Mara moja mwanamke huyo mwenye hekima akaenda kuzungumza na watu wote, nao wakamkata kichwa Sheba mwana wa Bikri na kukitupa kwa Yoabu. Basi Yoabu akapiga pembe, nao wakatawanyika kutoka kwenye jiji hilo, kila mmoja akarudi nyumbani kwake;+ naye Yoabu akarudi Yerusalemu kwa mfalme.
23 Yoabu alikuwa mkuu wa jeshi lote la Israeli;+ Benaya+ mwana wa Yehoyada+ alikuwa mkuu wa Wakerethi na Wapelethi.+
24 Adoramu+ alikuwa msimamizi wa wale walioandikishwa kufanya kazi ya kulazimishwa; na Yehoshafati+ mwana wa Ahiludi alifanya kazi ya kuweka kumbukumbu.
25 Sheva alikuwa mwandishi; Sadoki+ na Abiathari+ walikuwa makuhani.
26 Na Ira, Myairi, akawa pia mhudumu mkuu* wa Daudi.