Ayubu 19:1-29

  • Jibu la Ayubu (1-29)

    • Akataa kukemewa na “rafiki” zake (1-6)

    • Asema kwamba ameachwa (13-19)

    • “Mkombozi wangu yuko hai” (25)

19  Ayubu akajibu:   “Mtaendelea kunikasirisha* mpaka lini,+Na kuniponda kwa maneno?+   Mmenikemea* mara kumi sasa;Mnanitesa bila aibu.+   Na ikiwa kwa kweli nilifanya kosa,Ni kosa langu mimi mwenyewe.   Ikiwa mnasisitiza kujikweza juu yangu,Mkidai kwamba mna haki ya kunishutumu,   Basi, jueni kwamba Mungu ndiye amenipotosha,Naye ameninasa katika wavu wake wa kuwindia.   Tazameni! Naendelea kulia kwa sauti, ‘Ukatili!’ lakini sijibiwi;+Naendelea kulilia msaada, lakini hakuna haki.+   Ameziba kijia changu kwa ukuta wa mawe, siwezi kupita;Amezifunika njia zangu kwa giza.+   Amenivua utukufu wanguNa kunivua taji kichwani. 10  Hunibomoa kila upande na kuniangamiza;Anang’oa tumaini langu kama mti. 11  Hasira yake huwaka dhidi yangu,Naye huniona kuwa adui yake.+ 12  Majeshi yake hukusanyika na kunizingira,Nayo hupiga kambi kuzunguka hema langu. 13  Ndugu zangu wenyewe amewafukuza mbali nami,Na wale wanaonijua wamegeuka na kuniacha.+ 14  Rafiki zangu wa karibu* wametoweka,Na wale niliowajua vema wamenisahau.+ 15  Wageni walio nyumbani mwangu+ na vijakazi wangu wananiona kuwa mgeni;Mimi ni mgeni machoni pao. 16  Ninamwita mtumishi wangu, lakini hajibu;Namsihi kwa kinywa changu anihurumie. 17  Pumzi yangu mwenyewe inamchukiza mke wangu,+Nami ni uvundo kwa ndugu* zangu wenyewe. 18  Hata watoto wachanga wananidharau;Ninaposimama, wanaanza kunifanyia mzaha. 19  Rafiki zangu wote wa karibu wananichukia,+Na wale niliowapenda wamenigeuka.+ 20  Mifupa yangu inashikamana na ngozi yangu na mwili wangu,+Nami ninaponyoka kwa ngozi ya meno yangu. 21  Nionyesheni rehema, rafiki zangu, nionyesheni rehema,Kwa maana mkono wa Mungu mwenyewe umenigusa.+ 22  Kwa nini mnaendelea kunitesa kama Mungu anavyonitesa,+Mkinishambulia bila kuacha?*+ 23  Laiti maneno yangu yangeandikwa,Laiti yangeandikwa katika kitabu! 24  Laiti yangechongwa milele kwenye mwamba,Kwa kalamu ya chuma na risasi! 25  Kwa maana najua vizuri kwamba mkombozi wangu+ yuko hai;Atakuja baadaye na kuinuka juu ya dunia.* 26  Baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi,Nikiwa bado hai, nitamwona Mungu, 27  Ambaye mimi mwenyewe nitamwona,Ambaye macho yangu mwenyewe yatamwona, si ya mwingine.+ Lakini ndani kabisa ninahisi nimelemewa!* 28  Kwa maana mnauliza, ‘Tunamtesa kwa njia gani?’+ Kwa maana mimi ndiye mzizi wa tatizo hili. 29  Ninyi wenyewe ogopeni upanga,+Kwa kuwa upanga huwaadhibu wakosaji;Mnapaswa kujua kwamba kuna mwamuzi.”+

Maelezo ya Chini

Au “kuikasirisha nafsi yangu.” Angalia Kamusi.
Au “Mmenitukana.”
Au “Watu wangu wa ukoo.”
Tnn., “wana wa tumbo langu la uzazi,” yaani, tumbo lililonibeba (tumbo la mama yangu).
Tnn., “Na hamtosheki na mwili wangu?”
Tnn., “juu ya (kwenye) mavumbi.”
Au “Figo zangu zimeacha kufanya kazi.”