Ayubu 39:1-30
39 “Je, unajua mbuzi wa milimani huzaa wakati gani?+
Je, umewahi kuwatazama paa wakizaa watoto wao?+
2 Je, wewe huhesabu miezi ambayo wanabeba mimba?
Je, unajua wakati wanapozaa?
3 Wao huchuchumaa wanapozaa watoto wao,Na uchungu wao wa kuzaa huisha.
4 Watoto wao hupata nguvu na kukua mbugani;Huenda zao na hawarudi.
5 Ni nani aliyemwacha huru punda mwitu,+Na ni nani aliyemfungua kamba punda mwitu?
6 Nimelifanya jangwa tambarare kuwa makao yakeNa nchi yenye chumvi kuwa makazi yake.
7 Yeye hudharau vurugu za mji;Hasikii kelele za mtu anayemwongoza.
8 Hutangatanga milimani, akitafuta malisho,Akitafuta mmea wowote wa kijani.
9 Je, fahali mwitu yuko tayari kukutumikia?+
Je, atalala zizini mwako* usiku?
10 Je, utamfunga fahali mwitu kwa kamba ili alime,Au, je, atakufuata ili alime* bondeni?
11 Je, utazitumaini nguvu zake nyingiNa kumwacha afanye kazi zako ngumu?
12 Je, utamtegemea akuletee mavuno yako,*Na je, atayakusanya kwenye uwanja wako wa kupuria?
13 Mabawa ya mbuni hupigapiga kwa shangwe,Lakini, je, mabawa na manyoya yake yanaweza kulinganishwa na ya korongo?+
14 Kwa maana yeye huacha mayai yake ardhini,Na kuyapasha joto mavumbini.
15 Yeye husahau kwamba mguu fulani unaweza kuyavunjaAu kwamba mnyama wa mwituni anaweza kuyakanyaga.
16 Huwatendea wanawe kwa ukatili, kana kwamba si wake;+Haogopi kwamba huenda kazi yake ngumu ikawa ya bure.
17 Kwa maana Mungu amemnyima* hekimaNaye hajamgawia uelewaji.
18 Lakini anapoinuka na kupigapiga mabawa yake,Humcheka farasi na yule aliyempanda.
19 Je, ni wewe unayempa farasi nguvu zake?+
Je, unamvika shingoni manyoya marefu yanayotikisika?
20 Je, unaweza kumfanya aruke kama nzige?
Mkoromo wake wa maringo unatisha.+
21 Yeye hukwangua ardhi bondeni na kushangilia kwa nguvu;+Hukimbia kwenda vitani.*+
22 Huicheka hofu na haogopi chochote.+
Harudi nyuma kwa sababu ya upanga.
23 Podo la mishale hutoa sauti kando yake,Mkuki na fumo humetameta.
24 Husonga mbele* huku akitetemeka kwa msisimko,Hawezi kusimama tuli anaposikia* mlio wa pembe.
25 Pembe inapolia, husema, ‘Aha!’
Hunusa vita kutoka mbali sanaNa kusikia kelele za makamanda na kelele za vita.+
26 Je, ni kwa uelewaji wako kwamba kipanga huruka,Akiyatandaza mabawa yake kuelekea kusini?
27 Au, je, ni kwa agizo lako kwamba tai hupaa juu+Na kujenga kiota chake juu sana,+
28 Na kulala usiku kucha juu ya jabali,Akiishi kwenye ngome yake juu ya mwamba uliochongoka?*
29 Akiwa hapo yeye hutafuta chakula;+Macho yake hutazama mbali sana.
30 Makinda yake hufyonza damu;Na penye mzoga, ndipo alipo.”+