Ayubu 5:1-27
5 “Ita, tafadhali! Je, kuna yeyote anayekujibu?
Ni mtakatifu gani utakayemlilia?
2 Kwa maana kinyongo kitamuua mpumbavu,Na wivu utamwangamiza mjinga.
3 Nimemwona mpumbavu akitia mizizi,Lakini kwa ghafla makao yake yanalaaniwa.
4 Wanawe hawana usalama wowote,Nao hupondwa kwenye lango la jiji,+ na hakuna yeyote wa kuwaokoa.
5 Mwenye njaa hula anachovuna,Hukichukua hata katikati ya miiba,Na mtego umetegwa ili kunasa mali zao.
6 Kwa maana mambo yenye kudhuru hayaoti mavumbini,Na taabu haichipuki ardhini.
7 Kwa maana mwanadamu huzaliwa ili ataabike,Hilo ni hakika kama cheche za moto zinavyoruka juu.
8 Lakini mimi ningemsihi Mungu,Nami ningewasilisha kesi yangu kwa Mungu,
9 Kwa Yule anayetenda mambo makuu na yasiyochunguzika,Mambo yenye kustaajabisha yasiyohesabika.
10 Yeye huleta mvua dunianiNa kupeleka maji mashambani.
11 Humwinua juu mtu wa hali ya chini,Humwinua aliyehuzunika na kumwokoa.
12 Huvuruga njama za wenye hila,Ili kazi ya mikono yao isifanikiwe.
13 Huwanasa wenye hekima katika ujanja wao wenyewe,+Hivi kwamba mipango ya watu werevu huvurugika.
14 Wao hukutana na giza wakati wa mchana,Nao hupapasa-papasa wakati wa adhuhuri kana kwamba ni usiku.
15 Huokoa kutokana na upanga wa kinywa chao,Humwokoa maskini kutoka katika mkono wa mwenye nguvu,
16 Hivi kwamba kuna tumaini kwa mtu wa hali ya chini,Lakini kinywa cha uovu hufumbwa.
17 Tazama! Mwenye furaha ni mtu ambaye Mungu humkaripia;Basi usikatae nidhamu ya Mweza-Yote!
18 Kwa maana yeye husababisha maumivu, lakini hufunga jeraha;Huvunja, lakini huponya kwa mikono yake.
19 Atakuokoa katika misiba sita,Hata wa saba hautakudhuru.
20 Wakati wa njaa kali atakukomboa kutoka katika kifo,Na kutoka katika nguvu za upanga wakati wa vita.
21 Utalindwa dhidi ya mashambulizi ya ulimi,+Nawe hutaogopa uharibifu utakapokuja.
22 Utacheka maangamizi na njaa,Wala hutawaogopa wanyama wa mwituni walio duniani.
23 Kwa maana mawe ya shambani hayatakudhuru,*Na wanyama wa mwituni wataishi nawe kwa amani.
24 Utajua kwamba hema lako liko salama,*Na hakuna kitakachokosekana utakapokagua malisho yako.
25 Utakuwa na watoto wengi,Na wazao wako watakuwa wengi kama mimea duniani.
26 Utaingia kaburini ukiwa bado na nguvu,Kama masuke ya nafaka yanayokusanywa wakati wa mavuno.
27 Tazama! Tumechunguza jambo hili, na ndivyo lilivyo.
Sikiliza na ulikubali.”