Danieli 3:1-30

  • Sanamu ya dhahabu ya Mfalme Nebukadneza (1-7)

    • Walazimishwa kuabudu sanamu (4-6)

  • Waebrania watatu washtakiwa kwa kukataa kuabudu (8-18)

    • “Hatutaiabudu miungu yako” (18)

  • Watupwa kwenye tanuru la moto (19-23)

  • Waokolewa kimuujiza kutoka motoni (24-27)

  • Mfalme amsifu Mungu wa Waebrania (28-30)

3  Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu yenye urefu wa mikono 60* na upana wa mikono 6.* Akaisimamisha kwenye nchi tambarare ya Dura katika mkoa wa* Babiloni.  Kisha Mfalme Nebukadneza akatuma ujumbe ili kuwakusanya maliwali, wasimamizi, magavana, washauri, watunza-hazina, waamuzi, mahakimu, na wasimamizi wote wa mikoa* waje kwenye sherehe ya kuzindua sanamu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa amesimamisha.  Basi maliwali, wasimamizi, magavana, washauri, watunza-hazina, waamuzi, mahakimu, na wakuu wote wa mikoa* wakakusanyika kwa ajili ya sherehe ya kuzindua sanamu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa amesimamisha. Nao wakasimama mbele ya sanamu iliyosimamishwa na Nebukadneza.  Mpiga mbiu akatangaza hivi kwa sauti kubwa: “Enyi watu wa makabila, mataifa, na lugha zote, mnaamriwa kwamba,  wakati mtakaposikia sauti ya pembe, zumari, zeze, kinubi cha pembe tatu, kinanda, zumari-tete, na ala nyingine zote za muziki, lazima mwanguke chini na kuabudu sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza amesimamisha.  Yeyote ambaye hataanguka chini na kuabudu atatupwa mara moja katika tanuru lenye moto mkali.”+  Basi watu wote waliposikia sauti ya pembe, zumari, zeze, kinubi cha pembe tatu, kinanda, zumari-tete, na ala nyingine zote za muziki, watu wa makabila, mataifa, na lugha zote wakaanguka chini na kuiabudu sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa amesimamisha.  Wakati huo Wakaldayo fulani wakajitokeza na kuwashtaki* Wayahudi.  Wakamwambia Mfalme Nebukadneza: “Ee mfalme, na uishi milele. 10  Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri kwamba kila mtu anayesikia sauti ya pembe, zumari, zeze, kinubi cha pembe tatu, kinanda, zumari-tete, na ala nyingine zote za muziki, anapaswa kuanguka chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu; 11  na kwamba yeyote ambaye hataanguka chini na kuiabudu anapaswa kutupwa katika tanuru lenye moto mkali.+ 12  Lakini kuna Wayahudi fulani uliowaweka kuwa wasimamizi wa mkoa wa* Babiloni: Shadraki, Meshaki, na Abednego.+ Wanaume hawa hawajakuheshimu wewe, Ee mfalme. Hawaabudu miungu yako, na wanakataa kuabudu sanamu ya dhahabu ambayo umesimamisha.” 13  Ndipo Nebukadneza, kwa hasira kali sana, akaagiza Shadraki, Meshaki, na Abednego waletwe mbele yake. Basi wanaume hao wakaletwa mbele ya mfalme. 14  Nebukadneza akawauliza: “Shadraki, Meshaki, na Abednego, je, ni kweli kabisa kwamba hamwabudu miungu yangu+ na kwamba mnakataa kuabudu sanamu ya dhahabu ambayo nimesimamisha? 15  Basi mtakaposikia sauti ya pembe, zumari, zeze, kinubi cha pembe tatu, kinanda, zumari-tete, na ala nyingine zote za muziki, mkiwa tayari kuanguka chini na kuabudu sanamu ambayo nimeitengeneza, ni sawa. Lakini mkikataa kuabudu, mtatupwa mara moja katika tanuru lenye moto mkali. Na ni mungu gani anayeweza kuwaokoa kutoka mikononi mwangu?”+ 16  Shadraki, Meshaki, na Abednego wakamjibu mfalme: “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kukujibu kuhusiana na jambo hili. 17  Ikiwa ni lazima iwe hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia anaweza kutuokoa kutoka katika tanuru hilo lenye moto mkali, Ee mfalme, na kutuokoa kutoka mikononi mwako.+ 18  Lakini hata asipotuokoa, Ee mfalme, ujue kwamba hatutaiabudu miungu yako wala kuabudu sanamu ya dhahabu uliyosimamisha.”+ 19  Ndipo Nebukadneza akawakasirikia vikali Shadraki, Meshaki, na Abednego hivi kwamba sura yake ikabadilika * kuwaelekea, akaagiza tanuru liongezwe moto mara saba kuliko kawaida.⁠ 20  Akawaagiza wanaume fulani hodari katika jeshi lake wawafunge Shadraki, Meshaki, na Abednego na kuwatupa katika tanuru hilo lenye moto mkali. 21  Basi wanaume hao wakafungwa wakiwa na majoho yao, mavazi, kofia, na nguo zao nyingine, nao wakatupwa katika tanuru hilo lenye moto mkali. 22  Kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa kali sana na tanuru lilikuwa na moto mkali isivyo kawaida, miali ya moto huo iliwaua wanaume waliowapeleka Shadraki, Meshaki, na Abednego. 23  Lakini wanaume hao watatu, Shadraki, Meshaki, na Abednego, wakaanguka ndani ya tanuru hilo lenye moto mkali wakiwa wamefungwa. 24  Ndipo Mfalme Nebukadneza akaogopa, akainuka haraka na kuwauliza maofisa wake wakuu: “Je, hatukuwafunga wanaume watatu na kuwatupa ndani ya moto?” Wakamjibu mfalme: “Naam, Ee mfalme.” 25  Mfalme akasema: “Tazama! Naona wanaume wanne wakitembeatembea katikati ya moto wakiwa huru, nao hawajapatwa na madhara, na yule wa nne anaonekana kama mwana wa miungu.” 26  Nebukadneza akaukaribia mlango wa lile tanuru lenye moto mkali na kusema: “Shadraki, Meshaki, na Abednego, ninyi watumishi wa Mungu Aliye Juu Zaidi,+ tokeni nje, mje hapa!” Shadraki, Meshaki, na Abednego wakatoka katikati ya moto. 27  Na maliwali, wasimamizi, magavana, na maofisa wakuu wa mfalme waliokuwa wamekusanyika mahali hapo+ wakaona kwamba moto haukuwadhuru* wanaume hao;+ hakuna unywele hata mmoja wa vichwa vyao uliokuwa umeungua, majoho yao hayakuwa yamebadilika, na miili yao haikuwa hata na harufu ya moto. 28  Ndipo Nebukadneza akatangaza hivi: “Na asifiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki, na Abednego,+ aliyemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Walimtegemea yeye na kutenda kinyume cha amri ya mfalme na walikuwa tayari kufa* badala ya kumtumikia au kumwabudu mungu mwingine yeyote isipokuwa Mungu wao wenyewe.+ 29  Kwa hiyo ninaagiza kwamba watu wa kabila lolote, taifa, au lugha ambao watasema jambo lolote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki, na Abednego, wanapaswa kukatwa vipandevipande, na nyumba zao zinapaswa kugeuzwa kuwa vyoo vya umma;* kwa maana hakuna mungu mwingine yeyote anayeweza kuokoa kama huyu.”+ 30  Kisha mfalme akawapandisha vyeo* Shadraki, Meshaki, na Abednego katika mkoa wa* Babiloni.+

Maelezo ya Chini

Mita 27 hivi (futi 88). Angalia Nyongeza B14.
Mita 2.7 hivi (futi 8.8). Angalia Nyongeza B14.
Au “wilaya ya utawala ya.”
Au “wilaya za utawala.”
Au “wilaya za utawala.”
Au “kuwachongea.”
Au “wilaya ya utawala ya.”
Au “mtazamo wake ukabadilika kabisa.”
Au “haukuwazidi nguvu.”
Au “na kutoa miili yao.”
Au labda, “maeneo ya takataka; marundo ya mavi.”
Tnn., “akawafanikisha.”
Au “wilaya ya utawala ya.”