Danieli 6:1-28
6 Mfalme Dario aliona vema kuwaweka maliwali 120 kusimamia ufalme wake wote.+
2 Juu yao kulikuwa na maofisa watatu wakuu, Danieli+ alikuwa mmoja wao; na maliwali+ walikuwa wakiwapelekea habari, ili mfalme asipate hasara.
3 Sasa, Danieli alijidhihirisha kuwa tofauti na wale maofisa wengine wakuu na maliwali, kwa maana roho isiyo ya kawaida ilikuwa ndani yake,+ na mfalme alikusudia kumkweza juu ya ufalme wote.
4 Wakati huo maofisa wakuu na maliwali walikuwa wakitafuta msingi fulani wa kumshtaki Danieli kuhusiana na mambo ya serikali,* lakini hawakuweza kupata msingi wowote wa kumshtaki wala ufisadi wowote, kwa sababu alikuwa mwenye kutegemeka, naye hakupatikana kamwe akiwa mzembe wala mfisadi.
5 Ndipo wanaume hao wakasema: “Hatutapata msingi wowote wa kumshtaki huyu Danieli, isipokuwa tutafute msingi wa kumshtaki kuhusiana na sheria ya Mungu wake.”+
6 Basi maofisa hao wakuu na maliwali wakaenda wakiwa kikundi kwa mfalme na kumwambia: “Ee Mfalme Dario, uishi milele.
7 Maofisa wote wa mfalme, wasimamizi, maliwali, maofisa wakuu wa mfalme, na magavana, wameshauriana ili mfalme atoe amri na kutangaza marufuku, kwamba kwa siku 30 mtu yeyote atakayemwomba mungu yeyote au mwanadamu isipokuwa wewe, Ee mfalme, anapaswa kutupwa ndani ya shimo la simba.+
8 Na sasa, Ee mfalme, itoe amri hiyo na kuitia sahihi,+ ili isiweze kubadilishwa kulingana na sheria ya Wamedi na Waajemi, ambayo haiwezi kufutwa.”+
9 Kwa hiyo Mfalme Dario akatia sahihi amri hiyo na marufuku hayo.
10 Lakini mara tu Danieli alipojua kwamba amri hiyo imetiwa sahihi alienda nyumbani kwake, na madirisha ya chumba chake kilichokuwa darini yalikuwa yamefunguliwa kuelekea Yerusalemu.+ Na mara tatu kwa siku alipiga magoti na kusali na kumsifu Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya kwa ukawaida kabla ya mambo hayo.
11 Wakati huo wanaume hao wakaingia kwa kishindo na kumkuta Danieli akimwomba na kumsihi Mungu wake apate kibali mbele zake.
12 Kwa hiyo wakaenda kwa mfalme na kumkumbusha kuhusu marufuku aliyotangaza: “Je, hukutia sahihi marufuku ukisema kwamba kwa siku 30 mtu yeyote atakayemwomba mungu yeyote au mwanadamu yeyote isipokuwa wewe, Ee mfalme, anapaswa kutupwa ndani ya shimo la simba?” Mfalme akasema: “Hivyo ndivyo ilivyo kulingana na sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kufutwa.”+
13 Mara moja wakamwambia mfalme: “Danieli, mmoja wa watu waliohamishwa kutoka Yuda+ hajakuheshimu wewe, Ee mfalme, wala marufuku uliyotia sahihi, badala yake anasali mara tatu kwa siku.”+
14 Mara tu mfalme aliposikia hivyo, alihuzunika sana, akajaribu kutafuta njia ya kumwokoa Danieli; alifanya kila jitihada ya kumwokoa mpaka jua likatua.
15 Mwishowe wanaume hao wakaenda mbele ya mfalme wakiwa kikundi na kumwambia: “Ee mfalme, zingatia kwamba sheria ya Wamedi na Waajemi inasema kwamba marufuku yoyote au amri yoyote iliyowekwa na mfalme haiwezi kubadilishwa.”+
16 Basi mfalme akatoa agizo, nao wakamleta Danieli na kumtupa ndani ya shimo la simba.+ Mfalme akamwambia Danieli: “Mungu wako unayemtumikia daima, atakuokoa.”
17 Kisha jiwe likaletwa na kuwekwa kwenye mwingilio* wa shimo hilo, naye mfalme akalitia muhuri kwa pete yake ya muhuri na kwa pete ya muhuri ya wakuu wake ili uamuzi kumhusu Danieli usibadilishwe hata kidogo.
18 Kisha mfalme akaenda kwenye jumba lake la kifalme. Akafunga usiku kucha na kukataa kutumbuizwa kwa njia yoyote,* naye akashindwa kulala usingizi.*
19 Hatimaye, alfajiri na mapema, mfalme aliondoka na kwenda haraka kwenye lile shimo la simba.
20 Alipokaribia shimo hilo, akamwita Danieli kwa sauti ya huzuni. Mfalme akamuuliza Danieli: “Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je, Mungu wako unayemtumikia daima ameweza kukuokoa kutoka kwa simba hao?”
21 Mara moja Danieli akamjibu mfalme: “Ee mfalme, uishi milele.
22 Mungu wangu alimtuma malaika wake akafunga vinywa vya simba,+ nao hawajanidhuru,+ kwa sababu sikupatikana na hatia mbele zake; wala sijakutendea jambo lolote baya, Ee mfalme.”
23 Mfalme akafurahi sana, akaamuru Danieli atolewe ndani ya lile shimo. Danieli alipotolewa shimoni, hakuwa amepatwa na madhara yoyote, kwa sababu alikuwa amemtumaini Mungu wake.+
24 Kisha mfalme akatoa agizo, na wanaume waliokuwa wamemshtaki* Danieli wakaletwa, nao wakatupwa ndani ya lile shimo la simba, pamoja na wake zao na watoto wao. Kabla hawajafika chini shimoni, simba waliwashinda nguvu na kuvunjavunja mifupa yao yote.+
25 Kisha Mfalme Dario akawaandikia watu wa makabila yote, mataifa, na lugha wanaokaa katika dunia yote:+ “Muwe na amani tele!
26 Ninatoa agizo kwamba katika kila eneo la ufalme wangu, watu wanapaswa kutetemeka kwa woga mbele za Mungu wa Danieli.+ Kwa maana yeye ndiye Mungu aliye hai naye huishi milele. Ufalme wake hautaangamizwa kamwe, na utawala wake ni wa* milele.+
27 Yeye huokoa,+ naye hufanya ishara na maajabu mbinguni na duniani,+ kwa sababu alimwokoa Danieli kutoka katika makucha ya simba.”
28 Basi Danieli huyo akafanikiwa katika ufalme wa Dario+ na katika ufalme wa Koreshi Mwajemi.+