Esta 5:1-14

  • Esta aenda mbele ya mfalme (1-8)

  • Hasira na kiburi cha Hamani (9-14)

5  Siku ya tatu+ Esta akavaa mavazi yake ya kifalme na kusimama katika ua wa ndani wa nyumba ya* mfalme, sehemu iliyotazamana na nyumba ya mfalme, naye mfalme alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha ufalme ndani ya nyumba ya mfalme akitazama langoni.  Mara tu mfalme alipomwona Malkia Esta akiwa amesimama kwenye ua, akafurahi kumwona, naye mfalme akamnyooshea Esta fimbo yake ya ufalme ya dhahabu+ iliyokuwa mkononi mwake. Basi Esta akakaribia na kuigusa ncha ya fimbo hiyo.  Mfalme akamuuliza: “Malkia Esta, kuna nini? Niambie unachotaka. Hata ukiomba nusu ya ufalme wangu utapewa!”  Esta akajibu: “Mfalme akipenda na aje leo pamoja na Hamani+ kwenye karamu ambayo nimemwandalia.”  Basi Mfalme akawaambia watumishi wake: “Mwambieni Hamani aje haraka, kama Esta anavyoomba.” Basi, mfalme na Hamani wakaenda kwenye karamu ambayo Esta alikuwa ameandaa.  Karamu ya divai ilipokuwa ikiendelea, mfalme akamwambia Esta: “Una ombi gani? Utapewa utakachoomba! Na unataka nini? Hata ukiomba nusu ya ufalme wangu, utapewa!”+  Esta akamjibu: “Hili ndilo ombi langu na jambo ninalotaka,  Ikiwa nimepata kibali chako Ee mfalme, nawe mfalme ukipenda kutimiza ombi langu na kunipa ninachotaka, naomba mfalme uje pamoja na Hamani kwenye karamu ambayo nitawaandalia kesho; na kesho nitafanya kama unavyosema mfalme.”  Siku hiyo Hamani aliondoka akiwa na shangwe na uchangamfu moyoni. Lakini Hamani alipomwona Mordekai katika lango la mfalme na kutambua kwamba hakusimama wala kutetemeka alipomwona, Hamani alimkasirikia sana Mordekai.+ 10  Hata hivyo, Hamani akajizuia na kwenda nyumbani kwake. Kisha akawatuma watu wawaite marafiki zake na pia Zereshi+ mke wake. 11  Hamani akajigamba kuhusu utajiri wake mwingi, wanawe wengi,+ na jinsi mfalme alivyompandisha cheo na kumkweza juu ya wakuu na watumishi wa mfalme.+ 12  Hamani akaendelea kusema: “Isitoshe, Malkia Esta hakumwalika mtu mwingine yeyote isipokuwa mimi nimsindikize mfalme kwenye karamu aliyoandaa.+ Kesho pia amenialika mimi ili niwe naye pamoja na mfalme.+ 13  Lakini mambo hayo yote hayaniridhishi ninapoendelea kumwona Mordekai Myahudi akiwa ameketi kwenye lango la mfalme.” 14  Ndipo Zereshi mke wake na marafiki zake wote wakamwambia: “Agiza mti wenye kimo cha mikono 50* usimamishwe. Kisha asubuhi umwambie mfalme kwamba Mordekai anapaswa kutundikwa juu yake.+ Halafu uende na mfalme kujifurahisha kwenye karamu.” Pendekezo hilo likampendeza Hamani, kwa hiyo akaagiza mti huo usimamishwe.

Maelezo ya Chini

Au “jumba la.”
Karibu mita 22.3 (futi 73). Angalia Nyongeza B14.