Esta 7:1-10
7 Basi mfalme na Hamani+ wakaja kwenye karamu ya Malkia Esta.
2 Mfalme akamuuliza tena Esta siku ya pili wakati wa karamu ya divai: “Malkia Esta, una ombi gani? Utapewa unachoomba. Unataka nini? Hata ukiomba nusu ya ufalme wangu utapewa!”+
3 Malkia Esta akajibu: “Ikiwa nimepata kibali chako, Ee mfalme, nawe mfalme ukipenda, naomba uuokoe uhai wangu,* na pia uhai wa watu wangu.+
4 Kwa maana tumeuzwa,+ mimi na watu wangu, tuangamizwe, tuuawe, na kufutiliwa mbali.+ Kama tungeuzwa tuwe watumwa wa kiume na wa kike, ningekaa kimya. Lakini msiba huu haufai, kwa sababu utamletea mfalme hasara.”
5 Ndipo mfalme Ahasuero akamuuliza Malkia Esta: “Ni nani huyo, na yuko wapi mwanamume aliyethubutu kufanya jambo hilo?”
6 Esta akasema: “Mpinzani na adui ni huyu Hamani mwovu.”
Hamani akaogopa sana kwa sababu ya mfalme na malkia.
7 Mfalme akasimama kwa hasira na kutoka kwenye karamu ya divai, akaenda kwenye bustani ya jumba la mfalme, lakini Hamani akasimama ili kumsihi Malkia Esta auokoe uhai wake,* kwa maana alijua mfalme alikuwa ameazimia kumwadhibu.
8 Mfalme aliporudi kutoka kwenye bustani ya jumba la mfalme na kuingia katika nyumba ya karamu ya divai na kumwona Hamani akiwa amejiangusha kwenye kochi, mahali alipokuwa Esta. Mfalme akasema: “Je, sasa anataka kumbaka malkia katika nyumba yangu mwenyewe?” Mara tu maneno hayo yalipotoka kinywani mwa mfalme, wakaufunika uso wa Hamani.
9 Harbona,+ mmoja wa maofisa wa makao ya mfalme akasema: “Pia Hamani alitengeneza mti kwa ajili ya Mordekai+ aliyetoa habari iliyomwokoa mfalme.+ Mti huo wenye kimo cha mikono 50* umesimamishwa nyumbani kwa Hamani.” Ndipo mfalme akasema: “Mtundikeni juu yake.”
10 Basi wakamtundika Hamani kwenye mti aliokuwa ameutengeneza ili kumtundika Mordekai juu yake, na hasira ya mfalme ikatulia.
Maelezo ya Chini
^ Au “nafsi yangu.”
^ Au “nafsi yake.”
^ Karibu mita 22.3 (futi 73). Angalia Nyongeza B14.