Ezekieli 32:1-32

  • Wimbo wa huzuni kuhusu Farao na Misri (1-16)

  • Misri kuzikwa pamoja na wasiotahiriwa (17-32)

32  Na katika mwaka wa 12, mwezi wa 12, siku ya kwanza ya mwezi huo, neno la Yehova lilinijia tena likisema:  “Mwana wa binadamu, mwimbie wimbo wa huzuni* mfalme Farao wa Misri, nawe umwambie, ‘Ulikuwa kama mwanasimba* mwenye nguvu wa mataifa, Lakini umenyamazishwa. Ulikuwa kama mnyama mkubwa sana wa baharini,+ ukitibua maji katika mito yako, Ukivuruga maji kwa miguu yako na kuchafua mito.’*   Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova anasema hivi: ‘Nitautumia umati wa mataifa mengi kutandaza wavu wangu juu yako, Nao watakukokota katika wavu wangu wa kukokotwa.   Nitakuacha nchini; Nitakutupa uwanjani. Nitawafanya ndege wote wa angani watue juu yako, Nami nitawashibisha wanyama wa mwituni wa dunia nzima kwa nyama yako.+   Nitaitupa nyama yako juu ya milima Na kuyajaza mabonde mabaki yako.+   Nitailowesha nchi kwa damu yako inayobubujika, mpaka juu ya milima, Nayo itajaa kwenye vijito.’*   ‘Na utakapozimwa nitazifunika mbingu na kuzitia giza nyota zake. Nitalifunika jua kwa mawingu, Na mwezi hautatoa nuru yake.+   Kwa sababu yako, nitaitia giza mianga yote inayong’aa mbinguni, Nami nitaifunika nchi yako kwa giza,’ asema Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova.   ‘Nitaitaabisha mioyo ya mataifa mengi nitakapowapeleka watu wako waliotekwa katika mataifa mengine, Katika nchi ambazo huzijui.+ 10  Nitayafanya mataifa mengi yashikwe na hofu, Na wafalme wao watatetemeka kwa woga kwa sababu yako nitakapoutikisa upanga wangu mbele yao. Wataendelea kutetemeka, kila mmoja akihofia uhai wake, Siku utakayoanguka.’ 11  Kwa maana Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova anasema hivi: ‘Upanga wa mfalme wa Babiloni utakushambulia.+ 12  Nitaufanya umati wako uuawe kwa panga za mashujaa hodari, Walio wakatili zaidi kati ya mataifa, wote.+ Watashusha chini kiburi cha Misri, na umati wake wote utaangamizwa.+ 13  Nitaiangamiza mifugo yake yote kando ya maji yake mengi,+ Na hakuna mguu wa mwanadamu au ukwato wa mnyama wa kufugwa utakaoyachafua tena.’+ 14  ‘Wakati huo nitayasafisha kabisa maji yao, Nami nitafanya mito yao itiririke kama mafuta,’ asema Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova. 15  ‘Nitakapoifanya nchi ya Misri iwe mahame na ukiwa, nchi iliyoporwa vitu vyote vilivyoijaza,+ Nitakapowaua wakaaji wote walio ndani yake, Watalazimika kujua kwamba mimi ni Yehova.+ 16  Huu ni wimbo wa huzuni, na hakika watu watauimba; Mabinti wa mataifa watauimba. Wataiimbia nchi ya Misri na umati wake wote,’ asema Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova.” 17  Kisha katika mwaka wa 12, siku ya 15 ya mwezi huo, neno la Yehova lilinijia likisema: 18  “Mwana wa binadamu, uombolezee umati wa Misri nawe umshushe kwenye nchi iliyo chini, yeye na mabinti wa mataifa yenye nguvu, pamoja na wale wanaoshuka chini shimoni.* 19  “‘Unamzidi nani kwa urembo? Shuka chini, ulale na watu ambao hawajatahiriwa!’ 20  “‘Wataanguka miongoni mwa wale waliouawa kwa upanga.+ Ametiwa mikononi mwa upanga; mkokote pamoja na umati wake wote. 21  “‘Kutoka kwenye vina vya Kaburi* mashujaa hodari zaidi watazungumza naye na wasaidizi wake. Hakika watashuka chini na kulala kama watu ambao hawajatahiriwa, waliouawa kwa upanga. 22  Ashuru yuko huko pamoja na umati wake wote. Makaburi yao yamemzunguka, wote wameuawa kwa upanga.+ 23  Makaburi yake yamo katika vina vya shimo,* na umati wake umezunguka kaburi lake, wote wameuawa kwa upanga, kwa sababu walisababisha hofu katika nchi ya walio hai. 24  “‘Elamu+ yuko huko pamoja na umati wake wote kulizunguka kaburi lake, wote wakiwa wameuawa kwa upanga. Wameshuka chini bila kutahiriwa katika nchi iliyo chini, wale waliosababisha hofu katika nchi ya walio hai. Sasa watabeba aibu yao pamoja na wale wanaoshuka chini shimoni.* 25  Wamemtengenezea kitanda kati ya watu waliouawa, pamoja na umati wake wote kuzunguka makaburi yake. Wote hawajatahiriwa, na waliuawa kwa upanga, kwa sababu walisababisha hofu katika nchi ya walio hai; nao watabeba aibu yao pamoja na wale wanaoshuka chini shimoni.* Amewekwa miongoni mwa wale waliouawa. 26  “‘Watu wa Mesheki na Tubali+ na umati wao* wote wako huko. Makaburi yao yamemzunguka. Wote hawajatahiriwa, wamechomwa kwa upanga, kwa sababu walisababisha hofu katika nchi ya walio hai. 27  Je, hawatalala pamoja na mashujaa hodari waliouawa ambao hawajatahiriwa, ambao walishuka Kaburini* wakiwa na silaha zao za vita? Nao wataweka panga zao chini ya vichwa vyao* na dhambi zao kwenye mifupa yao, kwa sababu mashujaa hawa hodari walisababisha hofu katika nchi ya walio hai. 28  Lakini wewe, utapondwa miongoni mwa watu ambao hawajatahiriwa, nawe utalala pamoja na wale waliouawa kwa upanga. 29  “‘Edomu+ yuko huko, wafalme wake na wakuu wake wote, ambao ingawa walikuwa hodari, walilazwa miongoni mwa wale waliouawa kwa upanga; wao pia watalala na watu ambao hawajatahiriwa+ na pamoja na wale wanaoshuka chini shimoni.* 30  “‘Wakuu* wote wa kaskazini wako huko, pamoja na Wasidoni wote,+ ambao wameshuka kwa aibu pamoja na waliouawa, ingawa walisababisha hofu kwa nguvu zao. Watalala wakiwa hawajatahiriwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga nao watabeba aibu yao pamoja na wale wanaoshuka chini shimoni.* 31  “‘Farao atawaona hao wote, naye atafarijiwa kwa sababu ya mambo yote yaliyoupata umati wake;+ Farao na jeshi lake lote watauawa kwa upanga,’ asema Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova. 32  “‘Kwa kuwa alisababisha hofu katika nchi ya walio hai, Farao na umati wake wote watalazwa ili wapumzike pamoja na watu ambao hawajatahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga,’ asema Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova.”

Maelezo ya Chini

Tnn., “mito yao.”
Au “mwanasimba mwenye manyoya marefu shingoni.”
Au “wimbo wa maombolezo.”
Tnn., “Nawe utazijaza sakafu za vijito.”
Au “kaburini.”
Au “Sheoli.” Angalia Kamusi.
Au “kaburi.”
Au “kaburini.”
Au “kaburini.”
Tnn., “wake.”
Au “Sheoli.” Angalia Kamusi.
Huenda inarejelea mashujaa waliozikwa wakiwa na panga zao, kwa heshima ya kijeshi.
Au “kaburini.”
Au “Viongozi.”
Au “kaburini.”