Ezekieli 40:1-49

  • Ezekieli aletwa Israeli katika maono (1, 2)

  • Ezekieli aona hekalu kwenye maono (3, 4)

  • Nyua na malango (5-47)

    • Lango la nje la mashariki (6-16)

    • Ua wa nje; malango mengine (17-26)

    • Ua wa ndani na malango (27-37)

    • Vyumba vya utumishi wa hekaluni (38-46)

    • Madhabahu (47)

  • Ukumbi wa hekalu (48, 49)

40  Katika mwaka wa 25 wa uhamisho wetu,+ mwanzoni mwa mwaka, siku ya 10 ya mwezi, katika mwaka wa 14 baada ya jiji kuanguka,+ siku hiyohiyo mkono wa Yehova ulikuwa juu yangu, naye akanipeleka jijini.+  Kupitia maono kutoka kwa Mungu, alinileta katika nchi ya Israeli na kuniweka juu ya mlima mrefu sana,+ na juu yake kulikuwa na jengo lililoonekana kama jiji, upande wa kusini.  Aliponipeleka huko, niliona mtu fulani ambaye alionekana kama shaba.+ Alikuwa na kamba ya kitani na utete wa kupimia* mkononi mwake,+ naye alikuwa amesimama langoni.  Mtu huyo akaniambia: “Mwana wa binadamu, tazama kwa uangalifu, sikiliza kwa makini, na ukazie fikira* kila kitu ninachokuonyesha, kwa maana uliletwa hapa kwa sababu hiyo. Waambie watu wa nyumba ya Israeli kila kitu unachoona.”+  Nikaona ukuta uliozunguka nje ya hekalu.* Mkononi mwa mtu huyo kulikuwa na utete wa kupimia wenye urefu wa mikono sita (kila mkono ulikuwa umeongezwa urefu wa kiganja kimoja).* Akaanza kupima ukuta, nao ulikuwa na unene wa utete mmoja na urefu wake ulikuwa utete mmoja.  Kisha akaja kwenye lango lililotazama mashariki+ na kupanda ngazi zake. Alipopima kizingiti cha lango hilo, upana wake ulikuwa utete mmoja, na upana wa kile kizingiti kingine ulikuwa utete mmoja pia.  Kila chumba cha walinzi kilikuwa na urefu wa utete mmoja na upana wa utete mmoja, na kulikuwa na kipimo cha mikono mitano kati ya vyumba vya walinzi.+ Kipimo cha kizingiti cha lango kando ya ukumbi wa lango linalotazama upande wa ndani kilikuwa utete mmoja.  Alipima ukumbi wa lango kuelekea ndani, nao ulikuwa utete mmoja.  Kisha akapima ukumbi wa lango, nao ulikuwa mikono minane; na akapima nguzo zake za pembeni, nazo zilikuwa mikono miwili; na ukumbi wa lango ulikuwa upande uliotazama ndani. 10  Kulikuwa na vyumba vitatu vya walinzi katika kila upande wa lango la mashariki. Vyumba hivyo vitatu vilikuwa na ukubwa uleule, nazo nguzo za pembeni zilizokuwa pande zote mbili zilikuwa na ukubwa uleule. 11  Kisha akapima upana wa lango, nao ulikuwa mikono 10; na urefu wa lango ulikuwa mikono 13. 12  Eneo lililogawanywa lililokuwa mbele ya vyumba vya walinzi kila upande lilikuwa na kipimo cha mkono mmoja. Vyumba vya walinzi pande zote mbili vilikuwa mikono sita kila kimoja. 13  Kisha akapima lango kutoka kwenye paa la chumba kimoja cha mlinzi* mpaka kwenye paa la kile kingine, na upana wake ulikuwa mikono 25; mlango mmoja ulitazamana na mlango mwingine.+ 14  Kisha akapima nguzo za pembeni, ambazo zilikuwa na urefu wa mikono 60, pia nguzo za pembeni katika malango kuzunguka ua. 15  Urefu kutoka upande wa mbele wa lango mpaka mbele ya ukumbi upande wa ndani wa lango ulikuwa mikono 50. 16  Ndani ya lango, kila upande kwenye vyumba vya walinzi na pia kwenye nguzo zake za pembeni kulikuwa na madirisha yenye viunzi ambavyo ukubwa wake ulipungua kutoka nje kwenda ndani.+ Upande wa ndani wa kumbi ulikuwa pia na madirisha kila upande, na kulikuwa na michongo ya mitende+ kwenye nguzo za pembeni. 17  Kisha akanileta kwenye ua wa nje, nami nikaona vyumba vya kulia chakula,*+ na sakafu iliyozunguka ua. Kulikuwa na vyumba 30 vya kulia chakula kwenye ile sakafu. 18  Urefu wa sakafu iliyokuwa kando ya malango ulikuwa sawa na urefu wa malango—hiyo ilikuwa sakafu ya chini. 19  Kisha akapima umbali* kutoka mbele ya lango la chini mpaka kwenye uzio wa ua wa ndani. Ulikuwa mikono 100 upande wa mashariki na wa kaskazini. 20  Ua wa nje ulikuwa na lango lililotazama kaskazini, naye akapima urefu wake na upana wake. 21  Kulikuwa na vyumba vitatu vya walinzi kila upande. Nguzo zake za pembeni na ukumbi wake ulikuwa na vipimo sawa na lile lango la kwanza. Urefu wake ulikuwa mikono 50 na upana wake mikono 25. 22  Madirisha yake, ukumbi wake, na michongo yake ya mitende+ yalikuwa na ukubwa ulio sawa na yale ya lango la mashariki. Watu wangeweza kuyafikia kwa kupanda ngazi saba, na ukumbi wake ulikuwa mbele yake. 23  Kulikuwa na lango katika ua wa ndani lililotazamana na lango la kaskazini na lingine lililotazamana na lango la mashariki. Alipima urefu kutoka lango moja hadi lingine, nao ulikuwa mikono 100. 24  Kisha akanileta upande wa kusini, nami nikaona lango upande wa kusini.+ Akapima nguzo zake za pembeni na ukumbi wake, nazo zilikuwa na ukubwa ulio sawa na zile nyingine. 25  Kila upande na pia katika ukumbi wake kulikuwa na madirisha, kama madirisha yale mengine. Urefu wake ulikuwa mikono 50 na upana wa mikono 25. 26  Kulikuwa na ngazi saba zilizoelekea langoni,+ na ukumbi wake ulikuwa mbele yake. Nalo lilikuwa na michongo ya mitende kwenye nguzo zake za pembeni, mmoja kila upande. 27  Ua wa ndani ulikuwa na lango lililotazama upande wa kusini, akapima kuelekea kusini kutoka lango moja mpaka lingine, na urefu wake ulikuwa mikono 100. 28  Kisha akanileta kwenye ua wa ndani kupitia lango la kusini; alipolipima lango la kusini, lilikuwa na ukubwa sawa na yale malango mengine. 29  Vyumba vyake vya walinzi, nguzo zake za pembeni, na ukumbi wake ulikuwa na ukubwa sawa na malango mengine. Kulikuwa na madirisha kila upande na pia kwenye ukumbi. Urefu wake ulikuwa mikono 50 na upana wake mikono 25.+ 30  Kulikuwa na kumbi pande zote; zilikuwa na urefu wa mikono 25 na upana wa mikono 5. 31  Ukumbi wake ulitazama ua wa nje, na kulikuwa na michongo ya mitende kwenye nguzo zake za pembeni,+ na ngazi nane zilielekea kwenye lango hilo.+ 32  Aliponileta kwenye ua wa ndani kutoka mashariki, alilipima lango, nalo lilikuwa na ukubwa sawa na malango mengine. 33  Vyumba vyake vya walinzi, nguzo zake za pembeni, na ukumbi wake ulikuwa na ukubwa sawa na malango mengine, na kulikuwa na madirisha kila upande na pia kwenye ukumbi. Urefu wake ulikuwa mikono 50 na upana wake mikono 25. 34  Ukumbi wake ulitazama ua wa nje, na kulikuwa na michongo ya mitende kwenye nguzo zake mbili za pembeni, na ngazi nane zilielekea kwenye lango hilo. 35  Kisha akanileta kwenye lango la kaskazini+ naye akalipima; ukubwa wake ulikuwa sawa na malango mengine. 36  Vyumba vyake vya walinzi, nguzo zake za pembeni, na ukumbi wake ulikuwa sawa na malango mengine. Lango hilo lilikuwa na madirisha kila upande. Urefu wake ulikuwa mikono 50 na upana wa mikono 25. 37  Nguzo zake za pembeni zilitazama ua wa nje na kulikuwa na michongo ya mitende kwenye nguzo zake mbili za pembeni, na ngazi nane zilielekea kwenye lango hilo. 38  Kulikuwa na chumba cha kulia chakula pamoja na mlango wake karibu na nguzo za pembeni za malango, mahali ambapo dhabihu nzima za kuteketezwa zilioshewa.+ 39  Kulikuwa na meza mbili kila upande wa ukumbi wa lango ambapo wanyama wa dhabihu nzima za kuteketezwa walichinjiwa,+ na wa dhabihu za dhambi,+ na wa dhabihu za hatia.+ 40  Kwenye njia inayopanda kuelekea katika lango la kaskazini, kulikuwa na meza mbili nje ya lango. Kulikuwa pia na meza mbili upande ule mwingine wa ukumbi wa lango. 41  Kulikuwa na meza nne kila upande wa lango—meza nane kwa ujumla—ambapo wanyama wa dhabihu walichinjiwa. 42  Zile meza nne za dhabihu nzima za kuteketezwa zilitengenezwa kwa mawe yaliyochongwa. Zilikuwa na urefu wa mkono mmoja na nusu, upana wa mkono mmoja na nusu, na kimo cha mkono mmoja. Juu yake waliweka vifaa vilivyotumiwa kuwachinjia wanyama wa dhabihu za kuteketezwa na dhabihu nyingine. 43  Rafu zenye upana wa kiganja kimoja, zilifungwa kuzunguka pande zote za kuta za ndani; na nyama za dhabihu za zawadi ziliwekwa kwenye zile meza. 44  Kulikuwa na vyumba vya kulia chakula vya waimbaji nje ya lango la ndani;+ vilikuwa katika ua wa ndani karibu na lango la kaskazini, vikitazama upande wa kusini. Kulikuwa na chumba kingine cha kulia chakula karibu na lango la mashariki, kilitazama kaskazini. 45  Akaniambia: “Chumba hiki cha chakula kinachotazama upande wa kusini ni cha makuhani walio na jukumu la kutimiza utumishi wa hekaluni.+ 46  Chumba cha kulia chakula kinachotazama upande wa kaskazini ni cha makuhani walio na jukumu la kutimiza utumishi wa madhabahu.+ Hao ni wana wa Sadoki,+ Walawi waliopewa kazi ya kumkaribia Yehova ili kumhudumia.”+ 47  Kisha akapima ua wa ndani. Ulikuwa na urefu wa mikono 100 na upana wa mikono 100, mraba. Madhabahu ilikuwa mbele ya hekalu. 48  Kisha akanileta kwenye ukumbi wa hekalu,+ naye akapima nguzo ya pembeni ya ukumbi, nayo ilikuwa mikono mitano upande mmoja na mikono mitano upande wa pili. Upana wa lango ulikuwa mikono mitatu upande mmoja na mikono mitatu upande wa pili. 49  Ukumbi ulikuwa na urefu wa mikono 20 na upana wa mikono 11.* Watu walipanda ngazi ili kufika kwenye ukumbi huo. Kulikuwa na nguzo kwenye miimo ya pembeni, nguzo moja kila upande.+

Maelezo ya Chini

Tnn., “uweke moyo wako kwa.”
Tnn., “nyumba.” Neno “hekalu” linatumiwa katika sura ya 40-48 wakati ambapo linarejelea majengo ya hekalu au hekalu lenyewe.
Tnn., “utete wa kupimia wa mikono sita, mkono mmoja na kiganja kimoja.” Hiki ni kipimo cha mikono mirefu. Angalia Nyongeza B14.
Labda inarejelea sehemu ya juu ya ukuta wa chumba cha mlinzi.
Au “nikaona vyumba.”
Tnn., “upana.”
Au labda, “12.”