Ezekieli 48:1-35
48 “Haya ndiyo majina ya makabila hayo, kuanzia mpaka wa kaskazini: Sehemu ya Dani+ inapita kwenye njia ya Hethloni hadi Lebo-hamathi*+ hadi Hasar-enani, kwenye mpaka wa Damasko kuelekea kaskazini kando ya Hamathi;+ nayo inaanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.
2 Sehemu ya Asheri+ iko kwenye mpaka wa Dani, kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.
3 Sehemu ya Naftali+ iko kwenye mpaka wa Asheri, kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.
4 Sehemu ya Manase+ iko kwenye mpaka wa Naftali, kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.
5 Sehemu ya Efraimu iko kwenye mpaka wa Manase,+ kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.
6 Sehemu ya Rubeni iko kwenye mpaka wa Efraimu,+ kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.
7 Sehemu ya Yuda iko kwenye mpaka wa Rubeni,+ kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.
8 Kwenye mpaka wa Yuda, kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi, mchango mtakaoweka kando unapaswa kuwa na upana wa mikono 25,000,*+ nao unapaswa kulingana na urefu wa zile sehemu nyingine za makabila kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi. Patakatifu patakuwa katikati yake.
9 “Mchango mtakaoweka kando kwa ajili ya Yehova utakuwa na urefu wa mikono 25,000 na upana wa mikono 10,000.
10 Huu ndio utakaokuwa mchango mtakatifu kwa ajili ya makuhani.+ Upande wa kaskazini utakuwa mikono 25,000, upande wa magharibi 10,000, na upande wa mashariki 10,000, na upande wa kusini 25,000. Patakatifu pa Yehova patakuwa katikati yake.
11 Patakuwa pa makuhani waliotakaswa kutoka kwa wana wa Sadoki,+ wale walioshughulikia majukumu niliyowapa na ambao hawakuniacha wakati Waisraeli na Walawi waliponiacha.+
12 Watapokea sehemu ya mchango wa nchi hiyo iliyowekwa kando kuwa kitu kitakatifu kabisa, kwenye mpaka wa Walawi.
13 “Kando tu ya eneo la makuhani, Walawi watakuwa na sehemu yenye urefu wa mikono 25,000, na upana wa mikono 10,000. (Urefu wote utakuwa 25,000 na upana 10,000.)
14 Hawapaswi kuuza, kubadilisha, au kumpa mtu mwingine eneo lolote la sehemu hii bora ya nchi, kwa maana ni kitu kitakatifu kwa Yehova.
15 “Eneo linalobaki lenye upana wa mikono 5,000 lililo kando ya mpaka wenye urefu wa mikono 25,000 litakuwa la matumizi ya kawaida ya jiji,+ kwa ajili ya makao na malisho. Jiji litakuwa katikati yake.+
16 Hivi ndivyo vipimo vya jiji: Mpaka wa kaskazini mikono 4,500, mpaka wa kusini 4,500, mpaka wa mashariki 4,500, na mpaka wa magharibi 4,500.
17 Malisho ya jiji yatakuwa mikono 250 upande wa kaskazini, 250 upande wa kusini, 250 upande wa mashariki, na 250 upande wa magharibi.
18 “Urefu wa sehemu inayobaki utalingana na mchango mtakatifu,+ upande wa mashariki mikono 10,000, na upande wa magharibi 10,000. Italingana na mchango mtakatifu na mazao yake yatakuwa chakula cha wale wanaolitumikia jiji.
19 Wale wanaolitumikia jiji kutoka katika makabila yote ya Israeli watailima sehemu hiyo.+
20 “Mchango mzima ni mikono 25,000 mraba. Mnapaswa kuuweka kando uwe mchango mtakatifu pamoja na miliki ya jiji.
21 “Sehemu itakayobaki pande zote za mchango mtakatifu na wa miliki ya jiji itakuwa mali ya kiongozi.+ Itakuwa kando ya mipaka yenye urefu wa mikono 25,000 iliyo upande wa mashariki na magharibi wa ule mchango. Italingana na sehemu zinazopakana, na itakuwa ya kiongozi. Mchango mtakatifu na patakatifu pa hekalu patakuwa katikati yake.
22 “Miliki ya Walawi na miliki ya jiji itakuwa kati ya mali ya kiongozi. Eneo la kiongozi litakuwa kati ya mpaka wa Yuda+ na Benjamini.
23 “Na kuhusu makabila yanayobaki, sehemu ya Benjamini inaanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.+
24 Sehemu ya Simeoni iko kando ya mpaka wa Benjamini,+ kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.
25 Sehemu ya Isakari+ iko kando ya mpaka wa Simeoni, kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.
26 Sehemu ya Zabuloni iko kando ya mpaka wa Isakari,+ kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.+
27 Sehemu ya Gadi iko kando ya mpaka wa Zabuloni,+ kuanzia mpaka wa mashariki hadi mpaka wa magharibi.
28 Mpaka wa kusini ulio kando ya mpaka wa Gadi utaanzia Tamari+ hadi kwenye maji ya Meribath-kadeshi,+ hadi kwenye lile Korongo*+ na kwenda hadi kwenye ile Bahari Kuu.*
29 “Hii ndiyo nchi ambayo mnapaswa kuigawa iwe urithi wa makabila ya Israeli,+ na hizo ndizo zitakazokuwa sehemu zao,”+ asema Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova.
30 “Hizi ndizo zitakazokuwa njia za kutokea za jiji: Kipimo cha upande wa kaskazini kitakuwa mikono 4,500.+
31 Malango ya jiji yatapewa majina ya makabila ya Israeli. Kati ya malango matatu ya kaskazini, kuna lango moja la Rubeni, moja la Yuda, na moja la Lawi.
32 Upande wa mashariki utakuwa na urefu wa mikono 4,500, na malango matatu: lango moja la Yosefu, lango moja la Benjamini, na lango moja la Dani.
33 Upande wa kusini utakuwa na urefu wa mikono 4,500, nao utakuwa na malango matatu: lango moja la Simeoni, lango moja la Isakari, na lango moja la Zabuloni.
34 Upande wa magharibi utakuwa na urefu wa mikono 4,500, nao utakuwa na malango matatu: lango moja la Gadi, lango moja la Asheri, na lango moja la Naftali.
35 “Urefu kuzunguka jiji lote utakuwa mikono 18,000. Na jina la jiji hilo kuanzia siku hiyo na kuendelea litakuwa, Yehova Yupo Hapo.”+
Maelezo ya Chini
^ Au “njia ya kuingia Hamathi.”
^ Hiki ni kipimo cha mikono mirefu. Angalia Nyongeza B14.
^ Yaani, Bahari ya Mediterania.
^ Yaani, Korongo la Misri.