Hesabu 22:1-41

  • Balaki amkodi Balaamu (1-21)

  • Punda wa Balaamu aongea (22-41)

22  Kisha Waisraeli wakaondoka na kupiga kambi kwenye jangwa tambarare la Moabu ng’ambo ya Yordani kutoka Yeriko.+  Sasa Balaki+ mwana wa Sipori aliona mambo yote ambayo Waisraeli waliwatendea Waamori,  na Wamoabu wakawaogopa sana Waisraeli, kwa sababu walikuwa wengi sana; naam, Wamoabu wakafadhaika kwa hofu kwa sababu ya Waisraeli.+  Basi Wamoabu wakawaambia wazee wa Midiani:+ “Sasa umati huu utaramba eneo letu lote kama ng’ombe dume anavyokula nyasi shambani.” Balaki mwana wa Sipori ndiye aliyekuwa mfalme wa Moabu wakati huo.  Aliwatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori huko Pethori,+ karibu na Mto Efrati katika nchi yake. Alimwambia hivi: “Sasa, kuna watu ambao wametoka Misri. Wamejaa kila mahali duniani,*+ na wanakaa papa hapa karibu nami.  Basi, tafadhali, njoo uwalaani watu hawa kwa niaba yangu,+ kwa maana wana nguvu kuliko mimi. Huenda nikawashinda na kuwafukuza kutoka nchini, kwa maana najua vema kwamba yule unayembariki amebarikiwa na yule unayemlaani amelaaniwa.”  Basi wazee wa Moabu na wazee wa Midiani wakachukua malipo ya uaguzi* na kwenda kumwona Balaamu,+ wakamwambia maneno ya Balaki.  Ndipo Balaamu akawaambia: “Laleni hapa usiku wa leo, nami nitawajulisha jambo lolote ambalo Yehova ataniambia.” Hivyo wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu.  Kisha Mungu akamtokea Balaamu na kumuuliza:+ “Wanaume hawa walio pamoja nawe ni nani?” 10  Balaamu akamwambia Mungu wa kweli: “Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amenitumia ujumbe akisema, 11  ‘Watu wanaotoka Misri wamejaa kila mahali duniani.* Sasa njoo uwalaani kwa niaba yangu.+ Huenda nikapigana nao na kuwafukuza.’” 12  Lakini Mungu akamwambia Balaamu: “Usiende na wanaume hawa. Usiwalaani watu hao, kwa maana wamebarikiwa.”+ 13  Balaamu akaamka asubuhi na kuwaambia wakuu wa Balaki: “Rudini katika nchi yenu, kwa maana Yehova amenikataza kwenda pamoja nanyi.” 14  Kwa hiyo wakuu wa Moabu wakaondoka, wakarudi kwa Balaki na kumwambia: “Balaamu amekataa kuja pamoja nasi.” 15  Hata hivyo, Balaki akawatuma tena wakuu wengine, wengi zaidi na wenye kuheshimika zaidi kuliko wale wa kwanza. 16  Wakafika kwa Balaamu na kumwambia: “Balaki mwana wa Sipori anasema hivi: ‘Tafadhali, usiruhusu chochote kikuzuie kuja kwangu, 17  kwa maana nitakuthawabisha sana, nami nitafanya chochote utakachoniambia. Njoo tafadhali, uwalaani watu hawa kwa niaba yangu.’” 18  Lakini Balaamu akawaambia watumishi wa Balaki: “Hata Balaki akinipa nyumba yake mwenyewe iliyojaa fedha na dhahabu, siwezi kukiuka jambo lolote ambalo Yehova Mungu wangu ameniagiza nifanye, liwe jambo dogo au kubwa.+ 19  Lakini tafadhalini, laleni hapa usiku wa leo pia, ili nijue Yehova ataniambia jambo gani lingine.”+ 20  Kisha Mungu akamtokea Balaamu usiku na kumwambia: “Ikiwa wanaume hao wamekuja kukuita, nenda pamoja nao. Lakini utasema tu maneno nitakayokwambia.”+ 21  Basi Balaamu akaamka asubuhi, akaweka matandiko juu ya punda wake na kwenda pamoja na wakuu wa Moabu.+ 22  Lakini Mungu akakasirika sana kwa sababu Balaamu alikuwa akienda, na malaika wa Yehova akasimama njiani ili kumzuia. Sasa Balaamu alikuwa amepanda juu ya punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. 23  Punda huyo alipomwona malaika wa Yehova amesimama njiani akiwa ameshika upanga uliochomolewa, alijaribu kutoka njiani ili aingie shambani. Lakini Balaamu akaanza kumpiga punda huyo ili arudi njiani. 24  Ndipo malaika wa Yehova akasimama kwenye kijia chembamba katikati ya mashamba mawili ya mizabibu, na kulikuwa na ukuta wa mawe upande huu na huu wa kijia hicho. 25  Punda alipomwona malaika wa Yehova, akaanza kujisukumiza ukutani na kuubana mguu wa Balaamu ukutani, na Balaamu akaanza kumpiga tena. 26  Sasa malaika wa Yehova akaenda mbele tena na kusimama mahali pembamba ambapo hapakuwa na nafasi ya kugeuka kulia au kushoto. 27  Punda alipomwona malaika wa Yehova, akalala chini Balaamu akiwa mgongoni, basi Balaamu akakasirika sana na kuendelea kumpiga punda kwa fimbo yake. 28  Mwishowe Yehova akamfanya punda huyo aongee,*+ akamuuliza Balaamu: “Nimekutendea nini hivi kwamba umenipiga mara tatu?”+ 29  Balaamu akamjibu hivi punda huyo: “Ni kwa sababu umenifanya mjinga. Ningekuwa na upanga mkononi, ningekuua!” 30  Kisha punda akamwambia Balaamu: “Je, mimi si punda wako ambaye amekubeba maisha yako yote mpaka leo? Je, nimewahi kukutendea hivi?” Balaamu akajibu: “Hapana!” 31  Ndipo Yehova akayafungua macho ya Balaamu,+ naye akamwona malaika wa Yehova amesimama njiani akiwa ameshika upanga uliochomolewa. Papo hapo Balaamu akainama chini na kusujudu. 32  Malaika wa Yehova akamwambia: “Kwa nini umempiga punda wako mara tatu? Mimi mwenyewe nimekuja kukuzuia kwa sababu njia yako haipatani na mapenzi yangu.+ 33  Punda aliniona na kujaribu kunikwepa mara hizo tatu.+ Kama hangenikwepa ningekuwa nimekuua na kumwacha yeye akiwa hai.” 34  Balaamu akamwambia malaika wa Yehova: “Nimetenda dhambi, kwa sababu sikujua kwamba ni wewe uliyesimama njiani ili kunizuia. Na sasa ikiwa hufurahii jambo hili, mimi nitarudi.” 35  Lakini malaika wa Yehova akamwambia Balaamu: “Nenda pamoja na wanaume hao, lakini utasema tu maneno nitakayokwambia.” Basi Balaamu akaendelea na safari pamoja na wakuu wa Balaki. 36  Balaki aliposikia kwamba Balaamu amefika, alitoka nje mara moja kumpokea katika jiji la Moabu, kwenye ukingo wa Arnoni, katika mpaka wa Moabu. 37  Balaki akamuuliza Balaamu: “Je, sikuwatuma wajumbe wakuite uje kwangu? Kwa nini hukuja? Je, ulidhani siwezi kukuthawabisha kwelikweli?”+ 38  Balaamu akamjibu hivi Balaki: “Sasa nimekuja kwako. Lakini, je, nitaruhusiwa kusema jambo lolote? Ninaweza kusema tu maneno ambayo Mungu anatia kinywani mwangu.”+ 39  Kwa hiyo Balaamu akaenda pamoja na Balaki, wakafika Kiriath-husothi. 40  Balaki akatoa dhabihu za ng’ombe na kondoo, naye akamgawia Balaamu na wakuu waliokuwa pamoja naye. 41  Asubuhi Balaki akamchukua Balaamu na kwenda naye Bamoth-baali; akiwa huko aliweza kuwaona Waisraeli wote.+

Maelezo ya Chini

Au “nchini.”
Au “ubashiri.”
Au “nchini.”
Tnn., “akakifungua kinywa cha huyo punda jike.”