Hesabu 23:1-30

  • Maneno ya kwanza ya kishairi ya Balaamu (1-12)

  • Maneno ya pili ya kishairi ya Balaamu (13-30)

23  Kisha Balaamu akamwambia Balaki: “Jenga madhabahu saba mahali hapa,+ nawe unitayarishie ng’ombe dume saba na kondoo dume saba.”  Mara moja Balaki akafanya kama Balaamu alivyomwambia. Kisha Balaki na Balaamu wakatoa dhabihu ya ng’ombe dume mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.+  Halafu Balaamu akamwambia Balaki: “Kaa hapa karibu na dhabihu yako ya kuteketezwa, nami nitaenda. Labda Yehova atawasiliana nami. Jambo lolote atakalonifunulia, nitakwambia.” Basi akaenda juu ya kilima kilicho wazi.  Ndipo Mungu akawasiliana na Balaamu,+ Balaamu akamwambia: “Nilijenga safu za madhabahu saba na kutoa dhabihu ya ng’ombe dume mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.”  Yehova akatia maneno haya katika kinywa cha Balaamu:+ “Rudi kwa Balaki, na hili ndilo utakalosema.”  Basi akarudi na kumkuta Balaki na wakuu wote wa Moabu wakiwa wamesimama karibu na dhabihu yake ya kuteketezwa.  Kisha akasema maneno haya ya kishairi:+ “Balaki mfalme wa Moabu amenileta kutoka Aramu,+Kutoka katika milima ya mashariki: ‘Njoo umlaani Yakobo kwa niaba yangu. Naam, njoo uwashutumu Waisraeli.’+   Ninawezaje kuwalaani watu ambao Mungu hajawalaani? Ninawezaje kuwashutumu wale ambao Yehova hajawashutumu?+   Kutoka juu ya miamba ninawaona,Na kutoka vilimani ninawatazama. Wanaishi peke yao kama taifa;+Hawajioni kuwa sawa na mataifa mengine.+ 10  Ni nani anayeweza kuhesabu chembe za mavumbi ya Yakobo+Au hata kuhesabu robo ya Waisraeli? Acha nife kifo cha watu wanyoofu,Na mwisho wangu uwe kama wao.” 11  Ndipo Balaki akamwambia Balaamu: “Kwa nini umenitendea hivi? Nilikuleta ili uwalaani maadui wangu, lakini badala yake umewabariki tu.”+ 12  Balaamu akasema: “Je, sipaswi kusema neno lolote ambalo Yehova anatia kinywani mwangu?”+ 13  Balaki akamwambia: “Tafadhali, twende mahali pengine ambapo unaweza kuwaona. Utaona baadhi yao; hutawaona wote. Ukiwa huko walaani kwa niaba yangu.”+ 14  Kwa hiyo akampeleka kwenye uwanja wa Sofimu, juu ya Pisga,+ naye akajenga madhabahu saba na kutoa dhabihu ya ng’ombe dume mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.+ 15  Kisha Balaamu akamwambia Balaki: “Kaa hapa karibu na dhabihu yako ya kuteketezwa ninapoenda pale kuwasiliana Naye.” 16  Basi Yehova akawasiliana na Balaamu na kutia neno hili kinywani mwake:+ “Rudi kwa Balaki, na hili ndilo utakalosema.” 17  Basi akarudi na kumkuta Balaki akisubiri karibu na dhabihu yake ya kuteketezwa, na wakuu wa Moabu walikuwa pamoja naye. Balaki akamuuliza: “Yehova amesema nini?” 18  Kisha Balaamu akasema maneno haya ya kishairi:+ “Inuka, Balaki, usikilize. Nisikilize, ewe mwana wa Sipori. 19  Mungu si mwanadamu anayesema uwongo,+Wala si binadamu anayebadili nia yake.*+ Akisema jambo, je, hatalitenda? Akinena jambo, je, hatalitimiza?+ 20  Tazama! Nimeletwa ili nibariki;Sasa Yeye amebariki,+ nami siwezi kubadili.+ 21  Havumilii nguvu zozote za uchawi dhidi ya Yakobo,Wala haruhusu taabu yoyote impate Israeli. Yehova Mungu wake yuko pamoja nao,+Nao humsifu kwa sauti kubwa kuwa mfalme wao. 22  Mungu anawatoa Misri.+ Yeye ni kama pembe za fahali mwitu.+ 23  Kwa maana hakuna ishara za msiba dhidi ya Yakobo,+Wala hakuna uaguzi* wowote dhidi ya Israeli.+ Sasa inaweza kusemwa hivi kumhusu Yakobo na Israeli: ‘Tazameni mambo ambayo Mungu ametenda!’ 24  Watu hawa watainuka kama simba,Na kama simba, watajiinua.+ Hawatalala chini mpaka wale mawindoNa kunywa damu ya waliouawa.” 25  Ndipo Balaki akamwambia Balaamu: “Ikiwa huwezi kamwe kuwalaani, basi usiwabariki pia.” 26  Balaamu akamwambia Balaki: “Je, sikukwambia, ‘Nitafanya mambo yote ambayo Yehova anasema’?”+ 27  Ndipo Balaki akamwambia Balaamu: “Tafadhali njoo nikupeleke mahali pengine. Labda Mungu wa kweli atakubali uwalaani kwa niaba yangu kutoka mahali hapo.”+ 28  Basi Balaki akampeleka Balaamu juu ya Mlima Peori, unaoelekeana na Yeshimoni.*+ 29  Kisha Balaamu akamwambia Balaki: “Jenga madhabahu saba mahali hapa, nawe unitayarishie ng’ombe dume saba na kondoo dume saba.”+ 30  Kwa hiyo Balaki akafanya kama Balaamu alivyomwambia, naye akatoa dhabihu ya ng’ombe dume mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.

Maelezo ya Chini

Au “anayejuta.”
Au “ubashiri.”
Au labda, “jangwa; nyika.”