Isaya 36:1-22

  • Senakeribu ashambulia Yuda (1-3)

  • Rabshake amdhihaki Yehova (4-22)

36  Katika mwaka wa 14 wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru+ alipanda kuja kuyashambulia majiji yote yenye ngome ya Yuda na kuyateka.+  Kisha mfalme wa Ashuru akamtuma Rabshake*+ pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi+ kwenda kwa Mfalme Hezekia kule Yerusalemu. Wakajipanga karibu na mfereji wa kidimbwi cha juu,+ kwenye barabara kuu ya uwanja wa mfuaji wa nguo.+  Ndipo Eliakimu+ mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba,* Shebna+ aliyekuwa mwandishi, na Yoa mwana wa Asafu aliyefanya kazi ya kuweka kumbukumbu wakaenda nje kukutana naye.  Basi Rabshake akawaambia: “Tafadhali, mwambieni hivi Hezekia: ‘Mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, anauliza, “Ujasiri wako unategemea msingi gani?+  Unasema, ‘Nina mbinu na nguvu za kupigana vita,’ lakini hayo ni maneno matupu. Unamtumaini nani, hivi kwamba unathubutu kuniasi?+  Tazama! Unautumaini msaada wa utete huu uliopondeka, Misri, ambao mtu yeyote akiuegemea utamchoma kiganja na kukitoboa. Hivyo ndivyo Farao mfalme wa Misri alivyo kwa wote wanaomtumaini.+  Nawe ukiniambia, ‘Tunamtumaini Yehova Mungu wetu,’ je, si yeye ndiye ambaye mahali pake pa juu na madhabahu zake zimeondolewa na Hezekia,+ huku akiwaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, ‘Mnapaswa kuinama mbele ya madhabahu hii’?”’+  Basi sasa, tafadhali, fanya mkataba huu pamoja na bwana wangu mfalme wa Ashuru:+ nitakupa farasi 2,000 ikiwa unaweza kupata wapanda farasi wa kutosha idadi hiyo.  Basi, unawezaje kumzuia hata gavana mmoja aliye mdogo zaidi kati ya watumishi wa bwana wangu, huku ukiitumaini nchi ya Misri ili upate magari ya vita na wapanda farasi? 10  Sasa je, nimepanda kuja kuishambulia nchi hii ili kuiharibu bila kupewa idhini na Yehova? Yehova mwenyewe aliniambia, ‘Panda uende kuishambulia nchi hii na kuiharibu.’” 11  Ndipo Eliakimu na Shebna+ na Yoa wakamwambia Rabshake:+ “Tafadhali, zungumza nasi watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu*+ kwa maana tunaweza kuielewa; usizungumze nasi kwa lugha ya Wayahudi huku watu walio ukutani wakisikia.”+ 12  Lakini Rabshake akasema: “Je, bwana wangu amenituma niwaambie ninyi na bwana wenu tu maneno haya? Je, sipaswi kuwaambia pia wanaume wanaoketi ukutani, wale watakaokula kinyesi chao wenyewe na kunywa mkojo wao wenyewe pamoja nanyi?” 13  Kisha Rabshake akasimama na kusema hivi kwa sauti kubwa kwa lugha ya Wayahudi:+ “Sikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru.+ 14  Mfalme anasema hivi, ‘Msikubali Hezekia awadanganye, kwa maana hawezi kuwaokoa.+ 15  Na msikubali Hezekia awafanye mumtumaini Yehova+ mkisema: “Kwa hakika Yehova atatuokoa, na jiji hili halitatiwa mikononi mwa mfalme wa Ashuru.” 16  Msimsikilize Hezekia, kwa maana mfalme wa Ashuru anasema hivi: “Fanyeni amani pamoja nami na mjisalimishe,* na kila mmoja wenu atakula matunda ya mzabibu wake mwenyewe na matunda ya mtini wake mwenyewe na kunywa maji kutoka katika tangi lake mwenyewe, 17  mpaka nitakapokuja na kuwapeleka katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe,+ nchi yenye nafaka na divai mpya, nchi yenye mikate na mashamba ya mizabibu. 18  Msikubali Hezekia awapotoshe akisema, ‘Yehova atatuokoa.’ Je, kuna mungu yeyote kati ya miungu ya mataifa ambaye amewahi kuiokoa nchi yake kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru?+ 19  Iko wapi miungu ya Hamathi na Arpadi?+ Iko wapi miungu ya Sefarvaimu?+ Na je, imeokoa Samaria kutoka mikononi mwangu?+ 20  Ni mungu yupi kati ya miungu yote ya nchi hizi ambaye ameokoa nchi yake kutoka mikononi mwangu, hivi kwamba Yehova aokoe Yerusalemu kutoka mikononi mwangu?”’”+ 21  Lakini walikaa kimya, hawakumjibu neno lolote, kwa maana mfalme aliwaagiza hivi: “Msimjibu.”+ 22  Lakini Eliakimu mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba,* Shebna+ aliyekuwa mwandishi, na Yoa mwana wa Asafu aliyekuwa akifanya kazi ya kuweka kumbukumbu wakaja kwa Hezekia mavazi yao yakiwa yameraruliwa, wakamwambia maneno ya Rabshake.

Maelezo ya Chini

Au “msimamizi mkuu wa vinywaji vya mfalme.”
Au “jumba la mfalme.”
Au “Kisiria.”
Tnn., “Fanyeni baraka pamoja nami na mtoke nje na kuja kwangu.”
Au “jumba la mfalme.”