Kulingana na Luka 15:1-32

  • Mfano wa kondoo aliyepotea (1-7)

  • Mfano wa sarafu iliyopotea (8-10)

  • Mfano wa mwana mpotevu (11-32)

15  Basi wakusanya kodi wote na watenda dhambi walikuwa wakikusanyika karibu naye ili kumsikiliza.+  Mafarisayo na waandishi wakaendelea kunung’unika wakisema: “Mtu huyu huwakaribisha watenda dhambi na kula pamoja nao.”  Ndipo akawaambia mfano huu:  “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo 100, naye ampoteze mmoja, je, hatawaacha wale 99 nyikani aende kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate?+  Na baada ya kumpata, anambeba mabegani na kushangilia.  Na anapofika nyumbani anawaita rafiki zake na jirani zake, na kuwaambia, ‘Shangilieni pamoja nami, kwa kuwa nimempata kondoo wangu aliyekuwa amepotea.’+  Vivyo hivyo, ninawaambia kwamba kutakuwa na shangwe nyingi mbinguni kwa sababu ya mtenda dhambi mmoja anayetubu+ kuliko kwa waadilifu 99 ambao hawahitaji kutubu.  “Au mwanamke aliye na sarafu kumi za drakma* akipoteza drakma* moja, je, hatawasha taa, afagie nyumba yake na kuitafuta kwa makini mpaka aipate?  Na baada ya kuipata, anawaita rafiki zake* na jirani zake na kuwaambia, ‘Shangilieni pamoja nami, kwa kuwa nimeipata sarafu ya drakma* niliyokuwa nimepoteza.’ 10  Vivyo hivyo, ninawaambia kwamba malaika wa Mungu hushangilia mtenda dhambi mmoja anapotubu.”+ 11  Kisha akasema: “Mtu fulani alikuwa na wana wawili. 12  Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe sehemu ya urithi ambayo ni yangu.’ Basi akawagawia wanawe mali yake. 13  Baada ya siku chache, yule mwana mdogo akakusanya vitu vyake vyote akasafiri kwenda nchi ya mbali, akiwa huko akatumia vibaya mali yake kwa kuishi maisha ya anasa.* 14  Alipokuwa ametumia kila kitu, njaa kali sana ikatokea katika nchi hiyo yote, naye hakuwa na chochote. 15  Hata alienda kuajiriwa na raia mmoja wa nchi hiyo, ambaye alimpeleka kwenye mashamba yake akalishe nguruwe.+ 16  Naye alitamani kujishibisha kwa maganda ya karuba ambayo nguruwe walikuwa wakila, lakini hakuna mtu aliyempa chochote. 17  “Aliporudiwa na fahamu akasema, ‘Baba yangu ameajiri wafanyakazi wengi nao wana mkate kwa wingi, lakini mimi ninakufa njaa! 18  Nitafunga safari kwenda kwa baba yangu na kumwambia: “Baba, nimetenda dhambi dhidi ya mbingu na dhidi yako. 19  Sistahili tena kuitwa mwanao. Naomba niwe mmoja wa wafanyakazi wako.”’ 20  Basi akaondoka na kwenda kwa baba yake. Akiwa mbali, baba yake akamwona na kumsikitikia, akakimbia, akamkumbatia* na kumbusu kwa wororo. 21  Kisha yule mwana akamwambia, ‘Baba, nimetenda dhambi dhidi ya mbingu na dhidi yako.+ Sistahili tena kuitwa mwanao.’ 22  Lakini baba yake akawaambia watumwa, ‘Leteni upesi kanzu bora zaidi na kumvika, pia mvisheni pete mkononi na viatu miguuni. 23  Vilevile, leteni ndama aliyenoneshwa, mchinjeni, nasi tule na tusherehekee, 24  kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yuko hai;+ alikuwa amepotea naye amepatikana.’ Basi wakaanza kusherehekea. 25  “Sasa mwanawe mkubwa alikuwa shambani, alipokuwa akirudi na kukaribia nyumba, akasikia sauti ya muziki na dansi. 26  Basi akamwita mtumishi mmoja akamuuliza kilichokuwa kikiendelea. 27  Akamjibu, ‘Ndugu yako amerudi, kwa hiyo baba yako amechinja ndama aliyenoneshwa kwa sababu amerudi akiwa na afya njema.’* 28  Lakini akakasirika na kukataa kuingia ndani. Basi baba yake akatoka nje akaanza kumbembeleza. 29  Akamjibu baba yake, ‘Tazama! nimekutumikia kwa miaka mingi na sijawahi kuvunja amri yako hata mara moja, lakini hujawahi kunipa hata mara moja mwanambuzi ili nijifurahishe pamoja na rafiki zangu. 30  Lakini mara tu alipofika huyu mwanao aliyetumia vibaya* mali yako na makahaba, ulimchinjia ndama aliyenoneshwa.’ 31  Baba yake akamjibu, ‘Mwanangu, umekuwa pamoja nami sikuzote, na vitu vyangu vyote ni vyako. 32  Lakini ilibidi tusherehekee na kushangilia, kwa maana ndugu yako alikuwa amekufa lakini sasa yuko hai; alikuwa amepotea naye amepatikana.’”

Maelezo ya Chini

Au “wanawake ambao ni rafiki zake.”
Au “upotovu; bila kujali.”
Tnn., “akamwangukia shingoni.”
Au “amerudi salama.”
Tnn., “aliyekula; aliyeharibu.”