Matendo ya Mitume 21:1-40

  • Safarini kwenda Yerusalemu (1-14)

  • Kuwasili Yerusalemu (15-19)

  • Paulo afuata ushauri wa wazee (20-26)

  • Vurugu hekaluni; Paulo akamatwa (27-36)

  • Paulo aruhusiwa kuhutubia umati (37-40)

21  Tulipofaulu kuachana nao na kusafiri baharini, tulienda moja kwa moja mpaka Kosi, siku iliyofuata tukafika Rode, na kutoka huko tukaenda Patara.  Tulipopata meli iliyokuwa ikivuka kwenda Foinike, tukapanda na kuondoka.  Baada ya kufika mahali tulipoweza kuona kisiwa cha Kipro, tukakiacha upande wa kushoto tukasafiri mpaka Siria, tukafika Tiro ambako meli ilipaswa kushusha shehena.  Tukawatafuta wanafunzi na tulipowapata tukakaa huko siku saba. Lakini kupitia roho, wakamwambia Paulo tena na tena asikanyage Yerusalemu.+  Baada ya muda wetu huko kwisha, tukaondoka na kuanza safari, lakini wote kutia ndani wanawake na watoto, wakatusindikiza mpaka nje ya jiji. Tukapiga magoti ufuoni, tukasali,  kisha tukaagana. Tukapanda meli, nao wakarudi nyumbani kwao.  Ndipo tukakamilisha safari ya baharini kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu akina ndugu na kukaa nao siku moja.  Siku iliyofuata tukaondoka na kufika Kaisaria, tukaingia katika nyumba ya Filipo mweneza-injili, aliyekuwa mmoja wa wale wanaume saba,+ nasi tukakaa pamoja naye.  Mtu huyo alikuwa na binti wanne ambao hawakuwa wameolewa,* nao walitoa unabii.+ 10  Lakini baada ya kukaa huko kwa siku kadhaa, nabii aliyeitwa Agabo+ akashuka kutoka Yudea. 11  Akaja mahali tulipokuwa akachukua mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono na kusema: “Hivi ndivyo roho takatifu inavyosema, ‘Wayahudi kule Yerusalemu watamfunga+ hivi mwanamume ambaye mshipi huu ni wake, nao watamtia mikononi mwa watu wa mataifa.’”+ 12  Tuliposikia hayo, sisi na wale waliokuwa hapo tukaanza kumsihi Paulo asipande kwenda Yerusalemu. 13  Kisha Paulo akasema: “Kwa nini mnalia na kujaribu kunivunja moyo?* Muwe na hakika kwamba niko tayari si kufungwa tu bali pia kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.”+ 14  Tuliposhindwa kumshawishi, tukaacha kumkataza,* tukasema: “Mapenzi ya Yehova* na yatendeke.” 15  Sasa baada ya siku hizo tukajitayarisha kwa ajili ya safari kisha tukaanza kuelekea Yerusalemu. 16  Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakaenda pamoja nasi, wakatupeleka kwa Mnasoni wa Kipro, mwanafunzi wa zamani ambaye tulipaswa kuwa wageni nyumbani kwake. 17  Tulipofika Yerusalemu, akina ndugu wakatukaribisha kwa furaha. 18  Lakini siku iliyofuata Paulo akaingia pamoja nasi kwa Yakobo,+ na wazee wote walikuwapo. 19  Akawasalimu na kuanza kusimulia kirefu mambo ambayo Mungu alifanya miongoni mwa mataifa kupitia huduma yake. 20  Baada ya kusikia jambo hilo, wakaanza kumtukuza Mungu, lakini wakamwambia: “Ndugu, unaona jinsi ambavyo maelfu ya Wayahudi wamekuwa waamini, na wote wanafuata Sheria kwa bidii.+ 21  Lakini wamesikia uvumi kukuhusu kwamba umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wote kati ya mataifa kuiasi sheria ya Musa, ukiwaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zilizowekwa.+ 22  Sasa tufanye nini? Kwa kweli watasikia kwamba umefika. 23  Basi fanya jambo tunalokuambia: Tuna wanaume wanne waliojiwekea nadhiri. 24  Nenda pamoja na watu hawa ukajitakase kisherehe pamoja nao na kuwagharimia, ili wanyolewe vichwa vyao. Ndipo kila mtu atajua kwamba uvumi walioambiwa kukuhusu si wa kweli, bali unatembea kwa utaratibu, na pia unashika Sheria.+ 25  Kuhusu waamini kutoka kati ya mataifa, tumewatumia uamuzi wetu kwa maandishi kwamba wanapaswa kuepuka vitu vilivyotolewa dhabihu kwa sanamu+ na pia damu,+ na vitu vilivyonyongwa,*+ na uasherati.”*+ 26  Ndipo Paulo akaenda pamoja na wanaume hao siku iliyofuata, akajitakasa kisherehe pamoja nao,+ naye akaingia hekaluni ili kutoa taarifa kuhusu wakati ambapo siku za kujitakasa zingekwisha na toleo litolewe kwa ajili ya kila mmoja wao. 27  Sasa zile siku saba zilipokaribia kwisha, Wayahudi kutoka Asia walipomwona hekaluni, wakauchochea umati wote, nao wakamkamata, 28  wakisema kwa sauti kubwa: “Wanaume wa Israeli, tusaidieni! Huyu ndiye mwanamume anayewafundisha watu kila mahali dhidi ya watu wetu na Sheria yetu na mahali hapa. Isitoshe, hata aliwaingiza Wagiriki hekaluni naye amepatia unajisi mahali hapa patakatifu.”+ 29  Kwa maana mwanzoni walikuwa wamemwona Trofimo+ Mwefeso jijini akiwa pamoja naye, nao wakadhani Paulo alikuwa amemwingiza hekaluni. 30  Jiji lote likawa na machafuko, watu wakakimbia pamoja wakamkamata Paulo na kumkokota nje ya hekalu, na mara moja milango ikafungwa. 31  Walipokuwa wakijaribu kumuua, kamanda wa kikosi cha jeshi akapata habari kwamba Yerusalemu yote ilikuwa na vurugu; 32  mara moja akachukua wanajeshi na maofisa wa jeshi wakakimbia kwenda huko. Walipomwona kamanda wa jeshi na wanajeshi, wakaacha kumpiga Paulo. 33  Ndipo yule kamanda wa jeshi akakaribia akamweka chini ya ulinzi na kuamuru afungwe kwa minyororo miwili;+ kisha akauliza huyo ni nani na alikuwa amefanya nini. 34  Lakini baadhi ya watu katika umati wakaanza kusema jambo moja kwa sauti kubwa na wengine jambo tofauti. Basi aliposhindwa kujua jambo lolote la hakika kwa sababu ya fujo hizo, akaamuru aletwe kwenye makao ya wanajeshi. 35  Lakini alipofika kwenye ngazi, alilazimika kubebwa na wanajeshi kwa sababu umati ulitaka kumuumiza, 36  kwa maana umati wa watu uliendelea kuwafuata, ukisema kwa sauti kubwa: “Auawe!” 37  Alipokuwa karibu kuingizwa katika makao ya wanajeshi, Paulo akamuuliza yule kamanda wa jeshi: “Je, ninaruhusiwa kukuambia jambo fulani?” Naye akamuuliza: “Je, unajua kuzungumza Kigiriki? 38  Kwani wewe si yule Mmisri ambaye hivi majuzi alianzisha uchochezi na kuwaongoza wale wanaume 4,000 wenye visu hadi nyikani?” 39  Paulo akamjibu: “Mimi kwa kweli ni Myahudi,+ wa Tarso+ huko Kilikia, raia wa jiji maarufu. Basi nakuomba uniruhusu nizungumze na watu hawa.” 40  Baada ya kupewa ruhusa, Paulo, akiwa amesimama kwenye ngazi, akawapungia watu mkono. Waliponyamaza kabisa, akawahutubia kwa lugha ya Kiebrania,+ akisema:

Maelezo ya Chini

Tnn., “walikuwa mabikira.”
Au “kuudhoofisha moyo wangu.”
Tnn., “tukakaa kimya.”
Au “ vitu vilivyouawa bila kutolewa damu.”
Neno la Kigiriki porneiʹa. Angalia Kamusi.