Matendo ya Mitume 25:1-27

  • Kesi ya Paulo mbele ya Festo (1-12)

    • “Ninakata rufaa kwa Kaisari!” (11)

  • Festo ashauriana na Mfalme Agripa (13-22)

  • Paulo mbele ya Agripa (23-27)

25  Kwa hiyo, baada ya Festo+ kufika katika mkoa na kuchukua mamlaka, siku tatu baadaye alipanda kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria.  Nao wakuu wa makuhani na watu mashuhuri kati ya Wayahudi wakamweleza mashtaka dhidi ya Paulo.+ Basi wakaanza kumwomba Festo  awaonyeshe kibali* kwa kumwita Paulo aje Yerusalemu. Lakini walikuwa wanapanga kumvizia Paulo na kumuua barabarani.+  Hata hivyo, Festo akajibu kwamba Paulo alipaswa kuzuiliwa huko Kaisaria na kwamba baada ya muda mfupi yeye mwenyewe angerudi huko.  Akasema: “Basi wale walio na mamlaka kati yenu washuke pamoja nami na kumshtaki, ikiwa kwa kweli mtu huyu amefanya kosa lolote.”+  Kwa hiyo, baada ya kukaa kati yao siku zisizozidi nane au kumi, akashuka kwenda Kaisaria, na siku iliyofuata akaketi kwenye kiti cha hukumu na kuamuru Paulo aletwe.  Alipoingia, Wayahudi waliokuwa wameshuka kutoka Yerusalemu wakasimama kumzunguka, wakitoa mashtaka mengi mazito ambayo hawakuweza kuyathibitisha.+  Lakini Paulo akajitetea hivi: “Sijatenda dhambi yoyote dhidi ya Sheria ya Wayahudi wala dhidi ya hekalu wala dhidi ya Kaisari.”+  Festo akitamani kukubaliwa na Wayahudi,+ akamjibu Paulo: “Je, ungependa kupanda kwenda Yerusalemu ukahukumiwe huko mbele yangu kuhusu mambo haya?” 10  Lakini Paulo akasema: “Mimi nimesimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ambapo ninapaswa kuhukumiwa. Sijawakosea Wayahudi, nawe pia umegundua jambo hilo. 11  Ikiwa, kwa kweli mimi ni mkosaji na nimefanya jambo lolote linalostahili kifo,+ niko tayari kufa; lakini kama mashtaka ya watu hawa hayana msingi, hakuna mtu aliye na haki ya kunikabidhi kwao ili tu apate kibali chao. Ninakata rufaa kwa Kaisari!”+ 12  Ndipo Festo, baada ya kuzungumza na baraza la washauri, akajibu: “Umekata rufaa kwa Kaisari; nawe utaenda kwa Kaisari.” 13  Baada ya siku kadhaa, Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria kwa ajili ya ziara ya kumsalimia Festo. 14  Kwa kuwa wangekaa huko siku kadhaa, Festo akawasilisha kesi ya Paulo mbele ya mfalme, akisema: “Kuna mwanamume ambaye Feliksi alimwacha akiwa mfungwa, 15  nami nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi walileta habari kumhusu,+ wakiomba ahukumiwe hatia. 16  Lakini nikawajibu kwamba si utaratibu wa Kiroma kumkabidhi mtu yeyote ili tu kupata kibali kabla ya mshtakiwa kukutana uso kwa uso na wale waliomshtaki na kupata nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka.+ 17  Basi walipofika hapa, sikukawia, bali kesho yake niliketi kwenye kiti cha hukumu na kuamuru mwanamume huyo aletwe. 18  Wale waliomshtaki waliposimama, hawakumshtaki kwa mambo maovu niliyotazamia.+ 19  Ila tu walikuwa wakibishana naye kuhusu ibada yao ya mungu*+ na kuhusu mtu fulani anayeitwa Yesu ambaye alikufa, lakini ambaye Paulo alikuwa akisisitiza kwamba yuko hai.+ 20  Sikujua jinsi ya kutatua mabishano haya, basi nikamuuliza kama angependa kwenda Yerusalemu ili akahukumiwe huko kuhusu mambo haya.+ 21  Lakini Paulo alipokata rufaa ili abaki kizuizini akisubiri uamuzi wa Augusto Mkuu,*+ nikaamuru azuiliwe mpaka nitakapomtuma kwa Kaisari.” 22  Ndipo Agripa akamwambia Festo: “Mimi mwenyewe ningependa kumsikia mtu huyo.”+ Akasema: “Kesho utamsikia.” 23  Basi kesho yake, Agripa na Bernike wakaja kwa fahari nyingi na kuingia katika ukumbi wa baraza pamoja na viongozi wa jeshi na vilevile wanaume mashuhuri wa jiji; naye Festo alipotoa amri, Paulo akaletwa. 24  Festo akasema: “Mfalme Agripa na nyote mlio hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu ambaye Wayahudi wote wameniomba huko Yerusalemu na huku pia, wakipaza sauti kwamba hapaswi kuendelea kuishi.+ 25  Lakini nikaona kwamba hakuwa amefanya jambo lolote linalostahili kifo.+ Basi mtu huyu alipokata rufaa kwa Augusto Mkuu, niliamua kumpeleka. 26  Lakini sina jambo hususa la kumwandikia Bwana wangu kumhusu. Basi nimemleta mbele yenu nyote, na hasa mbele yako wewe, Mfalme Agripa, ili baada ya kumchunguza kihukumu, nipate jambo la kuandika. 27  Kwa maana ninaona haifai kumpeleka mfungwa bila kuonyesha mashtaka yanayomkabili.”

Maelezo ya Chini

Tnn., “kibali dhidi yake.”
Au “dini yao.”
Jina la cheo la maliki Mroma.