Matendo ya Mitume 27:1-44

  • Paulo asafiri baharini kwenda Roma (1-12)

  • Meli yapigwa na dhoruba (13-38)

  • Wavunjikiwa na meli (39-44)

27  Basi kwa kuwa iliamuliwa tusafiri baharini kwenda Italia,+ wakamkabidhi Paulo na wafungwa wengine kwa ofisa wa jeshi anayeitwa Yulio, wa kikosi cha Augusto.  Tukapanda meli kutoka Adramitiamu iliyokuwa karibu kusafiri kwenda kwenye bandari zilizo kando ya pwani ya mkoa wa Asia, tukaanza safari; naye Aristarko+ Mmakedonia wa Thesalonike, alikuwa pamoja nasi.  Siku iliyofuata tukafika Sidoni, na Yulio akamtendea Paulo kwa fadhili* na kumruhusu aende kwa rafiki zake akatunzwe nao.  Tulipotoka huko, tukasafiri karibu na Kipro ili kujikinga na pepo zilizokuwa zikivuma kinyume nasi.  Kisha tukapita kwenye bahari kuu kandokando ya Kilikia na Pamfilia na kutia nanga kwenye bandari ya Mira huko Likia.  Huko ofisa wa jeshi akapata meli kutoka Aleksandria iliyokuwa ikielekea Italia, naye akatuagiza tupande meli hiyo.  Kisha baada ya kusafiri polepole kwa siku kadhaa, tukafika kwa shida huko Kinido. Kwa sababu upepo ulituzuia kusonga mbele, tukasafiri chini ya Krete karibu na Salmone.  Tukasafiri kwa shida kandokando ya pwani, tukafika mahali panapoitwa Bandari Nzuri, karibu na jiji la Lasea.  Muda mrefu ulikuwa umepita na kufikia sasa ilikuwa hatari kusafiri baharini, kwa sababu hata kipindi cha kufunga kwa Siku ya Kufunika Dhambi+ tayari kilikuwa kimepita, basi Paulo akatoa pendekezo, 10  akawaambia: “Ninaona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara kubwa si kwa shehena na meli tu bali pia kwa uhai wetu.”* 11  Hata hivyo, ofisa wa jeshi akamsikiliza nahodha na mwenye meli badala ya kusikiliza alichokuwa akisema Paulo. 12  Kwa kuwa bandari hiyo haikufaa wakati wa majira ya baridi kali, wengi wakapendekeza kuendelea na safari, ili kuona kama wangefaulu kukaa wakati wa majira ya baridi kali huko Feniki, ambayo ni bandari ya Krete inayofunguka kuelekea kaskazini mashariki na kuelekea kusini mashariki. 13  Upepo wa kusini ulipovuma kwa utulivu, walifikiri kwamba wametimiza kusudi lao, wakang’oa nanga na kuanza kusafiri kandokando ya Krete karibu na ufuo. 14  Hata hivyo, baada ya muda mfupi, upepo mkali unaoitwa Euroakilo* ukavuma kwa kasi juu yake. 15  Kwa kuwa meli ilipigwa na upepo wenye nguvu na ikashindwa kuukabili, tukaiachilia nao upepo ukatusukuma. 16  Kisha tukapita chini ya kisiwa kidogo kinachoitwa Kauda, na bado ilikuwa vigumu kuiokoa mashua ndogo* iliyokuwa kwenye tezi ya meli. 17  Lakini baada ya kuiingiza ndani, wakaifunga ile mashua kwenye meli, na kwa kuwa waliogopa kukwama kwenye mchanga wa Sirti,* wakashusha vifaa vya kuendeshea na hivyo wakasukumwa na upepo. 18  Kwa sababu tulikuwa tukirushwarushwa kwa nguvu na dhoruba, siku iliyofuata wakaanza kupunguza uzito wa meli. 19  Siku ya tatu, wakatupa ayari za meli hiyo kwa mikono yao wenyewe. 20  Tulipokosa kuona jua wala nyota kwa siku nyingi na kupigwa na dhoruba kali,* mwishowe tulianza kupoteza tumaini la kuokoka. 21  Baada ya watu kukaa kwa muda mrefu bila kula, Paulo alisimama katikati yao na kusema: “Ikiwa mngefuata ushauri wangu hamngesafiri baharini kutoka Krete na hivyo hamngepatwa na madhara na hasara hii.+ 22  Hata hivyo, sasa ninawahimiza mjipe moyo, kwa maana hakuna hata mmoja wenu atakayepotea,* meli tu ndiyo itakayopotea. 23  Usiku huu malaika+ wa Mungu ambaye mimi ni mali yake na ambaye ninamtolea utumishi mtakatifu, alisimama kando yangu 24  akasema: ‘Usiogope, Paulo. Utasimama mbele ya Kaisari,+ na tazama! Mungu amekupa wale wote wanaosafiri pamoja nawe.’ 25  Basi jipeni moyo, kwa maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa kama nilivyoambiwa. 26  Hata hivyo, ni lazima tutupwe kwenye ufuo wa kisiwa fulani.”+ 27  Sasa usiku wa 14 ulipofika nasi tukawa tukirushwa huku na huku katika Bahari ya Adria, katikati ya usiku mabaharia walianza kuhisi kwamba walikuwa wakikaribia nchi kavu. 28  Wakapima kina kwa bildi na kupata pima 20,* basi wakasonga mbele kidogo wakapima tena na kupata pima 15.* 29  Wakiogopa kwamba tungekwama kwenye miamba, wakashusha nanga nne kutoka kwenye tezi na kuanza kutamani kupambazuke. 30  Lakini mabaharia walipojaribu kutoroka kutoka kwenye meli na kushusha mashua ndogo ndani ya bahari wakisingizia kwamba walikusudia kuzishusha nanga kutoka kwenye omo, 31  Paulo akamwambia ofisa wa jeshi na wanajeshi: “Watu hawa wasipobaki katika meli, ninyi hamwezi kuokoka.”+ 32  Ndipo wanajeshi wakakata kamba za ile mashua ndogo na kuiacha ianguke. 33  Sasa kulipokaribia kupambazuka, Paulo akawahimiza wote wale chakula, akisema: “Kwa siku 14 mmekuwa mkisubiri kwa wasiwasi, bila kula chochote. 34  Basi ninawatia moyo mle chakula; kwa ajili ya usalama wenu, kwa maana hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyenu utakaopotea.” 35  Baada ya kusema hivyo, akachukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega, na kuanza kula. 36  Kwa hiyo wote wakajipa moyo, nao pia wakaanza kula. 37  Kwa ujumla, sote tulikuwa watu* 276 katika meli. 38  Walipokula chakula wakashiba, wakapunguza uzito wa meli kwa kutupa ngano baharini.+ 39  Kulipopambazuka, hawakuitambua nchi hiyo,+ lakini waliona ghuba yenye ufuo, nao waliazimia kuipeleka meli ufuoni kama wangeweza. 40  Basi wakazikata nanga na kuziacha zianguke baharini, wakati huohuo wakifungua kamba za makasia ya usukani; na baada ya kutweka tanga la mbele kwenye upepo, wakaelekea ufuoni. 41  Wakagonga rundo kubwa la mchanga lililorundikwa na bahari pande zote, wakaendesha meli juu ya mchanga nayo omo ikakwama na kukaa bila kutikisika, lakini mawimbi yakaanza kuvunja tezi vipandevipande kwa nguvu.+ 42  Ndipo wanajeshi wakaamua kuwaua wafungwa ili yeyote asiogelee na kutoroka. 43  Lakini ofisa wa jeshi alikuwa ameazimia kumfikisha Paulo salama naye akawazuia ili wasitekeleze mpango wao. Akawaamuru wale ambao wangeweza kuogelea wajitupe baharini na watangulie kuogelea mpaka nchi kavu, 44  na wale wengine wangefuata, wengine wakiwa juu ya mbao na wengine juu ya vipande vya meli. Basi wote wakafika salama kwenye nchi kavu.+

Maelezo ya Chini

Au “fadhili za kibinadamu.”
Au “nafsi zetu.”
Yaani, upepo wa kaskazini mashariki.
Mashua ndogo inayotumiwa kuokoa uhai.
Angalia Kamusi.
Tnn., “isiyo ndogo.”
Au “nafsi itakayopotea.”
Karibu mita 36 (futi 120). Angalia Nyongeza B14.
Karibu mita 27 (futi 90). Angalia Nyongeza B14.
Au “nafsi.”