Mwanzo 34:1-31

  • Dina abakwa (1-12)

  • Wana wa Yakobo watenda kwa udanganyifu (13-31)

34  Sasa Dina, binti ya Yakobo na Lea,+ alizoea kwenda kuwatembelea* mabinti wengine nchini.+  Shekemu mwana wa Hamori Mhivi,+ mkuu wa nchi, alipomwona, alimchukua na kumbaka.  Shekemu akavutiwa sana na Dina binti ya Yakobo, akampenda msichana huyo na kuanza kumtongoza.*  Hatimaye Shekemu akamwambia Hamori+ baba yake: “Nichukulie msichana huyu awe mke wangu.”  Yakobo aliposikia kwamba Shekemu alikuwa amembaka Dina binti yake, wanawe walikuwa na mifugo yake malishoni. Basi Yakobo akakaa kimya mpaka waliporudi.  Baadaye Hamori, baba ya Shekemu, akaja kuzungumza na Yakobo.  Lakini wana wa Yakobo wakasikia habari hizo, wakarudi haraka kutoka malishoni. Waliumia moyoni na kukasirika sana kwa sababu Shekemu alikuwa amemfedhehesha Israeli kwa kumbaka binti ya Yakobo,+ jambo ambalo halipaswi kufanywa.+  Hamori akazungumza nao, akisema: “Mwanangu Shekemu anamtamani sana* binti yenu. Tafadhali mpeni binti yenu awe mke wake,  na mfanye mapatano ya ndoa* pamoja nasi. Tupatieni mabinti wenu, nanyi mchukue mabinti wetu.+ 10  Mnaweza kuishi nasi na kukaa mahali popote nchini. Kaeni humu na kufanya biashara na kutulia nchini.” 11  Kisha Shekemu akamwambia baba ya Dina na ndugu zake: “Naomba nipate kibali machoni penu, nami nitawapa chochote mtakachoniomba. 12  Mnaweza kudai nitoe kiasi kikubwa sana cha mahari na zawadi.+ Niko tayari kuwapa chochote mtakachoniambia. Nipeni tu msichana huyu awe mke wangu.” 13  Wana wa Yakobo wakamjibu kwa hila Shekemu na Hamori baba yake, kwa sababu Shekemu alikuwa amembaka dada yao Dina. 14  Wakawaambia: “Hatuwezi kamwe kufanya jambo kama hilo, kukubali dada yetu aolewe na mwanamume ambaye hajatahiriwa,*+ kufanya hivyo ni fedheha kwetu. 15  Tunaweza kukubali tu kwa sharti hili: watahirini wanaume wenu wote, muwe kama sisi.+ 16  Ndipo tutakapowapa mabinti wetu na kuwachukua mabinti wenu, nasi tutaishi nanyi na kuwa familia moja. 17  Lakini msipotusikiliza na kutahiriwa, basi tutamchukua binti yetu na kwenda zetu.” 18  Maneno yao yakamfurahisha Hamori+ na Shekemu mwanawe.+ 19  Kijana huyo hakukawia kutimiza ombi lao,+ kwa sababu alimpenda binti ya Yakobo, naye Shekemu aliheshimiwa kuliko watu wote wa nyumba ya baba yake. 20  Kwa hiyo Hamori na Shekemu mwanawe wakaenda kwenye lango la jiji, wakazungumza na wanaume wa jiji lao+ wakisema: 21  “Wanaume hawa wangependa tuishi nao kwa amani. Waruhusuni wakae nchini na kufanya biashara humu, kwa maana nchi yetu ni kubwa vya kutosha. Tunaweza kuwaoa mabinti wao, nasi tunaweza kuwapa mabinti wetu.+ 22  Lakini watakubali tu kuishi nasi ili tuwe familia moja kwa sharti hili moja: kwamba kila mwanamume miongoni mwetu atahiriwe kama tu wanavyotahiriwa.+ 23  Tukifanya hivyo, je, mali zao, utajiri wao, na mifugo yao yote haitakuwa yetu? Basi acheni tutimize sharti lao ili waishi nasi.” 24  Wote waliokuwa wakitoka nje kupitia lango la jiji lake wakamsikiliza Hamori na Shekemu mwanawe, na wanaume wote wakatahiriwa, wote waliokuwa wakitoka nje kupitia lango la jiji. 25  Hata hivyo, siku ya tatu, walipokuwa bado wana maumivu, wana wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, ndugu za Dina,+ wakachukua kila mmoja wao upanga wake, wakaenda ghafla katika jiji hilo na kumuua kila mwanamume.+ 26  Wakamuua Hamori na Shekemu mwanawe kwa upanga, kisha wakamchukua Dina kutoka katika nyumba ya Shekemu na kuondoka. 27  Wana wengine wa Yakobo walipofika waliona maiti za wanaume waliouawa, wakalipora jiji hilo kwa sababu dada yao alibakwa.+ 28  Wakachukua kondoo wao, mbuzi wao, ng’ombe wao, punda wao, na kitu chochote kilichokuwa jijini na shambani. 29  Walichukua pia mali zao zote, wakawachukua mateka wake zao na watoto wao wote, na kupora vitu vyote vilivyokuwa katika nyumba zao. 30  Basi Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi:+ “Mmeniletea taabu kubwa* kwa kunifanya niwe uvundo kwa wakaaji wa nchi hii, Wakanaani na Waperizi. Nina watu wachache, nao kwa hakika wataungana na kunishambulia, nao wataniangamiza, mimi na nyumba yangu.” 31  Lakini wakamwambia: “Je, kuna yeyote anayepaswa kumtendea dada yetu kama kahaba?”

Maelezo ya Chini

Au “kuwaona.”
Tnn., “kuzungumza na moyo wa msichana huyo.”
Au “nafsi ya mwanangu Shekemu imeshikamana na.”
Au “na muoane nasi.”
Tnn., “aliye na govi.”
Au “Mmenifanya nitengwe.”