Mwanzo 37:1-36

  • Ndoto za Yosefu (1-11)

  • Yosefu na ndugu zake wenye wivu (12-24)

  • Yosefu auzwa utumwani (25-36)

37  Yakobo akaendelea kuishi katika nchi ya Kanaani, alikoishi baba yake akiwa mgeni.+  Hii ndiyo historia ya Yakobo. Kijana Yosefu+ alipokuwa na umri wa miaka 17, alikuwa akichunga kondoo+ pamoja na wana wa Bilha+ na wana wa Zilpa,+ wake za baba yake. Naye Yosefu akamletea baba yake habari mbaya kuwahusu.  Sasa Israeli alimpenda sana Yosefu kuliko wanawe wengine+ kwa sababu alimzaa uzeeni, naye alikuwa amemshonea joho la pekee.*  Ndugu zake walipoona kwamba baba yao alimpenda sana kuliko yeyote miongoni mwao, wakaanza kumchukia, na hawakuzungumza naye kwa amani.  Baadaye Yosefu aliota ndoto na kuwasimulia ndugu zake,+ nao wakapata sababu zaidi ya kumchukia.  Aliwaambia hivi: “Tafadhali sikilizeni ndoto hii niliyoota.  Tulikuwa tukifunga matita ya masuke katikati ya shamba kisha tita langu likainuka na kusimama wima, nayo matita yenu yakalizunguka tita langu na kuliinamia.”+  Ndugu zake wakamuuliza: “Je, kweli utajiweka kuwa mfalme wetu na kututawala?”+ Basi wakapata sababu nyingine ya kumchukia, kwa sababu ya ndoto zake na mambo aliyosema.  Baada ya hayo akaota tena ndoto nyingine, naye akawasimulia ndugu zake ndoto hiyo: “Nimeota ndoto nyingine. Wakati huu jua na mwezi na nyota 11 zilikuwa zikiniinamia.”+ 10  Kisha akamsimulia baba yake na ndugu zake ndoto hiyo, baba yake akamkemea na kumuuliza: “Ndoto hiyo yako inamaanisha nini? Je, kweli mimi na pia mama yako na ndugu zako tutakuja na kukuinamia mpaka ardhini?” 11  Basi ndugu zake wakazidi kumwonea wivu,+ lakini baba yake akayaweka akilini maneno yake. 12  Sasa ndugu zake wakaenda kulisha kondoo wa baba yao karibu na Shekemu.+ 13  Baadaye Israeli akamwambia Yosefu: “Ndugu zako wanachunga kondoo karibu na Shekemu, sivyo? Njoo nikutume kwao.” Yosefu akamwambia: “Niko tayari!” 14  Yakobo akamwambia: “Tafadhali, nenda uone kama ndugu zako wako salama. Angalia hali ya kondoo, uniletee habari.” Basi akamtuma kutoka katika bonde la* Hebroni,+ naye akashika njia kuelekea Shekemu. 15  Baadaye mtu fulani akamkuta akitangatanga mbugani. Mtu huyo akamuuliza: “Unatafuta nini?” 16  Akamjibu: “Ninawatafuta ndugu zangu. Tafadhali niambie, wanachunga kondoo wapi?” 17  Mtu huyo akamwambia: “Wameondoka hapa, niliwasikia wakisema, ‘Twendeni Dothani.’” Kwa hiyo Yosefu akawafuata ndugu zake na kuwakuta Dothani. 18  Sasa wakamwona akiwa mbali, na kabla hajafika karibu, wakaanza kupanga njama ya kumuua. 19  Wakaambiana: “Tazama! Ndiye yule mwota-ndoto anakuja.+ 20  Haya basi, njooni tumuue na kumtupa ndani ya shimo moja la maji, halafu tutasema kwamba aliliwa na mnyama mkali sana wa mwituni. Tuone itakuwaje kwa ndoto zake.” 21  Rubeni+ aliposikia maneno hayo, alijaribu kumwokoa ili wasimuue. Akasema: “Tusimuue.”+ 22  Kisha akawaambia: “Msimwage damu.+ Mtupeni ndani ya shimo hili la maji lililo nyikani, lakini msimdhuru.”*+ Rubeni alikusudia kumwokoa kutoka mikononi mwao ili amrudishe kwa baba yake. 23  Mara tu Yosefu alipowafikia ndugu zake, wakamvua joho lake la pekee,+ 24  kisha wakamchukua na kumtupa ndani ya shimo la maji. Wakati huo shimo hilo lilikuwa tupu; halikuwa na maji. 25  Kisha wakaketi chini ili wale chakula. Walipoinua macho yao, waliona msafara wa Waishmaeli+ ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamebeba gundi ya labdanamu, zeri, na magome yenye utomvu,+ nao walikuwa wakiteremka kwenda Misri. 26  Ndipo Yuda akawaambia ndugu zake: “Tutapata faida gani tukimuua ndugu yetu na kufunika damu yake?+ 27  Haya basi, acheni tumuuze+ kwa Waishmaeli, mkono wetu usimguse. Kwa kweli, yeye ni ndugu yetu na nyama yetu.” Kwa hiyo wakamsikiliza ndugu yao. 28  Basi wafanyabiashara hao Wamidiani+ walipokuwa wakipita, ndugu zake walimtoa shimoni na kumuuza kwa hao Waishmaeli kwa vipande 20 vya fedha.+ Watu hao wakampeleka Yosefu Misri. 29  Baadaye Rubeni aliporudi kwenye lile shimo la maji na kuona kwamba Yosefu hayumo shimoni, akayararua mavazi yake. 30  Aliporudi kwa ndugu zake, alisema kwa mshangao: “Mtoto amepotea! Sasa mimi—nitafanya nini?” 31  Basi wakalichukua joho la Yosefu, wakamchinja mbuzi dume na kulichovya joho hilo katika damu ya mbuzi huyo. 32  Kisha wakamtumia baba yao joho hilo na kumwambia: “Hiki ndicho tulichopata. Tafadhali chunguza uone ikiwa joho hili ni la mwanao au la.”+ 33  Basi akalichunguza na kusema kwa mshtuko: “Ni joho la mwanangu! Inaonekana ameliwa na mnyama mkali wa mwituni! Kwa hakika Yosefu ameraruliwa vipandevipande!” 34  Ndipo Yakobo akayararua mavazi yake na kuvaa nguo za magunia kiunoni na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi. 35  Na wanawe wote na mabinti zake wote wakajaribu sana kumfariji, lakini alikataa kabisa kufarijiwa, akisema: “Nitashuka Kaburini*+ nikimwombolezea mwanangu!” Na baba yake akaendelea kumlilia. 36  Basi Wamidiani wakamuuza Yosefu Misri kwa Potifa, ofisa wa makao ya Farao+ aliyekuwa pia mkuu wa walinzi.+

Maelezo ya Chini

Au “nguo ndefu maridadi.”
Au “nchi tambarare ya chini ya.”
Au “msimguse.”
Au “Sheoli.” Angalia Kamusi.