Mwanzo 4:1-26

  • Kaini na Abeli (1-16)

  • Wazao wa Kaini (17-24)

  • Sethi na Enoshi mwanawe (25, 26)

4  Basi Adamu akafanya ngono na Hawa mke wake, na Hawa akapata mimba.+ Akamzaa Kaini+ na kusema: “Nimezaa mtoto wa kiume kwa msaada wa Yehova.”  Baadaye akamzaa Abeli,+ ndugu ya Kaini. Abeli akawa mchungaji, lakini Kaini akawa mkulima.  Baada ya muda, Kaini alileta baadhi ya mazao ya shambani ili ayatoe kuwa dhabihu kwa Yehova.  Lakini Abeli alileta baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo+ yake, pamoja na mafuta yao. Yehova alipendezwa na Abeli na dhabihu+ yake,  lakini hakupendezwa hata kidogo na Kaini na dhabihu yake. Basi Kaini akawaka hasira kali na kusononeka.*  Basi Yehova akamuuliza Kaini: “Kwa nini umekasirika sana na kusononeka?  Ukitenda mema, je, hutapata kibali tena?* Lakini usipotenda mema, dhambi inakunyemelea mlangoni, nayo inatamani sana kukutawala; lakini je, utaishinda?”  Baada ya hayo Kaini akamwambia Abeli ndugu yake: “Twende zetu shambani.” Basi walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua.+  Baadaye, Yehova akamuuliza Kaini: “Yuko wapi Abeli ndugu yako?” naye akajibu: “Sijui. Kwani mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” 10  Basi Mungu akasema: “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia kwa sauti kutoka ardhini.+ 11  Na sasa umelaaniwa kwa kufukuzwa kutoka katika ardhi ambayo imefungua kinywa chake ili kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako.+ 12  Utakapolima ardhi, haitakurudishia mazao yake.* Utakuwa mtu anayetangatanga na mkimbizi duniani.” 13  Kisha Kaini akamwambia Yehova: “Adhabu ya kosa langu ni kubwa mno kwangu kustahimili. 14  Leo unanifukuza kutoka katika nchi hii,* nami nitafichwa kutoka mbele za uso wako; nitakuwa mtu anayetangatanga na mkimbizi duniani, na yeyote atakayenipata kwa hakika ataniua.” 15  Kwa hiyo Yehova akamwambia: “Kwa sababu hiyo, yeyote atakayemuua Kaini atalipizwa kisasi mara saba.” Basi Yehova akaweka alama kwa ajili ya Kaini ili yeyote atakayempata asimuue. 16  Kisha Kaini akaenda zake kutoka mbele za Yehova, akaanza kuishi katika nchi ya Uhamisho,* upande wa mashariki wa Edeni.+ 17  Baadaye Kaini akafanya ngono na mke wake,+ naye akapata mimba na kumzaa Enoko. Kisha akajenga jiji na kuliita jiji hilo Enoko, jina la mwanawe. 18  Baadaye Enoko akamzaa Iradi. Na Iradi akamzaa Mehuyaeli, na Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, na Methushaeli akamzaa Lameki. 19  Lameki akaoa wake wawili. Mke wa kwanza aliitwa Ada, na wa pili aliitwa Zila. 20  Ada akamzaa Yabali. Ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa wale wanaokaa katika mahema na wenye mifugo. 21  Ndugu yake aliitwa Yubali. Ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa wale wote wanaopiga kinubi na zumari.* 22  Pia Zila alimzaa Tubal-kaini, aliyekuwa akitengeneza vifaa vya kila aina vya shaba na chuma. Na dada ya Tubal-kaini aliitwa Naama. 23  Kisha Lameki akatunga maneno haya kwa ajili ya wake zake, Ada na Zila: “Sikieni sauti yangu, enyi wake za Lameki;Sikilizeni maneno yangu: Nimemuua mwanamume kwa sababu ya kunijeruhi,Naam, mwanamume kijana kwa sababu ya kunipiga. 24  Ikiwa Kaini atalipizwa kisasi mara 7,+Basi Lameki ni mara 77.” 25  Adamu akafanya ngono tena na mke wake, naye akazaa mwana. Akampa jina Sethi,*+ kwa sababu kama mama yake alivyosema, “Mungu amenichagulia mzao mwingine* atakayechukua mahali pa Abeli, kwa sababu Kaini alimuua.”+ 26  Pia Sethi akazaa mwana na kumpa jina Enoshi.+ Wakati huo watu walianza kuliitia jina la Yehova.

Maelezo ya Chini

Tnn., “na uso wake ukakunjamana.”
Au “hutakwezwa?”
Tnn., “nguvu zake.”
Tnn., “kutoka kwenye uso wa ardhi.”
Au “nchi ya Nodi.”
Au “filimbi.”
Maana yake “Aliyechaguliwa; Aliyesimamishwa.”
Tnn., “mbegu nyingine.”