Mwanzo 41:1-57

  • Yosefu aeleza maana ya ndoto za Farao (1-36)

  • Yosefu akwezwa na Farao (37-46a)

  • Yosefu awekwa kuwa msimamizi wa chakula (46b-57)

41  Mwishoni mwa miaka miwili kamili, Farao aliota ndoto;+ katika ndoto hiyo alikuwa amesimama kando ya Mto Nile.  Na tazama! ng’ombe saba wazuri, walionona, walikuwa wakipanda kutoka mtoni, nao walikuwa wakila nyasi za Mto Nile.+  Baada yao, ng’ombe wengine saba wenye sura mbaya na waliokonda walipanda kutoka katika Mto Nile, wakasimama karibu na wale ng’ombe wanono kwenye ukingo wa Mto Nile.  Kisha wale ng’ombe wenye sura mbaya, waliokonda, wakaanza kuwala wale ng’ombe saba wazuri, walionona. Ndipo Farao akaamka.  Kisha akarudi kulala, akaota ndoto ya pili. Kulikuwa na masuke saba ya nafaka yakitokea katika bua moja, yalikuwa yamejaa nafaka nayo yalikuwa mazuri sana.+  Na baada ya hayo, masuke mengine saba ya nafaka yakakua, yalikuwa membamba na yalikuwa yamechomwa na upepo wa mashariki.  Kisha masuke hayo membamba ya nafaka yakaanza kuyameza yale masuke saba ya nafaka yaliyojaa nafaka na ambayo yalikuwa mazuri sana. Ndipo Farao akaamka na kugundua kwamba ilikuwa ndoto.  Lakini asubuhi, roho yake ikafadhaika. Basi akaagiza makuhani wote wachawi wa Misri na watu wake wote wenye hekima waitwe. Farao akawasimulia ndoto zake, lakini hakuna yeyote aliyeweza kumwambia Farao maana yake.*  Ndipo msimamizi mkuu wa vinywaji akamwambia Farao: “Ninaungama dhambi zangu leo. 10  Ee Farao, ulitukasirikia sisi watumishi wako. Kwa hiyo ukanifunga gerezani katika nyumba ya mkuu wa walinzi, mimi na mwokaji mkuu.+ 11  Kisha kila mmoja wetu akaota ndoto usiku uleule. Yeye na mimi, kila mmoja wetu aliota ndoto, na kila ndoto ilikuwa na maana yake.+ 12  Humo gerezani tulikuwa pamoja na kijana Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa walinzi.+ Tulipomsimulia ndoto zetu,+ alitueleza maana ya kila ndoto. 13  Mambo yote yalitimia kama alivyotuambia.* Nilirudishwa katika cheo changu, lakini yule mwingine alitundikwa mtini.”+ 14  Kwa hiyo Farao akaagiza Yosefu aletwe,+ basi wakamleta haraka kutoka gerezani.*+ Akajinyoa na kubadili nguo zake na kuingia mbele ya Farao. 15  Kisha Farao akamwambia Yosefu: “Niliota ndoto, lakini hakuna yeyote anayeweza kunieleza maana yake. Sasa nimesikia habari zako kwamba ukisimuliwa ndoto unaweza kueleza maana yake.”+ 16  Ndipo Yosefu akamjibu Farao: “Sistahili kusifiwa! Mungu ndiye atakayesema kuhusu hali yako, Ee Farao.”+ 17  Farao akamwambia Yosefu: “Katika ndoto yangu, nilikuwa nimesimama kwenye ukingo wa Mto Nile. 18  Na tazama! ng’ombe saba wazuri, walionona, walikuwa wakipanda kutoka katika Mto Nile, wakaanza kula nyasi za Mto Nile.+ 19  Baada yao, ng’ombe wengine saba dhaifu, wenye sura mbaya sana, na waliokonda walipanda kutoka katika Mto Nile. Sijawahi kamwe kuona ng’ombe wenye sura mbaya hivyo katika nchi yote ya Misri. 20  Na ng’ombe hao waliokonda, wenye sura mbaya, wakaanza kuwala wale ng’ombe saba wa kwanza walionona. 21  Lakini baada ya kuwala, hakuna yeyote angejua kwamba wamewala ng’ombe hao, kwa kuwa sura yao ilikuwa mbaya kama mwanzoni. Ndipo nikaamka. 22  “Kisha nikaona katika ndoto yangu masuke saba ya nafaka yakitokea katika bua moja, yalikuwa yamejaa nafaka nayo yalikuwa mazuri sana.+ 23  Halafu yakafuatwa na masuke mengine saba ya nafaka yaliyonyauka, membamba, na yaliyochomwa na upepo wa mashariki. 24  Kisha yale masuke membamba ya nafaka yakaanza kuyameza yale masuke saba mazuri sana ya nafaka. Basi nikawasimulia makuhani wachawi ndoto hiyo,+ lakini hakuna yeyote aliyeweza kunieleza maana yake.”+ 25  Ndipo Yosefu akamwambia Farao: “Ndoto zako ni ndoto moja, ndoto ileile. Mungu wa kweli amekuambia mambo atakayofanya.+ 26  Wale ng’ombe saba wazuri ni miaka saba. Na yale masuke saba mazuri ya nafaka ni miaka saba pia. Ndoto zako ni ndoto moja, ndoto ileile. 27  Wale ng’ombe saba waliokonda na wenye sura mbaya ambao walipanda baada ya wale wanono, ni miaka saba, na yale masuke saba ya nafaka yaliyo matupu, yaliyochomwa na upepo wa mashariki, yanamaanisha miaka saba ya njaa kali. 28  Hivi ndivyo nilivyokuambia, Ee Farao: Mungu wa kweli amekuonyesha mambo atakayofanya. 29  “Kutakuwa na miaka saba ya chakula kingi sana katika nchi yote ya Misri. 30  Lakini baada ya miaka hiyo, hakika kutakuwa na miaka saba ya njaa kali, nanyi hakika mtasahau chakula kingi sana kilichokuwa katika nchi ya Misri, na njaa hiyo kali itaiharibu nchi.+ 31  Nanyi hamtakumbuka chakula kingi sana kilichokuwa nchini kwa sababu ya njaa kali itakayofuata, kwa maana itakuwa kali sana. 32  Ee Farao, ulionyeshwa ndoto hiyo mara mbili kwa sababu Mungu wa kweli amekusudia kabisa jambo hilo, na Mungu wa kweli atalitimiza hivi karibuni. 33  “Sasa basi, Ee Farao, mtafute mwanamume mwenye busara na hekima umweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri. 34  Ee Farao, chukua hatua, waweke wasimamizi nchini, nawe utakusanya sehemu ya tano ya mazao yote nchini Misri katika miaka saba ya chakula kingi.+ 35  Nao wakusanye chakula chote katika miaka hiyo mizuri inayokuja, nao waweke nafaka katika maghala chini ya mamlaka yako Farao, na chakula hicho kihifadhiwe na kutunzwa katika majiji.+ 36  Chakula hicho kitaliwa nchini katika ile miaka saba ya njaa kali itakayoikumba nchi ya Misri, ili nchi isiangamie kwa sababu ya njaa hiyo kali.”+ 37  Pendekezo hilo lilimfurahisha Farao na watumishi wake wote. 38  Kwa hiyo Farao akawaambia watumishi wake: “Je, kweli kuna mwanamume mwingine anayeweza kupatikana kama huyu aliye na roho ya Mungu?” 39  Kisha Farao akamwambia Yosefu: “Kwa kuwa Mungu amekuwezesha kuyajua yote hayo, hakuna yeyote aliye na busara na hekima kama wewe. 40  Wewe binafsi utaisimamia nyumba yangu, na watu wangu wote watakutii kabisa.+ Nitakuwa tu mkuu kuliko wewe ninapotimiza jukumu langu nikiwa mfalme.”* 41  Kisha Farao akamwambia Yosefu: “Tazama, ninakuweka kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri.”+ 42  Halafu Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kwenye mkono wake mwenyewe na kumvisha Yosefu mkononi, akamvisha pia mavazi ya kitani bora na mkufu wa dhahabu shingoni mwake. 43  Zaidi ya hayo, akampandisha katika gari lake la pili la heshima, na watu walikuwa wakimtangulia na kusema kwa sauti, “Avrekh!”* Kwa hiyo Farao akamweka kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri. 44  Tena Farao akamwambia Yosefu: “Mimi ni Farao, lakini hakuna mtu anayepaswa kufanya jambo lolote* bila idhini yako katika nchi yote ya Misri.”+ 45  Kisha Farao akampa Yosefu jina Zafenath-panea, na pia akampa Asenathi+ binti ya Potifera kuhani wa Oni* awe mke wake. Naye Yosefu akaanza kuisimamia* nchi ya Misri.+ 46  Yosefu alikuwa na umri wa miaka 30+ alipoanza kumtumikia* Farao mfalme wa Misri. Kisha Yosefu akaondoka mbele ya Farao na kutembea katika nchi yote ya Misri. 47  Na katika miaka saba ya chakula kingi, nchi ilizaa chakula kingi sana. 48  Naye aliendelea kukusanya chakula chote cha miaka saba katika nchi ya Misri, akakiweka katika maghala majijini. Katika kila jiji alikusanya chakula kutoka katika mashamba yaliyozunguka jiji hilo. 49  Yosefu akaendelea kukusanya nafaka nyingi sana katika maghala, kama mchanga wa bahari, hivi kwamba mwishowe wakaacha kuipima kwa sababu haingeweza kupimwa. 50  Kabla ya mwaka wa kwanza wa njaa kali, Asenathi, binti ya Potifera kuhani wa Oni* alimzalia Yosefu wana wawili.+ 51  Yosefu alimwita mzaliwa wa kwanza Manase,*+ kwa maana alisema, “Mungu amenifanya nisahau taabu yangu yote na nyumba yote ya baba yangu.” 52  Akamwita yule wa pili Efraimu,*+ kwa maana alisema, “Mungu ameniwezesha kuzaa watoto katika nchi ya mateso yangu.”+ 53  Hatimaye miaka saba ya chakula kingi katika nchi ya Misri ikaisha,+ 54  na miaka saba ya njaa kali ikaanza, kama Yosefu alivyokuwa amesema.+ Njaa hiyo ilienea katika nchi zote, lakini kulikuwa na chakula* katika nchi yote ya Misri.+ 55  Mwishowe, nchi yote ya Misri ikakumbwa na njaa hiyo kali, watu wakaanza kumlilia Farao awape chakula.*+ Basi Farao akawaambia Wamisri wote: “Nendeni kwa Yosefu, na mfanye lolote atakalowaambia.”+ 56  Njaa hiyo ikaenea duniani pote.+ Ndipo Yosefu akaanza kuyafungua maghala yote ya nafaka yaliyokuwa katika majiji yao na kuwauzia Wamisri chakula,+ kwani njaa hiyo ilikuwa imeilemea sana nchi ya Misri. 57  Isitoshe, watu kutoka kila mahali duniani wakaja Misri kununua chakula kutoka kwa Yosefu, kwa sababu njaa hiyo ilikuwa imeilemea sana dunia yote.+

Maelezo ya Chini

Au “fasiri yake.”
Au “alivyotufasiria.”
Tnn., “ndani ya tangi la maji; shimoni.”
Au “inapohusu tu kiti cha ufalme.”
Inaonekana ni neno linalowaamuru watu waonyeshe heshima na staha.
Tnn., “kuinua mkono wake au mguu wake.”
Yaani, Heliopolisi.
Au “kutembea kotekote katika.”
Tnn., “aliposimama mbele ya.”
Au “Heliopolisi.”
Maana yake “Anayesahaulisha; Anayemfanya Mwingine Asahau.”
Maana yake “Anayezaa Maradufu.”
Au “mkate.”
Au “mkate.”