Mwanzo 47:1-31

  • Yakobo akutana na Farao (1-12)

  • Usimamizi wenye hekima wa Yosefu (13-26)

  • Israeli aishi Gosheni (27-31)

47  Basi Yosefu akaenda na kumwambia Farao:+ “Baba yangu na ndugu zangu wamekuja kutoka katika nchi ya Kanaani wakiwa na kondoo wao na ng’ombe wao na mali zao zote, wako katika nchi ya Gosheni.”+  Yosefu akachukua watano kati ya ndugu zake na kuwaleta mbele ya Farao.+  Farao akawauliza ndugu zake: “Mnafanya kazi gani?” Wakamjibu: “Sisi watumishi wako ni wafugaji wa kondoo, sisi na mababu zetu.”+  Kisha wakamwambia Farao: “Sisi watumishi wako tumekuja kuishi nchini kama wageni+ kwa sababu hakuna malisho kwa ajili ya mifugo yetu, kwa kuwa njaa ni kali sana katika nchi ya Kanaani.+ Basi tafadhali turuhusu sisi watumishi wako tuishi katika nchi ya Gosheni.”+  Ndipo Farao akamwambia Yosefu: “Baba yako na ndugu zako wamekuja hapa kwako.  Nchi ya Misri iko mbele yako. Wape baba yako na ndugu zako sehemu bora kabisa ya nchi+ ili waishi humo. Waache waishi katika nchi ya Gosheni, na ikiwa unajua wanaume wowote wenye ustadi miongoni mwao, waweke wasimamie mifugo yangu.”  Kisha Yosefu akamleta Yakobo baba yake na kumpeleka mbele ya Farao, naye Yakobo akambariki Farao.  Farao akamuuliza Yakobo: “Una umri gani?”  Yakobo akamwambia Farao: “Nimekuwa nikitangatanga* kwa miaka 130. Miaka yangu imekuwa michache na yenye taabu,+ nayo si mingi kama miaka ambayo mababu zangu waliishi walipokuwa wakitangatanga.”*+ 10  Kisha Yakobo akambariki Farao na kutoka mbele yake. 11  Basi Yosefu akawapa makao baba yake na ndugu zake, aliwapa miliki katika nchi ya Misri, katika sehemu bora kabisa ya nchi, katika eneo la Ramesesi,+ kama Farao alivyoamuru. 12  Na Yosefu akaendelea kumpa chakula* baba yake na ndugu zake na watu wote wa nyumba ya baba yake, kulingana na idadi ya watoto wao. 13  Sasa nchi yote haikuwa na chakula* kwa sababu njaa ilikuwa kali sana, basi watu wakadhoofika katika nchi ya Misri na nchi ya Kanaani kwa sababu ya njaa hiyo.+ 14  Yosefu alikuwa akikusanya pesa zote katika nchi ya Misri na nchi ya Kanaani, pesa za nafaka iliyonunuliwa na watu,+ naye alikuwa akizipeleka katika nyumba ya Farao. 15  Hatimaye watu wa nchi ya Misri na nchi ya Kanaani wakaishiwa na pesa, na Wamisri wote wakaanza kwenda kwa Yosefu na kumwambia: “Tupe chakula! Kwa nini tufe ukituangalia kwa kuwa pesa zetu zimekwisha?” 16  Yosefu akawaambia: “Ikiwa pesa zenu zimekwisha, leteni mifugo yenu, nami nitawapa chakula na kuchukua mifugo yenu.” 17  Basi wakaanza kumletea Yosefu mifugo yao, naye alikuwa akiwapa chakula na kuchukua farasi wao, mifugo yao, na punda wao, na mwaka huo wote alikuwa akiwapa chakula na kuchukua mifugo yao yote. 18  Mwaka huo ulipokwisha, walianza kumjia mwaka uliofuata wakisema: “Hatutakuficha bwana wetu kwamba tumekupa pesa zetu zote na mifugo yetu yote. Hatuna chochote kilichobaki cha kukupa bwana wetu isipokuwa miili yetu na ardhi yetu. 19  Kwa nini tufe ukituangalia, sisi na ardhi yetu? Tununue sisi pamoja na ardhi yetu tupate chakula, nasi pamoja na ardhi yetu tutakuwa watumwa wa Farao. Tupe mbegu ili tuendelee kuishi, tusife, na ardhi yetu isibaki ukiwa.” 20  Basi Yosefu akamnunulia Farao ardhi yote ya Wamisri, kwa sababu kila Mmisri aliuza ardhi yake, kwa maana njaa ilikuwa kali sana; ardhi ikawa mali ya Farao. 21  Kisha akawahamisha watu na kuwapeleka majijini, kutoka mwisho mmoja wa nchi ya Misri mpaka mwisho mwingine.+ 22  Ila tu hakununua ardhi ya makuhani,+ kwa sababu makuhani walipata posho ya chakula kutoka kwa Farao, nao waliishi kwa kutegemea posho waliyopewa na Farao. Ndiyo sababu hawakuuza ardhi yao. 23  Kisha Yosefu akawaambia watu: “Tazameni, leo nimewanunua ninyi na ardhi yenu kuwa mali ya Farao. Hapa pana mbegu kwa ajili yenu, zipandeni mashambani. 24  Mtakapopata mavuno, mpeni Farao sehemu ya tano ya mavuno hayo,+ lakini sehemu nne zitakuwa zenu; zitakuwa mbegu za kupanda shambani na chakula chenu na cha watu wa nyumbani mwenu na cha watoto wenu.” 25  Basi wakamwambia: “Umeokoa uhai wetu.+ Na tupate kibali machoni pako bwana wetu, nasi tutakuwa watumwa wa Farao.”+ 26  Kisha Yosefu akaifanya hiyo kuwa sheria ambayo ingali inafanya kazi nchini Misri hadi leo, kwamba sehemu ya tano ya mavuno ni ya Farao. Ni ardhi ya makuhani tu ambayo haikununuliwa na Farao.+ 27  Waisraeli wakaendelea kuishi Misri, katika nchi ya Gosheni,+ wakakaa humo, nao wakaongezeka na kuwa wengi sana.+ 28  Na Yakobo akaendelea kuishi katika nchi ya Misri kwa miaka 17, kwa hiyo siku zote za maisha ya Yakobo zilikuwa miaka 147.+ 29  Wakati wa Israeli kufa ulikuwa ukikaribia,+ kwa hiyo akamwita Yosefu mwanawe na kumwambia: “Ikiwa sasa nimepata kibali machoni pako, tafadhali, weka mkono wako chini ya paja langu, na unitendee kwa upendo mshikamanifu na uaminifu. Tafadhali, usinizike Misri.+ 30  Nitakapokufa,* unapaswa kunibeba na kunitoa Misri na kunizika katika kaburi la mababu zangu.”+ Basi Yosefu akasema: “Nitafanya tu kama unavyosema.” 31  Kisha Yakobo akasema: “Niapie.” Basi akamwapia.+ Ndipo Israeli akainama upande wa kichwa cha kitanda chake.+

Maelezo ya Chini

Au “nikihamahama; nikikaa kama mgeni.”
Au “wakihamahama; wakikaa kama wageni.”
Tnn., “mkate.”
Tnn., “mkate.”
Tnn., “Nitakapolala na baba zangu.”