Wimbo wa Sulemani 5:1-16

  • Mchungaji (1a)

  • Wanawake wa Yerusalemu (1b)

    • ‘Leweni mapenzi!’

  • Msichana (2-8)

    • Asimulia ndoto yake

  • Mabinti wa Yerusalemu (9)

    • “Mpenzi wako ni bora kuliko wapenzi wengine wote jinsi gani?”

  • Msichana (10-16)

    • “Anavutia zaidi miongoni mwa wanaume elfu kumi” (10)

5  “Nimeingia katika bustani yangu,+Ewe dada yangu, bibi harusi wangu. Nimekusanya manemane yangu na viungo* vyangu.+ Nimekula sega langu na asali yangu;Nimekunywa divai yangu na maziwa yangu.”+ “Kuleni, rafiki zangu wapendwa! Kunyweni, mlewe maonyesho ya upendo!”+   “Nimelala usingizi, lakini moyo wangu uko macho.+ Ndiyo hiyo sauti ya mpenzi wangu akipiga hodi!” “Nifungulie, ewe dada yangu, mpenzi wangu,Njiwa wangu, mpenzi wangu asiye na kasoro! Kwa maana kichwa changu kimelowa umande,Mashungi ya nywele zangu yamejaa unyevu wa usiku.”+   “‘Nimevua kanzu yangu. Ni lazima niivae tena? Nimeosha miguu yangu. Ni lazima niichafue tena?’   Mpenzi wangu aliondoa mkono wake kwenye tundu la mlango,Hisia zangu kumwelekea zikasisimka.   Niliinuka ili nimfungulie mpenzi wangu;Mikono yangu ikadondosha manemane,Na vidole vyangu manemane ya maji,Ikadondoka kwenye vitasa vya mlango.   Nilimfungulia mpenzi wangu,Lakini mpenzi wangu alikuwa ameondoka, alikuwa ameenda zake. Nilitamauka* alipoenda. Nilimtafuta, lakini sikumpata.+ Nikamwita, lakini hakuitika.   Nilikutana na walinzi waliokuwa wakizunguka jijini. Wakanipiga na kunijeruhi. Walinzi wa kuta wakanivua mtandio wangu.*   Nawaapisha, enyi binti za Yerusalemu: Mkimpata mpenzi wangu,Mwambieni naugua kwa mapenzi.”   “Mpenzi wako ni bora kuliko wapenzi wengine wote jinsi gani,Ewe mwanamke mrembo kuliko wote? Mpenzi wako ni bora kuliko mpenzi mwingine yeyote jinsi gani,Hivi kwamba unatuapisha hivyo?” 10  “Mpenzi wangu anang’aa tena ni mwekundu;Anavutia zaidi miongoni mwa wanaume elfu kumi. 11  Kichwa chake ni dhahabu, dhahabu bora zaidi. Mashungi ya nywele zake ni kama majani ya mtende yanayotikisika.* Nywele zake ni nyeusi kama kunguru. 12  Macho yake ni kama njiwa kando ya vijito vya maji,Wanaooga ndani ya maziwa,Wakiwa wameketi kando ya dimbwi lililojaa maji. 13  Mashavu yake ni kama kitalu cha viungo,+Vilima vya mimea yenye manukato. Midomo yake ni mayungiyungi, yanayodondosha manemane ya maji.+ 14  Mikono yake ni fito za dhahabu, zilizopambwa kwa krisolito. Tumbo lake ni pembe ya tembo iliyong’arishwa na kufunikwa kwa yakuti. 15  Miguu yake ni nguzo za marumaru zilizowekwa kwenye vikalio vya dhahabu bora zaidi. Sura yake ni kama Lebanoni, kama mierezi isiyo na kifani.+ 16  Kinywa chake* ni utamu mtupu,Na kila kitu kumhusu kinatamanika.+ Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye mpendwa wangu, enyi binti za Yerusalemu.”

Maelezo ya Chini

Yaani, vikolezo.
Au “Nafsi yangu ilizimia.”
Au “shela yangu.”
Au labda, “vishada vya tende.”
Tnn., “Kaakaa lake.”