Yeremia 40:1-16

  • Nebuzaradani amwachilia huru Yeremia (1-6)

  • Gedalia awekwa kuwa msimamizi nchini (7-12)

  • Njama dhidi ya Gedalia (13-16)

40  Neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Yehova baada ya Nebuzaradani+ mkuu wa walinzi kumwachilia huru kutoka Rama.+ Alikuwa amempeleka huko akiwa amefungwa pingu mikononi, naye alikuwa miongoni mwa watu wote waliohamishwa kutoka Yerusalemu na Yuda waliokuwa wakipelekwa uhamishoni Babiloni.  Kisha mkuu wa walinzi akamchukua Yeremia na kumwambia: “Yehova Mungu wako alitabiri msiba huu dhidi ya mahali hapa,  na Yehova ameuleta msiba huo kama alivyosema, kwa sababu ninyi watu mlimtendea dhambi Yehova na hamkuitii sauti yake. Ndiyo sababu jambo hili limewapata.+  Sasa ninakufungua pingu zilizo mikononi mwako. Ikiwa unaona ni vema kwako kwenda pamoja nami Babiloni, njoo, nami nitakutunza. Lakini ikiwa hutaki kwenda pamoja nami Babiloni, usije. Angalia! Nchi nzima iko mbele yako. Nenda popote unapotaka.”+  Hata kabla Yeremia hajageuka kuondoka, Nebuzaradani akamwambia: “Rudi kwa Gedalia+ mwana wa Ahikamu+ mwana wa Shafani,+ ambaye mfalme wa Babiloni amemweka juu ya majiji ya Yuda, nawe ukae pamoja naye miongoni mwa watu; au uende popote unapotaka.” Ndipo mkuu wa walinzi akampa posho ya chakula na zawadi, akamruhusu aende zake.  Basi Yeremia akaenda kwa Gedalia mwana wa Ahikamu kule Mispa+ na kukaa pamoja naye miongoni mwa watu waliobaki nchini.  Baadaye wakuu wote wa majeshi waliokuwa uwanjani pamoja na watu wao wakasikia kwamba mfalme wa Babiloni amemweka Gedalia mwana wa Ahikamu awe msimamizi wa nchi na kwamba alikuwa amemweka awe msimamizi wa wanaume, wanawake, na watoto, watu maskini nchini ambao hawakuwa wamepelekwa uhamishoni Babiloni.+  Basi wakaenda kwa Gedalia huko Mispa.+ Wakuu hao ni Ishmaeli+ mwana wa Nethania, Yohanani+ na Yonathani wana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi, wana wa Efai Mnetofa, na Yezania+ mwana wa Mmaakathi, pamoja na wanajeshi wao.  Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani akawaapia wao pamoja na wanajeshi wao, akisema: “Msiogope kuwatumikia Wakaldayo. Kaeni katika nchi hii na kumtumikia mfalme wa Babiloni, na mambo yatawaendea vema.+ 10  Lakini mimi, nitakaa Mispa, ili niwawakilishe kwa* Wakaldayo watakaokuja kwetu. Lakini ninyi mnapaswa kukusanya divai, matunda ya wakati wa kiangazi, na mafuta na kuviweka vitu hivyo katika vyombo vyenu vya kuhifadhia na mkae katika majiji mliyoyachukua.”+ 11  Na Wayahudi wote waliokuwa Moabu, Amoni, na Edomu, na wale waliokuwa katika nchi nyingine zote, wakasikia pia kwamba mfalme wa Babiloni alikuwa amewaacha watu fulani wabaki Yuda na kwamba alikuwa amemweka Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani awe msimamizi wao. 12  Basi Wayahudi wote wakaanza kurudi kutoka kila mahali ambako walikuwa wametawanywa, nao wakaja katika nchi ya Yuda, kwa Gedalia huko Mispa. Nao wakakusanya divai na matunda ya wakati wa kiangazi kwa wingi sana. 13  Yohanani mwana wa Karea na wakuu wote wa jeshi waliokuwa uwanjani wakaja kwa Gedalia huko Mispa. 14  Wakamwambia: “Je, hujui kwamba Baalisi mfalme wa Waamoni,+ amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania akuue?”*+ Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu hakuwaamini. 15  Kisha Yohanani mwana wa Karea akamwambia kisiri Gedalia huko Mispa: “Ninataka kwenda kumuua Ishmaeli mwana wa Nethania, na hakuna mtu atakayejua. Kwa nini akuue,* na kwa nini watu wote wa Yuda waliokusanyika kwako watawanyike na watu wa Yuda waliobaki waangamie?” 16  Lakini Gedalia+ mwana wa Ahikamu akamwambia Yohanani mwana wa Karea: “Usifanye hivyo, kwa maana unasema uwongo kumhusu Ishmaeli.”

Maelezo ya Chini

Tnn., “nisimame mbele ya.”
Au “aiue nafsi yako.”
Au “aiue nafsi yako.”