Zaburi 64:1-10
-
Ulinzi dhidi ya mashambulizi yaliyofichika
-
“Mungu atawapiga mishale” (7)
-
Kwa kiongozi. Muziki wa Daudi.
64 Ee Mungu, sikia sauti yangu ninapokusihi.+
Ulinde uhai wangu kutokana na hofu ya adui.
2 Nikinge kutokana na njama za siri za waovu,+Kutoka kwa umati wa watenda maovu.
3 Wanaunoa ulimi wao kama upanga;Wanayalenga maneno yao ya ukatili kama mishale,
4 Ili wampige mtu asiye na hatia wakiwa mafichoni;Wanampiga ghafla, bila kuogopa.
5 Wanashikamana sana na kusudi lao ovu;*Wanazungumzia jinsi ya kuficha mitego yao.
Wanasema: “Ni nani atakayeiona?”+
6 Wanatafuta njia mpya za kutenda uovu;Wanatunga kwa siri mbinu zao za ujanja;+Fikira zilizo ndani ya moyo wa kila mmoja wao hazieleweki kamwe.
7 Lakini Mungu atawapiga mishale;+Watajeruhiwa kwa ghafla na mshale.
8 Ulimi wao wenyewe utasababisha waanguke;+Wote wanaowatazama watatikisa kichwa.
9 Ndipo watu wote wataogopa,Nao watatangaza mambo ambayo Mungu ametenda,Nao watayafahamu matendo yake.+
10 Mwadilifu atashangilia kwa sababu ya Yehova na kumkimbilia;+Wote walio wanyoofu moyoni watashangilia.*